Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeitangaza Simba itacheza mchezo wa kirafiki na Sevilla utakaopigwa Mei 23 mwaka huu.
Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu nchini Hispania inaletwa nchini mwaka huu kwa udhamini wa kampuni ya Sportpesa.
Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema awali walipokea wazo kutoka Sportpesa la kuzikutanisha timu za Simba na Yanga kisha bingwa ndio acheze na Sevilla, lakini ratiba ilikuwa inabana hivyo na kufanya uamuzi mengine.
"Wote tunajua kabisa kwamba Ligi yetu na ratiba yake jinsi hatukutaka kuharibu kalenda yetu, kwahiyo tulikaa vikao vingi sana na watu wa Sportpesa kujua tunafanyeje ili kuweza kupata timu ya kucheza mchezo huu, tuliandikiwa barua ya kuangalia namna ambavyo tunaweza kupata timu kwa kuangalia vigezo muhimu" alisema.
Kidao alisema baada ya kukaa na wadhamini wa Sportpesa waliona watumie kigezo cha Mashindano ya Sportpesa kwa timu ya Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika mashindano hayo.
"Tulikubaliana tupate timu kupitia mashindano ya wadhamini kwa sababu ndio msingi wa wadhamini, tukaja kuona kwamba ambaye anafanya vizuri ni Simba baada ya kufika hatua ya nusu fainali na wenzetu walikubaliana na sisi," alisema Kidao.
Aliongeza mechi hiyo sio bonanza kwani ni mechi ya ushindani kama ushindani wa mechi zingine ambazo zinakuwa zinafanyika.
Wakati kwa upande wa Sportpesa, Mkurugenzi wa utafiti, Udhibiti na Utawala, Abas Tarimba alisema katika uchaguzi wa timu waliumiza vichwa wakishirikiana na TFF mpaka kuja kupata timu hiyo.
"Tumetumia Vigezo vya Mashindano ya Sportpesa kupata timu, Simba wamekuwa wakifanya vizuri takribani miaka mitatu hivyo hii itafanya timu zetu kuweka uzito katika Mashindano ambayo tunayandaa kwasababu watakuwa wanapata fursa kama hizi na wachezaji kujitangaza, mechi hii itakuwa ikiangaliwa dunia nzima," alisema.
Tarimba aliongeza kwa kigezo hicho kilichotumika hata yeye kitamuokoa kwa mashabiki wa Yanga kutokana na yeye kuwa miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo.
Sevilla inatarajiwa kuwasili nchini Mei 21 na taratibu zingine zitatangazwa kuelekea katika mchezo huo.
Comments
Post a Comment