TATIZO LA UGUMBA KWA WANAWAKE




TATIZO LA UGUMBA KWA WANAWAKE. 
Ugumba ni hali ambapo mwanaume na mwanamke hupoteza uwezo wa kubeba ama kusababisha ujauzito. Kwa mwanaume ugumba ni hali ya kukosa ya kushindwa kusababisha ujauzito kwa mwanamke kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuwa na mbegu zisizokuwa na nguvu ya kutosha ama kuwa na mbegu chache kabisa.
Kwa mwanamke hali hii hutokea pale mwanamke anaposhindwa kubeba ujauzito, na hii inaweza kusababishwa na mambo mbalimbali kama kuvurugika kwa homoni, uvimbe katika kizazi, maambukizi ya aina mbalimbali kwenye kizazi cha mwanamke na mambo mengine mengi.
Ugumba unaweza kuwa katika hali mbili kuu. Kuna aina ya ugumba ambayo yenyewe inahusisha wanawake ambao hawajawahi kuzaa hata mara moja na kukutwa na hali hii ya kutokuweza kupata ujauzito. Aina ya pili ya ugumba ni ile ambayo humpata mwanamke aliyewahi kupata ujauzito na kuzaa ama kutokuzaa kwa mara ya kwanza na baadae kupatwa na hali ya kutoweza kubeba ujauzito tena.
DALILI ZA TATIZO la ugumba kwa mwanamke ni pamoja na;


*Mwanamke kukosa hedhi ama kupata matatizo ya hedhi kwa ujumla. Hasa kwa wanawake ambao hedhi zao hazina siku maalum, ama hedhi kukoma kabla ya wakati, hedhi nyingi kupita kiasi, hedhi ndogo kupita kiasi na matatizo yote yanayohusisha hedhi kwa mwanamke.
*Dalili nyingine ni kutokwa uchafu ukeni. Hili ni janga kubwa sana kwa wanawake, kwani kutokwa na uchafu kwa wanawake ni tatizo linaloendelea siku hadi siku.
*Kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa na kuwa mwenye kufanya ili tu kutimiza wajibu bila kufurahia. Hali hii wakati mwingine huambatana na wanawake wengine baada ya masaa mawili ama matatu tangu alipofanya tendo la ndoa mbegu(shahawa) hutoka. Ama kwa wengine hutoka baada ya siku moja ama mbili. Hii ni dalili kubwa sana ya ugumba kwa wanawake, kwani shingo ya kizazi huwa imeziba mbegu na hivyo hushindwa kupita ama iko wazi ama imelegea.
*Dalili nyingine kubwa huwa ni pale mwanamke anapokuwa anashika ujauzito na hutoka. Wengine hugundua kuwa ujauzito umetoka na wapo wengine ambao hushindwa kugundua kuwa ujauzito wao na mara nyingi huandamwa na hedhi isiyoeleweka eleweka na wakati mwingine kupata hedhi nzito sana na ya mabonge mabonge.
Ili mwanamke aweze kupata mimba, sehemu zote za mwili wake zinazohusika na uzazi zinatakiwa zifanye kazi inavyotakiwa na katika hatua zote. Hatua katika utengenezaji wa mimba ni kama zifuatazo;


