Jurgen Klopp: Kocha wa Liverpool alalamikia msongamano wa mechi katika msimu wa Sikukuu

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amesema ni uhalifu mkubwa kwa timu za Ligi ya Primia kucheza mechi mbili ndani ya siku tatu katika msimu huu wa Sikukuu.

Majogoo wa Jiji Liverpool, wanaminyana na Leicester siku ya Alhamisi, na baada ya hapo kucheza na 'Wolves' siku ya Jumapili, lakini timu zingine zimepata siku moja tu ya kupumzika kabla ya kuingia tena uwanjani.
Liverpool itakuwa imecheza michezo tisa ndani ya mwezi huu Disemba, baada ya kushinda kombe la klabu la dunia nchini Qatar na kushindwa katika kombe la Carabao.
''Sio sawa kabisa'' amelalama Klopp.
''Na bado tuna mechi. Hakuna meneja hata mmoja aliyekuwa na tatizo la kuwa na mechi katika siku ya ''Boxing Day'' lakini kucheza tarehe 26 na 28 ni uhalifu.''
''Tunaweza kusema chochote tunachokitaka lakini hakuna mtu yoyote anayejali, lakini kila mwaka kitu hicho kinajirudia kwa makocha wanaoshiriki.''
Kombe la klabu la dunia ni taji la pili kwa Liverpool msimu huu na wana alama 10 juu ya chati ya Ligi ya Primia wakiwa na mechi moja ya kiporo mkononi. Taji lao la kwanza lilikuwa kombe la Uefa Super Cup waliolipata Agosti baada ya kuichapa Chelsea kwa mikwaju ya penati.
Nusu fainali na fainali nchini Qatar ziligongana na kwa robo fainali za kombe la Carabao dhidi ya Aston Villa, kitendo ambacho kiliwafanya watume timu nyingine kushindana katika mashindano hayo.
Vijana wa Klopp, ambao wanaikimbiza nafasi ya kwanza kwa Liverpool ndani ya miaka 30 kushinda Ligi ya Primia, watakuwa na siku mbili tu za kupumzika katikati ya mechi za ligi katika msimu huu wa sikukuu , lakini klabu 14 zitakuwa na siku moja tu ya kupumzika kati ya mechi nyingine.
"Hakuna sababu ya kutoa saa chini ya 48 kwa timu kucheza mechi nyengine katika ligi," Klopp ameongeza.
"Sayansi ya michezo haikupi kitu cha kukabiliana nacho, mwili unahitaji muda fulani kupumzika. Ni rahisi. Hiyo ni sayansi. Lakini hilo linapuuzwa kabisa."
Crystal Palace inayonolewa na Roy Hodgson inacheza na West Ham nyumbani Alhamisi hii saa 18:00 (Saa za Afrika Mashariki) na saa 48 baadaye itakipiga na Southampton ugenini Jumamosi saa 18:00 (Saa za Afrika Mashariki).
"Nilifurahia mazoezi, mechi zenyewe ni kidogo na nafikiri kwamba kucheza kwa kiwango tunachocheza ukilinganisha na muda tunaopumzika haviendani," amesema Hodgson.
"Si jambo gumu kutatuliwa. Silifurahii kwa kweli na najua huu ni wakati hatari sana - kunaweza kuwa na majeruhi, pamoja na uchovu. Na ghafla utajiona unaangalia juu ya jwedwali badala ya chini."

Comments