Donald Trump amekuwa rais wa tatu
katika historia ya Marekani kupigiwa kura ya matumizi mabaya ya
madaraka, hatua inayompeleka moja kwa moja katika kesi dhidi yake
itakayoamua ikiwa atabakia mamlakani au la.
Bunge la Wawakilishi
(Kongresi) lilipigia kura mashtaka mawili - kwamba rais alitumia vibaya
mamlaka yake na kwamba alizuia shughuli za Bunge hilo. Kura zote zilipigwa kulingana na mirengo ya vyama huku karibu wabunge wote wa chama cha Democtrats wakipiga kura kuunga mkono ashtakiwe huku Republican wakipinga kura hiyo.
Wakati kura ilipokua inapigwa, Bwana Trump alikuwa akihutubia mkutano wa wafuasi wake.
Aliuambia umati wa watu waliokua wamekusanyika katika eneo la Battle Creek, jimboni Michigan kwamba: "Wakati tunabuni ajira na kupambana kwa ajili ya Michigan, wenye itikadi kali za mrengo wa kushoto katika Congress wamejawa na wivu na chuki na hasira kubwa, unaona kile kinachoendelea."
Ikulu ya White House ilitoa taarifa inayosema kuwa rais "anaimani kwamba atasafishwa na tuhuma zote" katika kesi hiyo kwenye Bunge la Seneti.
Vikao vya Jumatano vya Kongresi vilianza kwa wajumbe wa wa chama cha rais Trump cha Republican kuomba kwanza utaratibu wenyewe wa siku upigiwe kura wakiwa na nia ya kuleta usumbufu.
Hiyo ilifuatiwa na kura juu ya sheria zitakazotumiwa kwa ajili ya uchunguzi, mchakato uliochukua muda wa saa sita za mjadala wa wabunge wa pande mbili juu ya uhalali, umuhimu na uzito wa mashtaka mawili dhidi ya Trump.
Ilipofika saa 10 unusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki ( sawa na 01:30 GMT), Bunge la wawakilishi likaitisha kura kwa ajili ya mashitaka mawili: Shitaka la kwanza likiwa ni kutumia vibaya mamlaka aliyonayo lililotokana na madai ya kwamba Trump alijaribu kuishinikiza Ukraine kutangaza uchunguzi dhidi ya hasimu wake wa kisiasa na muwadia urais kupitia chama cha Democrats, Joe Biden. ,
Shitaka la pili lilikua ni kuzuia shughuli za bunge la Kongresi kwasababu rais anadaiwa kukataa kutoa ushirikiano katika uchunguzi dhidi yake, kwa kukataa kutoa nyaraka za ushahidi na kuwazuwia wasaidizi wake kutoa ushahidi katika uchunguzi huo.
Kura katika kipengele cha kwanza cha uchunguzi, cha kutumia vibaya mamlaka zilikuwa 230 ndiyo na 197 hapana na kipengele cha pili cha kuzuwia utendaji wa Kongresi zikawa 229 ndiyo na 198 hapana.
Kuchuguzwa kwa Bwana Trump kunamuweka katika nafasi za marais wengine wawili tu katika historia ya taifa hilo- Andrew Johnson na Bill Clinton - na sasa Bunge la Seneti litaendesha kesi juu ya urais wake.
Hata hivyo chama cha Republican kina wawakilishi wengi katika Bunge la Seneti na hivyo anatarajiwa kushinda kesi hiyo na kusalia madarakani.
Ilikua ni siku ya ushabiki wa mirengo ya kisiasa
Shughuli imekamilika. Donald Trump sasa amekuwa ni rais wa tatu katika klabu ya wajumbe maalumu ambayo- hakuna mtu anataka kuwa mjumbe wake.
Lakini waliotunga katiba yenye kipengele cha uchunguzi wake hawakutarajia kuwa kungekua na ushabiki wa upendeleo wa hali ya juu - katika pande zote za kisiasa- ambao ulishuhudiwa wakawa vikao vya Jumatano katika bunge.
Kila upande na msimamo wake, hakuna upande uliomsikiliza mwenzake. Na mtu anaweza kusema kwa uhakika kwamba si jambo la ajabu kwamba hali hii ikatokea tena wakati kesi itakapofikishwa katina bunge la Seneti mwaka ujao.
