IRAN YAFIKIRIA KUJITTOA KWENYE MKATABA WA KUTOENEZA SILAHA ZA NYUKLIA HUKU MAREKANI IKIZIPA ONYO LA MWISHO NCHI ZINAZOFANYA BIASHARA NA IRAN MWISHO MEI MOSI 2019.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Bw.Mohammad Javad Zarif amesema nchi yake inafikiria hatua mbalimbali za kujibu uamuzi wa Marekani kurejesha vikwazo dhidi ya Iran,ikiwemo hatua ya kujitoa kwenye Mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia.
Baada ya kujitoa kwenye Makubaliano ya nyuklia ya Iran mwaka 2015,mwezi Novemba mwaka jana serikali ya Marekani ilirejesha vikwazo dhidi ya sekta za benki,nishati na uchukuzi za Iran,na kuwapa nchi wanunuzi wakubwa wa mafuta ya Iran muda wa miezi sita kuacha kununua mafuta kutoka nchi hiyo.
Wiki iliyopita,Marekani ilitangaza kumalizika kwa muda wa mpito na kuzitaka nchi hizo kutonunua tena mafuta kutoka Iran kabla ya mwezi Mei.
Uamuzi wa serikali ya Marekani wa kuziwekea vikwazo nchi zinazonunua mafuta kutoka Iran umeibua wasiwasi kuhusu usambazaji wa kimataifa wa mafuta ghafi,huku bei ya mafuta ikiwa imepanda kwa kiasi kikubwa.
Wiki moja iliyopita ,Marekani ilizitaka nchi zinazonunua mafuta kutoka Iran zisite kufanya hivyo kuanzia Mei 1,au zitakabiliwa na vikwazo vikali.Uamuzi huo utamaliza muda wa miezi sita ambapo nchi nane nyingi kutoka bara la Asia,ziliruhusiwa kununua mafuta hayo kutoka Iran.
Wataalamu wa sekta hiyo wamesema kuwa vikwazo hivyo vinaweza kupelekea kupungua kwa hadi mapipa milioni 1.2 ya mafuta katika soko la Kimataifa.
Idadi hiyo inaweza ikawa ndogo zaidi kulingana na jinsi nchi zitakavyoupokea uamuzi huo wa Marekani,na kiasi cha mafuta ambacho Iran itaenedelea kusafirisha.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema anataka kusambaratisha mapato ya Iran yanayotokana an mauzo ya mafuta.Trump anaamini fedha hizo zinatumiwa na Iran kufadhili shughuli za uharibifu katika Mashariki ya Kati na kwengineko.
Uamuzi huo unamaanisha ruhusa ya kununua mafuta kutoka Iran haitoongezwa muda wake utakapomalizika Mei 2 kwa mataifa matano tofauti,China na India pamoja na washirika wa Marekani Japan,Korea Kusini na Uturuki.
Lakini wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu ameikosoa hatua hiyo ya Marekani ya kuziwekea vikwazo nchi zinazonunua mafuta kutoka Iran, akisema itahatarisha utulivu wa eneo zima.
"Kisiasa sio uamuzi sahihi.Kimaadili sio haki.Kwa mtazamo wa kibiashara,pia sio sawa.Na pia ni kinyume na sheria ya kimataifa ya biashara,na ni kinyume na sheria za Shirika la Biashara Duniani na ni hatari kwa kanda nzima Nani atakaefaidika? Badala yake bei ya mafuta itaongezeka katika nchi zinazoshirikiana kwa karibu na Marekani.Uamuzi huu haujawahi kushuhudiwa duniani hadi sasa," amesema Mevlut Cavusoglu,Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki.
Waziri wa Mafuta ya Petroli na Gesi asilia wa India Dharmendra Pradhan,amesema kuwa nchini hiyo itatumiwa mafuta ya ziada kutoka nchi nyingine zinazochimba mafuta ili kufidia pengo litakalojitokeza kwa kukosa mafuta ya Iran.
Saudi Arabia,msafirishaji mkubwa wa mafuta duniani,imesema kwamba itashirikiana na nchi nyingine zinazochimba mafuta kuhakikisha kuna usambazaji wa kutosha wa mafuta ghafi katika soko la Kimataifa.
Comments
Post a Comment