TANZANIA YASHUKA NAFASI 25 UHURU WA HABARI DUNIANI




SHIRIKA la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF), limetoa ripoti yake mpya ikionesha Tanzania imeporomoka kwa nafasi 25 katika orodha ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Katika ripoti hiyo ya dunia, ikizungumzia namna mabadiliko ya utawala yanavyoweza kuleta maendeleo ya uhuru wa habari barani Afrika, RSF iliitolea mfano Ethiopia, tangu ujio wa Waziri Mkuu mpya, Abiy Ahmed.

Mbali ya Ethiopia, iliyopanda kwa nafasi 40 na kushika nafasi ya 110, mataifa mengine yaliyopata tawala mpya na kuendelea kuimarika ni pamoja na Gambia na Angola.

“Hata hivyo, mabadiliko ya utawala hayaonekani kuwa chanzo cha kupanda kwa uhuru wa vyombo vya habari, Tanzania ikiwa mfano mbaya.

“Tangu ujio wa Serikali ya Awamu ya Tano mwaka 2015, Tanzania imeshuhudia mashambulizi dhidi ya wanahabari, vyombo vya habari kufungiwa na sheria kandamizi kwa wanahabari na vyombo vya habari zikipitishwa,” ilieleza ripoti hiyo.


Aidha, ripoti hiyo imekosoa kitendo cha kutetea mmoja wa wakuu wa mikoa aliyevamia chombo cha habari binafsi akisindikizwa na polisi Machi 2017.

“Kwa kufungia vyombo vya habari mara nyingi kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kuvinyima vyombo vya habari binafsi matangazo kunajenga mazingira ya woga na hofu,” ilisema.

Aidha, ripoti hiyo ilikosoa sheria mpya inayotaka wamiliki wa tovuti na blogu kulipa ada kubwa pamoja na kupata kibali kutoka mamlaka husika.

RSF imelaumu pia kukamatwa kwa watetezi wawili wa uhuru wa habari, waliotimuliwa mwishoni mwa mwaka 2018, wakati wakishughulikia moja ya kesi, ikiwamo ya kupotea kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea, Azory Gwanda.

Kutokana na mwenendo huo, Tanzania imeshuka kwa nafasi 25 hadi nafasi ya 118 ya orodha hiyo.

Wakati ripoti hiyo ikionyesha hivyo, mapema wiki hii Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi, aliliambia Bunge jinsi nchi za nje zinavyoisifia Tanzania katika suala zima la uhuru wa habari.

Pamoja na hayo, gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abass, ili aweze kuzungumzia ripoti hiyo, lakini simu yake iliita pasipo kupokelewa na baadaye ilizimwa kabisa.

Kwa ujumla RSF ilisema mwenendo mbaya ulioshuhudiwa duniani, hasa chuki dhidi ya wanahabari inayochochewa na viongozi wa mirengo mikali na wa kiimla, inasababisha vurugu kote duniani.

Kwa mfano, ilisema hali ya uadui katika kauli za Rais Donald Trump dhidi ya waandishi imechangia Marekani kuporomoka hadi nafasi ya 48.

Ripoti hiyo inasema waandishi wa habari nchini humo wanakabiliwa na vitisho vingi na kukimbilia kampuni binafsi za usalama kwa ajili ya ulinzi.

Mwaka uliopita, mshambuliaji mmoja aliingia katika chumba cha habari cha gazeti la Capital katika Jimbo la Maryland na kuwaua wanahabari wanne.

Aidha, kuuawa kwa mwandishi wa habari, Jamal Khashoggi katika Ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki pia kulituma ujumbe mkali kwa wanahabari nje ya mipaka ya Saudia.

“Katika nchi nyingine, vitisho, matusi na mashambulizi vimekuwa hatari ya kazi,” imesema ripoti hiyo.

India, ambayo imeshika nafasi ya 140, ilishuhudia wanahabari sita wakiuawa mwaka jana na Brazil iliyoko namba 105 waandishi wamekuwa wakilengwa na wafuasi wa Rais wa nchi hiyo, Jair Bolsonaro.

Norway imekuwa kinara wa uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka wa tatu mfululizo, wakati Finland ikishika nafasi ya pili na Sweden nafasi ya tatu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Uturuki ni miongoni mwa nchi zilizo katika hali mbaya ya uhuru wa waandishi.

RSF pia limeorodhesha idadi ya matukio ya kukamatwa na visa vya vurugu vilivyofanywa na mamlaka ya Venezuela ambako waandishi kadhaa waliikimbia kuepuka kuadhibiwa.

Nchi ya Turkmenistan iliyoko Asia ya Kati imekamata nafasi ya mwisho na kuiondoa Korea Kaskazini.


Comments