Dodoma. Si unajua kuwa Niabu Spika, Dk Tulia Ackson ameambatana na Rais John Magufuli katika ziara yake mkoani Mbeya wakati vikao vya chombo hicho cha kutunga sheria vikiendelea, sasa jambo hilo limetolewa ufafanuzi bungeni leo Jumanne Aprili 30, 2019.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu amesema leo bungeni jijini Dodoma kuwa suala hilo linamhusu Spika, Job Ndugai.
Zungu alitoa kauli hiyo akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.
Msigwa alitaka kujua kwa nini Dk Tulia amekacha vikao vya Bunge la bajeti badala yake, anaonekana kwenye ziara ya Rais huku akijua Serikali ina mihimili mitatu inayojitegemea.
Rais ataka viongozi kuacha marumbano ya siri siri
"Naomba mwongozo wako mwenyekiti. Alipoteuliwa Dk Tulia aliapa kuwa ni mbunge wa Kinondoni na ameshashiriki uchaguzi na shughuli nyingine za halmashauri hiyo. Kwenye ziara ya Rais anafanya nini?" amehoji Msigwa.
Akijibu mwongozo huo, Zungu amesema Dk Tulia ni mteule wa Rais ambaye anaweza akaitwa wakati wowote na mamlaka za juu.
Hata hivyo, amesisitiza uwapo au kutokuwapo kwa naibu spika huyo bungeni si suala linalomhusu kila mbunge.
"Anayepaswa kujua ni Spika, si mimi wala wewe," amesema Zungu.
Comments
Post a Comment