FAIDA YA KUWA MBALI NA MPENZI WAKO






FAIDA YA KUWA MBALI NA MPENZI WAKO.

MAMBO vipi wewe unayesoma maandishi haya sasa hivi? Acha kutabasamu bwana, sema poa! Mimi ni mzima rafiki yangu, ni imani yangu hata wewe utakuwa upo sawa na mipango mbalimbali ya maisha yako inaendelea sawa.
Nakushukuru sana kwa kuchagua kusoma blog hii, maana hujafanya uchaguzi wa makosa, utavuna vitu vingi sana na kwa hakika mapenzi hayatakupa mateso, maana utakuwa mwalimu wa walimu katika eneo hilo.

Twende kwenye mada; Watu wengi wanaamini kwamba kukaa karibu na mume/mpenzi kunaongeza zaidi mapenzi. Hii ni hoja inayoungwa mkono na wengi sana.
Aidha, nimekuwa nikipokea maswali mengi kutoka kwa wasomaji wangu wakitaka kujua mbinu za kuboresha mapenzi yao kwa wenzi ambao wanakaa nao mbali.

Hata hivyo, rafiki zangu leo nitawapa kitu kipya kichwani, wenzi wanaokaa mbalimbali, mapenzi yao hudumu na huwa matamu yaliyojaa msisimko zaidi kuliko wale ambao wanaishi eneo/nyumba moja.
Nafahamu kuna wengi ambao watapingana nami, lakini hapa nitakupa dondoo ambazo ukizipitia kwa umakini mkubwa, utaelewa maana ya ninachokiandika hapa. Kwanza twende tukaone aina za umbali kabla ya kumalizia na faida zake.


KUISHI MBALIMBALI
Hapa ni kwa pande zote, nikimaanisha kwa walio ndani ya ndoa na wale ambao wapo kwenye uchumba/urafiki. Kuna baadhi ya wapenzi wanalazimika kukaa mbalimbali kwa sababu ya kazi au majukumu mengine ya kimaisha.
Utakuta mmoja anaishi Mkoa wa Mara, mwingine yupo Dar es Salaam. Hata hivyo, utafiti unaonesha kwamba, wenzi wa aina hii hunung’unikia hali hii na wengine hufanya mipango ya haraka ya kuhamia au kumuhamishia mwenzi wake eneo ambalo anaishi. Kuna nini? Hebu angalia vijisehemu vifuatavyo:

(i) Hofu ya usaliti
Hisia za wengi ni kwamba, kukaa mbali kunaweza kuongeza usaliti. Kwamba mwenzi akiwa mbali naye, kwa sababu ana hisia za mapenzi, ni rahisi sana kuamua kukutana na mtu mwingine kwa lengo la kujiridhisha.
(ii) Hofu ya penzi kuchuja
Wengine wanaamini kwamba, kukaa mbali na mwenzi ni rahisi penzi kuchuja na baadaye kuachana kwa vile anakutana na wengine ambao eti labda wana mvuto kuliko wao na hivyo kuachwa.


UKWELI NI HUU
Kukaa mbali na mwenzi wako, kunaongeza zaidi mapenzi. Kunakuwa na hali fulani ya ‘kumisiana’ kwa muda mrefu, hivyo kukumbukana sana. Hata mnapokutana mapenzi yenu huwa na msisimko zaidi.

Suala la usaliti ni tabia ya mtu, hata kama utaishi naye sehemu moja, ukalala naye kila siku, akiamua kukusaliti atafanya hivyo, maana humfungi kamba na wala hutembei naye kila mahali.


TAFITI MWENYEWE
Naamini hata wewe ni shahidi kwamba, unaposafiri au mpenzi wako akisafiri hata kama ni wiki moja, unamkumbuka zaidi kuliko ukikaa naye. Anaporudi kila mmoja humuona mwenzake kama mpya, kumbe ni yule yule wa siku zote, isipokuwa alikuwa mbali na wewe kwa muda.
UNAISHI MBALI NA MWENZAKO?
Kama wewe upo kwenye kundi hili, usiwe na wasiwasi, unaweza kufanya penzi lako kuwa bora na imara zaidi kuliko wale wanaokaa karibu. Mweke karibu kwa mawasiliano, mtumie zawadi mara nyingi iwezekanavyo.
Mfanyie vituko vidogo vidogo na mara nyingi pendelea zaidi kuongea naye usiku. Kikubwa zaidi ni kumuweka karibu na kumfanya ahisi kama yupo nawe muda wote ingawa mnaishi mbalimbali.
NI DAWA YA MIKWARUZANO
Wanandoa wanapogombana, hasa ugomvi mkubwa unaohusisha usaliti, wengi huamua kuondoka nyumbani kwa muda, lakini wanaume wengi huwaambia wake zao waende nyumbani kwao au ukweni.

Hata katika vikao vya usuluhishi, wazee hutumia njia hii kurudisha amani katika familia. Hushauri mama aende ukweni kwanza, kisha baada ya mwezi mmoja au chini ya hapo kidogo, mume aende wakayazungumze huko.
Jambo hili hufanyika wakiwa na imani kubwa kwamba, wakikaa mbali baada ya muda huo, kila mmoja hasira yake hupungua na kila mmoja kwa wakati humkumbuka mwenzake, hivyo wakikutana muda huo, ni rahisi kupata suluhu na kurudi pamoja nyumbani.

Comments