Viongozi wawili Chadema wadaiwa watekwa


   

   
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini Tanzania (Chadema) kimedai viongozi wake wawili wamechukuliwa na watu wasiojulikana leo mchana Jumamosi Julai 6, 2019 wakiwa kwenye kikao cha ndani.


Kikao hicho kilifanyika katika kata ya Mng’aa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida. Viongozi hao ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha) jimbo la Segerea,  Agnesta Kaiza na Jumanne Rajab, mwenyekiti wa Chadema jimbo la Singida Mashariki.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Julai 6, 2019 mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene amesema viongozi hao wakiwa na wanachama wengine walikuwa kwenye kikao cha ndani ikiwa ni sehemu ya operesheni ya  ujenzi wa chama.

Amesema wakati kikao hicho kikiendelea kundi la watu wanaokadiriwa kufikia 300 walivamia kuwachukua Kaiza na Rajab.

“Walivamia nje kwanza wakamkuta dereva akakimbia wakavunja vioo vya gari na kuingia ndani wakavuruga kikao, watu wengine wakakimbia lakini wao wakawachukua viongozi hao wawili tu na kutokomea nao kusikojulikana,”

Makene ameeleza kuwa tukio hilo limetokea leo mchana.

“Tumetoa taarifa kituo cha polisi cha wilaya ya Ikungi na dereva pia amekwenda kituo cha Makihungu,” amesema Makene

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbeart Njewike alipoulizwa kuhusu madai ya kutekwa kwa viongozi hao amesema, “Hizo taarifa bado sijazipata nikipata nitawajulisha.”


Mwananchi

Comments