Salam za mwaka mpya za Cuf zimezua mawsali mengi kwa Watanzania kwa hatma ya demokrasia ya taifa.
HALI YA UCHUMI
Kwa Watanzania wengi mwaka 2019 umekuwa mgumu kimaisha. Vyuma vimekaza umekuwa msamiati wa kawaida. Taarifa ya furaha duniani ya mwaka 2019 (World Happiness Report 2019) inaonyesha Tanzania ni nchi ya nne kati ya nchi 156 kwa kukosa furaha. Nchi zilizoko chini ya Tanzania kwa kukosa furaha ni
Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan ya Kusini. Nchi zote tatu zina matatizo ya kisiasa na vita vya ndani.
Taarifa ya Furaha Duniani inaonyesha unyonge na kunyon’gonyea kwa Watanzania kumekuwa kunaongezeka miaka ya awamu ya tano. Mwaka 2012, Tanzania ilikuwa ya nane kutoka chini na ilipata alama 4.01. Mwaka 2018 imekuwa ya nne kutoka chini na imepata alama 3.44.
Takwimu za serikali zinaonyesha idadi ya watu masikini imeongezeka kutoka watu milioni 13 mwaka 2007 na kufikia watu milioni 14 mwaka 2018. Hata hivyo asilimia ya watu masikini imepungua kutoka 34.4 mwaka 2007 na kufikia 26.4 mwaka 2018. Kigezo kinachotumiwa na Serikali kupima kama mtu mzima ni masikini ni kutumia shilingi 50,000/- kwa mwezi. Ukitumia kigezo cha kimataifa cha mtu mzima kutumia dola 1.90 karibu nusu ya Watanzania wote wamo katika dimbwi la umaskini.
Ili Tanzania itokomeze umaskini ni muhimu kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo. Wakulima wengi wa korosho wameathirika na sera za serikali zilivyotekelezwa katika ununuzi wa korosho. Hawajalipwa fedha zao za msimu wa 2017/18. Pia kuna wakulima wa pamba ambao hawajalipwa fedha za msimi uliopita. Wakulima wa tumbaku wamekosa soko baada ya mnunuzi mkubwa wa tumbaku kuacha kushiriki kwa madai ya tozo na kodi kubwa za serikali. Matumizi ya serikali katika sekta ya kilimo ni madogo mno. Mwaka 2017/18 sekta ya kilimo ilitengewa asilimia 2.5 ya matumizi yote ya serikali. Ili kuleta mapinduzi ya kilimo serikali inapaswa kutenga na kutumia vizuri alau asilimia 10 ya bajeti yake kwenye sekta ya kilimo.
Takwimu za Serikali zinaonyesha uchumi ulikua kwa asilimia 7.1 mwaka 2018 lakini Wataalamu wa Benki ya Dunia wanakadiria ukuaji halisi wa uchumi ni asilimia 5.4. Mzunguuko wa fedha umepungua. Serikali inakawia kulipa madeni ya wauza bidhaa na watoa huduma wa ndani na kusababisha wao kushindwa kuwalipa wanao wadai. Benki Kuu iongeze ukuaji wa ugavi wa fedha alau ufikie asilimia 15.
Mazingira ya kufanya biashara nchini Tanzania bado ni magumu. Utafiti wa Benki ya Dunia kuhusu wepesi wa kufanya biashara katika mwaka 2019, unaonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya 141 kati ya nchi 190. Rwanda ni nchi ya 38 na Kenya ni nchi ya 56. Ugumu wa kufanya biashara unapunguza uwekezaji wa sekta binafsi katika maeneo mbalimbali ya uchumi na kwa hiyo kupunguza ongezeko la ajira.
Ugumu wa kufanya biashara umesababisha kupungua kwa kampuni mpya zilizojisajiriwa kutoka 8890 mwaka 2015 na kufikia 5276 mwaka 2018 wakati nchini Rwanda kampuni mpya zilizosajiriwa zimeongezeka kutoka 9775 mwaka 2015 na kufikia 10635 mwaka 2018.
Lengo la sera za CUF ni kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwekeza katika sekta zote za uchumi. Sera za serikali ya CUF zitatabirika. Kodi zikusanywa bila kusababisha biashara nyingi kufungwa na uwekezaji kusitishwa. Uchumi utakua kwa asilimia 10 na kuongeza ajira kwa vijana wetu.
Hali ya Siasa
Tanzania imerudi nyuma katika ujenzi wa demokrasia. Kimsingi, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa haukufanyika. Zaidi ya asilimia 90 ya wagombea wa CUF waliojitokeza kugombea uongozi wa Vitongoji, vijiji na mitaa hawakupewa fursa ya kugombea kwa kunyimwa fomu za kugombea au kuenguliwa baada ya kujaza fomu za kugombea. Tulilazimika kutoshiriki uchaguzi huo baada ya wagombea wetu kuondolewa. Vyama vingine vya upinzani pia havikushiriki baada ya wagombea wao kunyimwa fursa ya kushiriki. CCM wanajidanganya kufurahia ushindi wa kishindo. Wanacheka baada ya kujitekenya wenyewe.
Taasisi inayofuatilia maendeleo ya demokrasia na uhuru duniani – Freedom House, kila mwaka inatoa Taarifa ya Hali ya Uhuru na Demokrasia duniani. Freedom House inatathmini haki za uhuru wa kisiasa na kijamii ulivyo katika kila nchi na kuzipa alama stahiki. Kwa kadri nchi inavyokaribia 100 ndiyo yenye haki na uhuru mkubwa wa kisiasa na kijamii. Katika Taarifa yake ya mwaka 2019, Tanzania imepata alama 45 kati ya 100 ukilinganisha na alama 52 mwaka 2018, alama 58 mwaka 2017, alama 60 mwaka 2016, alama 63 mwaka 2015, alama 64 mwaka 2014 na alama 66 mwaka 2013. Utafiti huu unaonesha hali ya uhuru na demokrasia nchini Tanzania imekuwa inapungua mfululizo katika kipindi cha awamu ya tano.