1. Moja kati ya ovari mbili za mwanamke kuachia yai lililokomaa.
2. Yai hili kusafirishwa na mrija wa uzazi (fallopian tube).
3. Mbegu za mwanaume na zilizo katika ubora unaostahili kusafiri hadi kwenye mlango wa mji wa mimba, kupitia tumbo la uzazi (uterus) hadi kwenye mrija wa uzazi, kulifikia yai na kulipevusha.
4. Yai lililopevushwa kusafiri kupitia mrija wa uzazi hadi kwenye tumbo la uzazi (uterus).
5. Yai kunata kwenye ukuta wa tumbo la uzazi (uterus) na kukua.
Ugumba kwa mwanamke unaweza kutokana na dosari katika hatua yoyote katika hizo zilizoainishwa na mara niyingine kutokana na dosari katika hatua zaidi ya moja. Pamoja na kuwa kuna sababu nyingi za mwanamke kutopata mimba, lakini sababu kuu tatu ndizo zinazohusika zaidi.
;Kushindwa Kuzalisha Mayai (Anovulation).
Hili ndilo tatizo ambalo linachangia ugumba kwa wanawake kwa asilimia 30. Mwanamke mwenye tatizo hili hutoa mayai mara chache ama hatoi mayai kabisa. Chanzo cha tatizo huwa ni moja ya yafuatayo;
1. Matatizo ya homoni
Matatizo ya homoni ndiyo yenye mchango mkubwa zaidi kwenye kumfanya mwanamke ashindwe kuzalisha mayai. Uzalishwaji wa mayai hutegemea mchanganyiko wa homoni utakaofanya kazi kwa kuhusiana bila kuvurugwa katika utendaji wake wa kazi.
Kuna matatizo ya aina tatu yanayoweza kuvuruga mpangilio huo.
:-Kuzalisha Mayai yasiyokomaa:
:-Matatizo ya sehemu ya ubongo inayohusika na kutoa ishara kwa tezi kuu inayotawala tezi zingine zote (pituitary gland) ambayo nayo huamsha homoni za kiwanda cha mayai zinazoruhusu yai kukomaa.
:-Matatizo ya tezi kuu,hasa pale tezi hii itatoa homoni kwa kiwango kidogo au kikubwa kupita kiasi, viwanda vya mayai vitashindwa kuzalisha na kutoa mayai ipaswavyo, kwa kuwa tezi hii huhusika katika kukomaza mayai. Hali hii hutokea pale tezi hii inapoharibiwa kwa ajali, kunapotokea uvimbe ndani yake ama kunapokosekana ulingano wa kikemikali ndani ya tezi hiyo.
2. Makovu kwenye Ovari.
Uharibifu kwenye kiwanda cha kuzalisha mayai(ovary) unaweza kusababisha ovari hizi kushindwa kuzalisha mayai. Operesheni za mara kwa mara hujenga makovu kwenye ovari hizo na kuzifanya zishindwe kuzalisha mayai. Maambukizi ya magonjwa huweza pia kusababisha ovari kushindwa kuzalisha na kutoa mayai.
3. Kukoma Hedhi Mapema.
Kukoma hedhi mapema ni tatizo ambalo halijaeleweka vizuri kisayansi. Baadhi ya wanawake huacha kupata siku zao za hedhi kwenye umri usiotegemewa. Dhana moja ni kuwa hifadhi yao ya mayai imekwisha ama nyingine ni kuwa inatokana na wanawake hawa kuwa wenye historia ya kuwa wanariadha waliokuwa na miili yenye uzito mdogo na waliofanya mazoezi ya nguvu kwa muda mrefu. Kukoma hedhi mapema ni suala linaloweza kuwa la urithi.
4. Matatizo ya mfuko wa mayai(Follicle).
Kuna tatizo lisilo na maelezo ya kisayansi “unruptured follicle syndrome” ambapo mwanamke hutengeneza mfuko wa kawaida wa yai wenye yai ndani yake kila mwezi lakini mfuko huo hugoma kupasuka na kuachia yai. Hivyo kwamba, yai hubaki ndai ya ovari na utolewaji wa yai nje ya ovari kutotokea.
;Mirija Ya Uzazi (Fallopian Tubes) Kushindwa Kufanya Kazi Vizuri.
Magonjwa katika mirija ya uzazi huathiri asilimia 25 ya wanafamilia ambapo tatizo linaweza kuwa dogo la kunata kwa yai au kubwa la mirija kuziba kabisa. Matatizo yanayopelekea kuziba kwa mirija ya uzazi ni kama;


