MWINGINE ADAIWA KUFIA MIKONONI MWA POLISI

MWINGINE ADAIWA KUFIA MIKONONI MWA POLISI.

Moshi/Mwanga. Matukio ya watuhumiwa kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi yanaendelea kulitikisa jeshi hilo la polisi baada ya kijana aitwaye Waziri Mlacha (18), kudaiwa kuuawa akiwa mikononi mwa askari wa jeshi hilo.


Tukio hilo limegubikwa na utata wa mahali hasa alipofia kijana huyo mkazi wa Lembeni, Mwanga kwani wakati polisi wakidai alifia hospitalini, ndugu wamedai kuwa alifia Kituo cha Polisi Kisangara.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson amedai kuwa purukushani kwenye kituo cha polisi kulimfanya kijana huyo aliyekuwa dereva wa bodaboda kuanguka kwa kifafa.

Ndugu wamedai kuwa marehemu aliuawa kwa kipigo cha polisi katika kituo hicho kwani mwili wake una majeraha maeneo mbalimbali yanayoashiria alipigwa.

Baba mlezi wa kijana huyo, Abdu Miaya alisema taarifa kuwa mtoto wao alikuwa na kifafa si za kweli na kwamba tangu alipomchukua akiwa na miaka saba, hajawahi kuumwa ugonjwa huo.


Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema jana kuwa wanamshikilia askari mmoja ili asaidie uchunguzi wa kilichotokea hadi mtuhumiwa huyo kufariki dunia.

Hata hivyo, alisema, “niko Mwanga kwa sasa na sio kwamba amefia mikononi mwa polisi kama mnavyosema, ni kwamba alikamatwa na alipofikishwa kituoni hali yake ilibadilika na alifariki wakati akipelekwa hospitali.”

Inadaiwa kuwa marehemu alikamatwa na polisi ili aeleze mahali alipo rafiki yake aliyekuwa akitafutwa kwa kosa ambalo halikuelezwa na aliwaeleza askari kuwa hafahamu mahali alipo na kwamba hicho ndicho kiini cha kipigo.

Kauli ya DC Mwanga

Katika maelezo yake, mkuu wa wilaya hiyo, alidai kuwa marehemu na mwenzake ambaye hakumtaja jina walikuwa wakitafutwa na polisi kwa tuhuma za shambulio na kumdhuru kijana mwingine.

Alisema kijana huyo alikamatwa na polisi mmoja wa upelelezi mwenye cheo cha koplo na kumpeleka kituo cha polisi, lakini aligoma kuingia chumba cha mahabusu.

“Alipofikishwa kituoni alighairi kuingia mahabusu ndipo palipotokea purukushani na kijana huyo baadaye alizimia na kupelekwa kituo cha Afya Mungare na kufariki dunia,” alisema Apson.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe alisema limemsikitisha kwa kuwa mpigakura wake huyo alikamatwa mchana kweupe akiwa mzima.

“Ni tukio baya, linasikitisha na linaumiza sana. Ni wiki iliyopita tu mtoto mdogo ameuawa kwa kukatwa mapanga na leo kijana mdogo wa miaka 18 anakufa,” alisema.

Mmoja wa majirani wa kijana huyo, Lemburusi Mchome alisema juzi kijana huyo alipokamatwa, walifanya jitihada za kumtoa ikashindikana mpaka walipoletewa taarifa za kifo chake.

Mwili wa kijana huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ukisubiri uchunguzi wa madaktari ili kubaini sababu za kifo chake.

Tukio jingine

Septemba mwaka jana, polisi mkoani Kilimanjaro, walituhumiwa kumpiga dereva wa daladala, mkazi wa Kiborlon, Andrew Kiwia (39), lakini wakadai alijinyonga akiwa mahabusu.

Ndugu waligoma kuchukua mwili wakimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola afike. Walikubali kumzika baada uchunguzi wa kifo hicho.
#Duniayako

Comments