Mwaka 2020 Kuwa Mwaka Wa Kuwalinda Watoto Dhidi Ya Ukatili Mkoani Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wanarukwa kutumia sherehe za siku ya kuzaliwa Yesu kristo kutafakari nafasi za watoto katika familia na kuongeza kuwa serikali ya imejipaga kuhakikisha kuwa mwaka 2020 unakuwa ni mwaka maalum wa Mtoto katika mkoa.

Amesema kuwa kwa muda mrefu wanarukwa wamekuwa wanashindwa kuthamini maendeleo ya mtoto kiafya na kielimu kwani watoto wamekuwa wakienda shule bila ya kula chochote nyumbani na hata akifika shuleni ambapo anakaa zaidi ya masaa kumi hapewi chakula chochote hali inayopelekea watoto hao kushindwa kuzingatia masomo.

“Tunawatesa watoto wetu kwanini, Muasham Baba Askofu ningependa tutumie nafasi hii za Krismai na Mwaka mpya kutafakari nafasi ya mtoto ndani ya familia na maendeleo ya taifa letu, tuwape haki zao watoto wetu, tuwape chakula, tuache manyanyaso ya kuwatukana na kuwapiga ovyo, kuwachoma moto, kuwabaka, hivfi vitendo vyote vinamchukiza Mwenyezi Mungu, na mahala pengine mabinti zetu wanawaua hawa watoto wanatoa mimba na hata akizaa anamtupa, huu ukatili wa namna hii Mwenyezi mungu haupendi,” Alisema kwa masikitiko.

Ameongeza kuwa mipango iliyopo kwa mwaka huo katika kumlinda mtoto ni pamoja na kuhakikisha heshima ya mtoto inarudishwa, haki ya mtoto inapatikana, mtoto anathaminiwa anapata elimu yake, mtoto anakuwa na maendeleo na malezi ya kimwili na kiroho tangu akiwa mdogo ili aje kuwa na utu.

Ameyasema hayo alipokuwa akitoa salamu zake za Krismasi leo 25.12.2019 kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa wakati aliposhiriki ibada ya ya Krismasi katika kanisa la KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika Mkoani Rukwa.

Kwengineko nao viongozi wa dini kila mmoja kwa wakati wake aliweza kutoa makatazo, maonyo na ilani kwa waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini yaliyopo mkoani humo kuhakikisha wanalinda, wanakemea na kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohusika pindi wanaposhuhudia vitendo vya ukatili vikifanyika dhidi ya watoto.

Askofu Mkuu Jimbo Katoliki Sumbawanga Askofu Beatus Urrasa alisema kuwa sababu zinazopelekea ukatili dhidi ya watoto katika mkoa wa Rukwa ni pamoja na mmomonyoko wa maadili katika jamii unaoanzia kwenye familia, watu kutokuwa na hofu ya Mungu na Imani za kishirikina, mila na desturi potofu miongoni mwa makabila hasa juu ya mirathi na wazazi kutotimiza wajibun wao kikamilifu katika familia.

“Kanisa linaamini siku zote kwamba watoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hili tunasoma katika Zaburi ya 127:3 ni kwasababu hiyo katika maandiko matakatifu Bwana wetu Yesu Kristo alipoona watu wengine walipokuwa wakiwafukuza watoto aliwakemea akisema waacheni watoto waje kwangu, msiwazuie,akawakumbatia, akawabariki na hili tunasoma katika Injili ya Marko 10:4,” Alisema

Aliongeza kuwa ili kukomesha vitendo hivyo vya Ukatili anawaalika watu wote wenye mapenzi mema kushirikiana kurudisha maadili mahala pake, katika familia na katika jamii na kuwataka wanandoa wote kuheshimu muungano na utakatifu wa ndoa zao na kuwajibika kwa pamoja kuwalea watoto vyema.

Shekh wa Mkoa wa Rukwa Shekh Rashid Akilimali amewaasa madereva wa bodaboda, bajaji pamoja na makonda wa daladala kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kuwalinda na kuwachunga watoto ili wapate fursa ya kuweza kutimiza ndoto zao.

“Mimi kama Kiongozi wa Waislamu mkoa wa Rukwa natoa Ilani watoto wa Kike tuwaache wasome, wapate elimu ya msingi, wapate elimu ya sekondari, wapate elimu ya Chuo kikuu, hizi mimba za utotoni ni jambo ambalo linapigwa vita na dini zote hata dini yetu ya kiislamu inakataza, wewe uliye boda boda, dereva wa bajaji, konda wa mabasi mwache mwanao, mwache mtoto wa mwenzio aweze kupata elimu ili ajue maisha yake kuliko kumkatisha ndoto ya maisha yake,”Alisisitiza

Halikadhalika alitoa wito kwa wanarukwa kuwapa uhuru watoto wa kwenda shule wapate kujua elimu yao ya mazingira na kuharibu maisha ya mtoto ni dhambi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Kikristo (CCT) Manispaa ya Sumbawanga Mchungaji Steven Malaki amewataka watoto wote Nchini kumtegemea Mungu na kutegemea Sala na maombi wawapo nyumbani lakini pia wajiepushe na zawadi na msaada binafsi yenye lengo baya ndani yake ili waweze kuepukana na vitendo vya ukatili .

“Tunawaomba sana ndugu zangu wanadoa, ndoa iheshimiwe, ili kuepusha mafarakano na hivyo kusababisha kuleta talaka ambayo matokeo yake ni watoto kujiingiza katika shida kutokana na umasikini na kukosa mahitaji na hatimae kuingia katika matatizo ya kubakwa, kulawitiwa na kadhalika,” Alisema. Sheria ya Mtoto Na 21ya mwaka 2009 inaelekeza utoaji wa huduma za ulinzi na ustawi wa mtoto. Aidha sheria imetoa wajibu kwa watoto kuwasaidia wazazi wao kazi zisizo hatarishi na ambazo hazina madhara kiafya na zitakazompa mtoto fursa ya kushiriki katika masomo na michezo. Vilevile jamii ina wajibu wa kuhakikisha kwamba watoto wanaishi katika maadili mema na kutoa taarifa kwa mamlaka za serikali iwapo mtoto ataonekana kuzurura na haendi shule au anajishughulisha na ajira hatarishi.

Comments