Dodoma. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetangaza ajira 5,410 kwa vikosi vyake vya Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto.
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alipokuwa akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Pamoja na ajira hizo, Waziri Lugola alitaja vipaumbele vingine vya wizara yake kuwa ni ujenzi wa majengo ya askari, maboresho ya vyuo vya polisi, vitendea kazi kwa vikosi vya Uhamiaji, Magereza, Polisi na Zimamoto.
“Vipaumbele vingine ni kuendelea kutekeleza mkakati wa Jeshi la Magereza na kujitosheleza kwa chakula, kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu kwa kuimarisha utendaji wa shirika la uzalishaji la magereza na kununua magari na vifaa vya kuzimia moto na kuongeza kasi ya utoaji wa Vitambulisho vya Taifa,” alisema Lugola.
Alisema vipaumbele hivyo vimezingatia maagizo ya Rais John Magufuli kwa nyakati tofauti, kuzuia ukatili dhidi ya wanawake, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2016/17 – 2020/21
Alisema hali ya usalama nchini imeendelea kuimarika licha ya kuwapo kwa matukio machache yaliyoripotiwa yakiwamo makosa makubwa 45,574 katika kipindi cha Machi 2018 hadi Machi 2019.
Ajira
Waziri Lugola alisema kwa mwaka 2019/20, Jeshi la Polisi limepanga kuajiri vijana 3,725 na kuwapandisha vyeo askari ambao wanastahili ili kuboresha utendaji kazi. Katika kipindi hicho, pia Magereza wanatarajia kutoa ajira 685 na kuwasomesha askari wake katika vyuo mbalimbali huku Zimamoto na Uhamiaji zikitengewa nafasi 500 kila mmoja.
Kuhusu magari 777 ambayo yamekuwa yakitajwa mara nyingi alisema hadi kufikia Machi 2019, wizara ilishapokea magari 497 hivyo bado 280.
Maoni ya kamati
Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mbunge wa Morogoro Kusini, Prosper Mbena alisema katika mwaka wa fedha 2019/20, Jeshi la Polisi linatarajia kukusanya Sh 118.317 bilioni kwa makosa ya ukiukwaji wa usalama barabarani akisema hilo ni kadirio la jumla ya makosa 3.1 milioni ambayo linalenga kuyakamata kwa vyombo vya moto barabarani.
Hata hivyo, alilitaka jeshi hilo kujikita zaidi katika kutoa elimu badala ya kutegemea makosa kama vyanzo vya mapato akiitaka Serikali kukamilisha mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani ili kusaidia kupunguza makosa ambayo yanasababisha ajali.
Alisema kazi mojawapo kwa Jeshi la Polisi ni kutoa elimu kabla ya kutoza faini kwa wakosaji ili waanze kwa kupunguza makosa yao.
Matukio ya utekaji
Waziri alisema kumeibuka uhalifu mpya wa utekaji watoto katika mikoa ya Njombe na Simiyu. Alisema Njombe watoto sita waliuawa na watatu walitekwa na polisi ilifanikiwa kuwapata watatu wakiwa hai.
“Vilevile, katika Mkoa wa Simiyu kulitokea mauaji ya watoto wanne ambao waliuawa na kukatwa baadhi ya viungo na watumishi 12 walikamatwa na taarifa zilionyesha viini vya matukio hayo ni imani za kishirikina,” alisema
Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, jumla ya matukio 2,593 yaliripotiwa ikiwa ni pungufu ya matukio 1,587 ambayo ni asilimia 38 ya matukio 4,180 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho 2017/18.
Matukio hayo yalisababisha vifo 1,216 ikilinganishwa na vifo 1,985 vilivyotokea mwaka 2017/18 ambayo ni pungufu ya vifo 769 sawa na asilimia 38.7 huku idadi ya majeruhi ikipungua kwa asilimia 40.7 kutoka majeruhi 4,447 hadi 2,639.
Kuhusu ajali, alisema jeshi la polisi lilifanya ukaguzi kwa mabasi 247,514 na 26,219 yaligundulika kuwa mabovu na hayaruhusiwi kuendelea na safari huku madereva 72 wa mabasi ya abiria wakifungiwa leseni baada ya kufikishwa mahakamani.
“Katika kipindi hicho jumla ya madereva 7,271 walifikishwa mahakamani wakiwamo madereva wa magari 1,436 na waendesha pikipiki 5,835. Lakini madereva wengine 95,081 walipewa adhabu ya kulipa faini kwa kukiuka sheria ya usalama barabarani,” alisema Lugola .
#Duniayako
Comments
Post a Comment