WINGA wa Yanga, Patrick Sibomana ameendelea kuipaisha timu hiyo baada ya kufunga bao la pekee kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Prisons ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Uwanja wa Samora mkoani Iringa.
Sibomana aliipatia Yanga bao hilo pekee dakika ya tano tangu kuanza kwa mechi hilo bao ambalo lilidumu hadi dakika 90 zote kumalizika.
Sibomana alifunga bao hilo lililotokana na mpira wa kurushwa na kiungo mkabaji Abdulziz Makame ambaye alikuwa muhimili katika mchezo huo kutokana na uwezo wa juu aliouonyesha dakika zote za mchezo huo.
Kwa ushindi huo, Yanga wamepanda hadi nafasi ya tatu kutoka nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi huku wakiwa wamekusanya pointi 21 katika mechi 10 walizocheza hadi sasa.
Yanga imeweka rekodi msimu huu kuwa timu ya kwanza kuifunga Tanzania Prison kwani wao tangu kuanza kwa ligi mwezo Agosti hawakupoteza mchezo wowote.
Yanga licha ya kuondoka na pointi tatu lakini walionekana kuwa na wakati mgumu hasa kwenye kumalizia ambapo washambuliaji Devid Molinga, Raphael Daudi, Deus Kaseke na Sibomana walikuwa wakikabwa muda mwingi na walinzi wa Prison.
Lakini hata nafasi chache ambazo walitengeneza za kufunga ambazo Yanga walipata kupitia Daud na Molinga walionekana kukosa umakini na kushindwa kuzitumia na kama wangekuwa makini huenda wangepata mabao zaidi.
Yanga katika kuhakikisha wanaimarisha kikosi chao walifanya mabadiliko ya wachezaji wawili dakika 45, alitoka Daud aliyeonekana kuwa katika kiwango cha kawaida na kuingia Mrisho Ngassa ambaye kuna muda alionekana kuongeza kasi ya ushindani eneo la ulinzi la Prisons.
Mabadiliko mengine Yanga walifanya dakika 65, alitoka Makame baada ya kuumia na nafasi yake kuingia Papy Tshishimbi ambaye alikwenda kutuliza kasi ya kushambulia kwa Prisons ambao walikuwa wakionekana kutafuta bao la kusawazisha.
Kwa upande wa Tanzania Prisons wao baada ya kupoteza mchezo huo katika msimamo wa ligi watashuka kutoka nafasi ya nne mpaka ya tano wakiwa na pointi zao 20 huku wakiwa wakicheza mechi 13.
Kuanzia dakika 60 mpaka dakika 72, Prisons walionekana kushambulia mara kwa mara kuliko Yanga lakini walishindwa kupata bao la kusawazisha huku wakiwa wametengeneza baadhi ya nafasi za kufunga ambazo walikutana nazo Jeremia Juma, Cleoface Mkandala na Samson Mbangula walishindwa kuzitumia na matokeo kuendelea kubaki vile vile mpaka dakika 90, zilipomalizika.
Katika mchezo huo kiungo wa Prison Adil Buha, alipata kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu kiungo mshambuliaji wa Yanga Mohammed Issa 'Banka' dakika za nyongeza baada ya zile 90, kumalizika.
Tukio hilo la kutoka kadi nyekundu ni kama linajirudia kwani msimu uliopita timu hizo zilipokutana Uwanja wa Sokoine wachezaji wawili Ngassa na Laulian Mpalile wa Prisons walipewa kadi nyekundu.
Comments
Post a Comment