1. Maambukizi ya wadudu.
Maambukizi ya virusi na bakteria yanayoenezwa kwa ngono husababisha makovu na uharibifu. Kwa mfano, maambukizi ya ‘Hydrosalpnix’ yanayosababisha mirija ya uzazi kuziba pande zote na kujaa maji.
2. Magonjwa ya tumbo.
Magonjwa ya kidole tumbo(appendicitis) na vidonda vya kwenye utumbo(colitis) huleta madhara kwenye tumbo ambayo yanayoweza kuiathiri mirija ya uzazi kwa kujenga makovu au kuiziba.
3. Upasuaji.
Hii ni sababu kubwa ya magonjwa na uharibifu wa mirija ya uzazi. Upasuaji wa kwenye maeneo ya kinena na tumbo huweza kusababisha uharibifu kiasi cha kuzuia upitaji wa yai.
4. Mimba ndani ya mirija ya uzazi (Ectopic Pregnancy).
Mimba zinazotunga ndani ya mirija ya kizazi huweza kuleta uharibifu kwenye mirija hiyo hata kama tahadhari ya juu itachukuliwa kuziondoa.
5. Matatizo ya kuzaliwa nayo.
Mara chache huweza kutokea kuwa mwanamke akazaliwa akiwa na dosari katika mirija yake ya uzazi.
;Kuota kwa seli (endometrial cells) zinazofanana na zile zinazotanda ndani na nje ya mfuko wa uzazi (uterus) kwenye eneo nje ya mfuko wa uzazi. Endometrial cells ndizo zinazoufunika mfuko wa uzazi, na seli hizi hubadilishwa kila mwezi wakati wa hedhi. Seli hizi huweza kuota kwenye maeneo mengine yaliyo nje kabisa ya mfuko wa uzazi na huitwa ‘endometriosis implants’. Maeneo ambayo seli huweza kuota ni kwenye ovari, mirija ya uzazi (fallopian tubes), kuta za nje za nyumba ya uzazi, utumbo, njia ya mkojo, ukeni , mlango wa mji wa mimba, kibofu na mara chache kwenye maini, mapafu na ubongo.
Tafiti zinaonesha kuota kwa seli hizi zaidi kwenye kundi la wanawake wenye umri kati miaka 25 na 35, ingawa mara chache imeonekana kwa wasichana wadogo wa miaka kama 11. ‘Endometriosis’ ni nadra kuonekana kwa wanawake waliokoma hedhi. Wanawake warefu ,wembamba wenye uzito mdogo huonekana zaidi na tatizo hili. Kupata ujauzito katika umri mkubwa sana, kutozaa na kukoma siku mapema huongeza uwezekano wa kutokea kuota kwa seli hizi.
Kuota kwa seli hizi za ziada na tendo la kuziondoa kwa upasuaji huweza kusababisha makovu ambayo huweza kuzuia yai la mwanamke lisiungane na mbegu ya mwanaume. Kuathirika kwa utando huu juu ya mji wa mimba huweza kuzuia kutungwa kwa yai lililopevushwa.
SABABU NYINGINE.

1. Sababu Za Kitabia

Baadhi ya tabia huathiri afya ya mwanamke ikiwa ni pamoja na afya ya viungo vya uzazi na kupunguza ama kuondoa uwezo wao wa kuzaa watoto.Bahati nzuri tabia hizi zinaweza kudhibitika.
. Chakula Na Mazoezi: Ili tuwe na uwezo mzuri wa kuzaa watoto tunahitaji kupata chakula kizuri na kuipa miili yetu mazoezi ya kutosha. Wanawake wenye unene wa kupindukia ama uzito mdogo sana hupata shida kushika mimba.
. Uvutaji Wa Sigara: Uvutaji wa sigara umethibitika kupunguza kiwango cha mbegu (low sperm count) kwa wanaume, kuongeza uwezekano wa mimba kutoka, kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo ama kabla ya wakati (njiti) kwa wanawake.
. Pombe: Unywaji wa pombe huongeza uwezekano wa kuzaa mtoto mwenye matatizo na unywaji uliozidi huweza kuleta ugonjwa, Fetal Alcohol Syndrome. Kwa mwanaume, pombe hupunguza kiwango chake cha mbegu.
. Madawa: Madawa kama bangi (marijuana) hupunguza kiwango cha mbegu kwa wanaume. Utumiaji wa ‘cocaine’ kwa wanawake huathiri figo za watoto watakaozaliwa.
2. Sababu Za Kimazingira
Uwezo wa mwanamke kutunga mimba unaweza unaweza kuathiriwa na uwepo wake kwenye mazingira yenye sumu ama kemikali. Hii inaweza kuwa kwenye mazingira ya kazi ama sehemu anayoishi. Baadhi ya kemikali zilizobainika na kuandikwa kuwa zinapunguza uwezo wa mwanamke kupata mimba ni;
. Madini ya risasi(Lead) ambayo hutumiwa pia kutengenezea rangi za midomoni (lipstiki) husababisha mimba kutoka.
. Matumizi ya mionzi ya mara kwa mara na ‘chemotherapy’ huathiri uzalishaji wa mbegu za kiume na matatizo ya ovari.
. Ethylene Oxide, kemikali inayotumika kuua wadudu kwenye vifaa vya upasuaji na kutengenza dawa za kuulia wadudu huleta dosari kwenye mimba changa na kusababisha mimba kutoka.
. Dibromochloropropane (DBCP), kemikali inayopatikana kwenye dawa za kuulia wadudu husababisha mwanamke kukoma hedhi mapema.

Comments