Mtanzania atwaa medali Ujerumani


   
Ushindi wa medali ya shaba ya mwanariadha, Failuna Abdi kwenye mbio za Haspa Hamburg Marathoni jana Jumapili umempa tiketi ya kufuzu kushiriki Olimpiki ya 2020.


Mbali na Olimpiki, mwanariadha huyo ameweza kuvunja rekodi yake ya marathoni kwa kukimbia muda bora zaidi na kutwaa medali ya shaba.

Failuna aling’ara katika mbio hizo za fedha zilizofanyika nchini Ujerumani.

Katika mbio hizo, Failuna alikimbia kwa saa 2:27:56 akiwa ameachwa kwa dakika 3:14 na mshindi wa medali ya dhahabu raia wa Ethiopia, Dibabe.

Dibabe alitumia saa 2:24:42 kumaliza mbio hizo na kutwaa medali ya dhahabu wakati Magdalyne Masai wa Kenya alimaliza wa pili akikimbia kwa saa 2:26:04.

“Zilikuwa mbio za ushindani, nilitamani kushinda medali ya dhahabu, lakini nilipitwa dakika za mwishoni ila nimefarijika kuvunja rekodi ya muda wangu,” alisema Failuna jana kwa simu muda mfupi baada ya kumaliza mbio hizo.

Kocha wa Failuna ambaye yuko naye Ujerumani, Thomas Tlanka alisema, Failuna amebebwa na mazoezi, jitihada na kujiamini.

“Mbio zilikuwa na ushindani, lakini tuliweka mikakati ya ushindi, alianza vizuri hadi mwishoni ambako mshindi alimpita dakika za mwisho, lakini tumefanikiwa kutwaa shaba,” alisema Tlanka.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelim Gidabuday alisema matokeo ya Failuna mbali na kutwaa medali, lakini pia yamempa rekodi ya muda mzuri zaidi kwenye mbio za dunia za Septemba nchini Qatar.

   

Comments