Ushiriki wa wananchi katika kuamua mambo yanayogusa maisha yao ni suala muhimu la maendeleo endelevu. Ni muhimu kwa Rais Magufuli kutambua kuwa ujenzi wa demokrasia ni sehemu muhimu ya maendeleo. Kuwanyima wananchi fursa ya kugombea na kuchagua viongozi wanaowataka ni kudumiza maendeleo ya kisiasa na kijamii. Unapowanyima haki za kisiasa wananchi unabomoa msingi wa amani ya kweli.
Amani ya kweli ya nchi yetu itaathirika sana ikiwa yaliyofanyika katika uchaguzi wa serikali za mitaa na chaguzi nyingi za marudio ndiyo yatakayoendelezwa katika uchaguzi mkuu wa 2020. Katika salamu hizi za mwaka mpya tunatoa wito kwa Rais Magufuli kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kuweka mazingira mazuri ya kushiriki uchaguzi mkuu wa 2020 uwe huru na wa haki.
Sheria mpya ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 2018 imeanzisha uwepo ya kura ya mapema kwa wale wananchi na askari watakaohusika katika kusimamia masuala ya uchaguzi. Ni muhimu kwa ZEC kuwahakikishia wananchi kura ya mapema haitakuwa mwanya wa kupanga matokeo yanayotakiwa na serikali.
Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Zanzibar ili uandikishwe kuwa mpiga kura lazima uwe na kitambulisho cha ukaazi. Kimsingi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kutoa vitambulisho vipya vya ukaazi. Bila kuwa na kitambulisho kipya huwezi kuandikishwa katika Daftari la Wapiga Kura hata kama una kitambulisho ulichotumia mwaka 2015 kupigia kura. Kujenga demokrasia na amani na utulivu wa kweli ni muhimu Wazanzibari wote bila ubaguzi wakapewa fursa ya kuandikishwa kuwa wapiga kura.
USALAMA WA RAIA NA HAKI ZA BINADAMU
Matukio ya utekaji wa raia na watu wasijulikana bado ni tishio la amani na usalama wa raia. Matukio yliyotokea siku za nyuma mengi hayajatolewa maelezo kwa familia za wananchi waliopotea. Kwa mfano, tarehe 12 Juni 2017 mnamo saa 9:00 za usiku, watu wasiojulikana waliokuwa na bunduki walifika nyumbani kwa Mhe. Ziada Salum Nongwa, kijiji cha Maparoni. Mhe. Ziada ni Diwani wa Viti Maalum kwa tiketi ya The Civic United Front – (CUF – Chama Cha Wananchi), Halmashauri ya Kibiti. Pia Ziada ni mke wa Mhe. Haji Ngachoka, Diwani wa CUF wa Kata ya Maparoni, Siku hiyo hakuwepo nyumbani. Alikuwa kwenye mji wake mwingine katika kijiji cha Kiechuru. Ziada alikuwa na mtoto mchanga wa mwezi mmoja. Alichukuliwa na watu hao na kumuacha mtoto mchanga aliyekuwa anamnyonyesha. Mmewe alitoa taarifa ya kutekwa kwa mke wake Jeshi la Polisi Kibiti na Mafia. Pia ameandika barua kwa Waziri Mkuu lakini mpaka hivi sasa hakuna taarifa ya uhakika nini kilichomtokea Ziada. Mtoto aliyemuacha wa mwezi mmoja sasa ana miaka miwili. Analelewa na bibi yake. Hajui mama yake yuko wapi. Kuna malalamiko mengi ya watu kupotea hasa mwaka 2017 katika maeneo ya Kibiti na Rufiji. Tatizo la raia kutekwa na Watu wasiojulikana limewakumba waandishi wa habari, wasanii na hata mfanya biashara mkubwa. Ni vyema Serikali ikaunda Tume huru ya kuchunguza suala la wananchi wengi waliopotea ili kujua ukweli wa malalamiko haya.
Katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, Rais Magufuli aliwasamehe wafungwa 5533 kati ya wafungwa 17,547 walioko magerezani. Tunapongeza hatua hizo. Pia alieleza anasikitishwa na idadi kubwa ya mahabusu 18,256. Kati ya mahabusu hao wako Masheikh waliowekwa ndani kwa zaidi ya miaka sita na ambao kesi zao zinasuasua Mahakamani kwa kukosa ushahidi. Tunamuomba na kumshauri Rais Magufuli kuwaachia Sheikh Msellem, Sheikh Farid na wenzake waweze kuungana na familia zao na kusheherekea mwaka mpya 2020
HITIMISHO
Kesho tunamaliza muhula wa miaka ya 2010. Chama cha CUF ni muumini wa demokrasia na haki sawa kwa wote. Tunajipanga kuweka Wagombea nchi nzima katika ngazi zote - Madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Madiwani, Wawakilishi na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tunawaomba Watanzania wote tuwe imara katika kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu wa 2020 unakuwa huru na wa haki. Hii ni nchi yetu sote. Ni wajibu wetu tushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa 2020 na tuchague viongozi watakaojenga amani ya kweli ambayo msingi wake ni haki na kujenga uchumi unaoongeza ajira na kuwapa furaha wananchi wote.
Nawatakia Watanzania Heri na Fanaka ya mwaka 2020 na sote tuwe ngangari kinoma katika kudai uchaguzi huru na wa haki mwaka 2020.
HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE
MUNGU IBARIKI CUF. MUNGU IBARIKI TANZANIA
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa Taifa
Comments
Post a Comment