Donald Trump ataondolewa mashitaka. Hatalazimishwa kuondoka madarakani.
Kwa hivyo je kuna mabadiliko gani? Donald Trump atakuwa na nafasi katika vitabu vya historia- na kwa mwanamme mwenye kujiamini binafsi kama yeye hilo litamuuma. Vibaya.
Lakini 2020? Mbali na kwamba hili ni pigo kubwa dhidi ya Trump , inaweza kuchochea azma ya kuchaguliwa kwake kwa muhula wa pili.
Spika wa bunge Nancy Pelosi alikuwa na wasi wasi juu ya kuchukua njia ya kumchunguza Trump. Tutabaini mwezi Novemba mwakani ikiwa hofu yake ilikuwa ya msingi.
Wakati wa mjadala wa bunge, Bwana Trump alituma jumbe za twitter mara kadhaa, akizitaja hoja za wajumbe wa Democratic "ZA UONGO MBAYA ZINAZOTOLEWA NA WATU WENYE ITIKADI KALI ZA MRENGO WA KUSHOTO" na za "KIKITUSI CHAMA CHA REPUBLICAN !!!!".
Chama cha Democrat kina wabunge wachache katika Seneti, na hivyo uamuzi wa kumuondoa rais huenda usitekelezwe wakati maseneta watakapopiga kura yao .
Spika wa Seneti ambaye anatoka chama cha Republican Mitch McConnell wiki iliyopita ali sema maseneta wa Republican watashughulikia uchunguzi wa Trump kwa "uratibu kamili" na timu ya rais wakati wa kesi na kupiga kura kupinga mchakato.
Je wabunge walisema nini?
Spika wa Bunge Nancy Pelosi alifungua mjadala kwa hotuba."Kwa karne nyingi Wamarekani walipigana na kufa kuilinda demokrasia kwa ajili ya watu, lakini inasikitisha sana sasa malengo ya waasisi wa jamuhuri yanapata tisho kutoka Ikulu ya White House," alisma,
"Kama hatutachukua hatua sasa, tutakua tunakwepa jukumu. Ni huzuni kwamba vitendo vya kijinga vya rais vinafanya uchunguzi uwe. Hakutupatia chaguo."
Muakilishi wa Democratic Joe Kennedy, ambaye ni kitukuu wa rais wa zamani President John F Kennedy, alitumia hotuba yake kuwaambia watoto wake moja kwa moja, akielezea juu ya uamuzi wake kupigia kurakufanyika kwa uchunguz
"Wapendwa Ellie na James: Huu ni wakati utakaosoma kuuhusu katika vitabu vyenu vya historia ," alisema mbunge huyo wa kongresi wa Massachusetts, kuchukua uamuzi wa kumtuhumu rais kwa "kutumia mamlaka yake vibaya kama silaha dhidi ya watu wake binafsi ".
Doug Collins, mbunge wa ngazi ya juu wa Republican katika kamati ya bunge ya sheria, aliwashutumu Democrats kwa kuendesha uchunguzi usio wa haki na usiokubalika kisheria.
"Huu ni uchunguzi wenye misingi ya dhana. Hii ni kura- ya jaribio la uchunguzi juu ya ni nini kinachoweza kuuzwa kwa Wamarekani ," Alisema Bwana Collins.
Republican Barry Loudermilk alilinganisha mchakato wa uchunguzi na mchakato wa hatma ya Yesu kristo . "Wakati wa kesi iliyotungwa, Ponsio Pilato aliweza kupata haki zaidi kwa Yesu kuliko Wademocrat walizopata katika mchakato huu wa rais ," Bwana Loudermilk alisema.
Democrats wanaripotiwa kuagizwa na Bi Pelosi kutekeleza mchakato huo kwa ukweli na haki. Aliwaambia waandishi wa habari nje ya bunge kuwa "inasikitisha" kuwa na kikao, na kwamba Wademocrat wengi wanasikitishwa na kuhusika kwao katika mchakato wa uchunguzi .
Kote nchini Marekani saa 24 kuelekea upigaji kura , waandamanaji wanaounga mkono uchunguzi huo waliandamana mitaani. Mamia ya watu walikusanika katika medani ya Times Square mjini New York Jumanne usiku wakishangilia : "Niambie ni nani alie juu ya sheria? Hakuna alie juu ya sheria!"
Comments
Post a Comment