Alichokisema Zitto kuhusu Takukuru kumzuia kusafiri nje.



Unguja. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ziito Kabwe amesema uamuzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kumzuia kusafiri nje ya nchi ni wa kisiasa.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 12, 2019 katika ofisi za chama hicho zilizopo Vuga kisiwani Unguja wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kadhia iliyomkumba jana Jumanne Juni 11, 2019 baada ya kuzuiwa kwenda Kenya.

Amesema licha ya kuwa hana kosa linalohusiana na Takukuru, amedai taasisi hiyo haina mamlaka ya kutoa amri ya kusitisha safari yake.

Amebainisha kuwa kufanya hivyo ni kuingilia majukumu ya mahakama ambayo ndio yenye mamlaka ya kutoa kibali cha kumzuia mtu kusafiri nje ya nchi.

Zitto amesema Takukuru kumuingiza katika mfumo wa uhamiaji ili azuiliwe kusafiri nje ya nchi ni suala la ukiukwaji wa katiba, kwamba  katiba imesema ni mafuruku kwa mwananchi kuwekewa pingamizi la kusafiri wakati ni haki yake ya msingi.

“Hivi sasa inaonekana Takukuru kuwa ni kichaka cha kuleta usumbufu kwa viongozi wa upinzani, na ni vizuri kuacha tabia yao hiyo kwa kufanya kazi zao zinazostahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni ziliopo,” amesema Zitto.

Comments