Wito huo umetolewa na shirika la afya duniani, WHO pamoja na washirika wake katika kuelekea siku ya homa ya ini duniani inayoadhimishwa kila mwaka Julai 28. Kauli mbiu ya mwaka huu ni : Pima, Tibu, homa ya ini.
WHO inasema homa ya ini aina ya B na C huathiri watu milioni 325 duniani na ikiwa vidudu vyake havitibiwi haraka vinauwezo wa kusababisha saratani ya ini ambavyo viliuwa watu zaidi ya milioni 1.3 mwaka 2015 pekee.
Pima,Tibu, homa ya Ini
Akizungumzia homa hiyo mkurugenzi mkuu wa WHO, Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema “tuna mtazamo thabiti wa kuutokomeza ugonjwa huo na nyenzo tunazo, lakini ni lazima tuchapuze mchakato ili kufanikisha lengo hilo ifikapo mwaka wa 2030.”
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa asilimia 20 tu ya watu ndio walipata huduma za kupimwa na kutibiwa dhidi ya maambukizi ya homa ya ini aina B na C mwaka 2016.
Naye mkurugenzi wa WHO anaehusika na VVU na homa ya Ini, Dr. Gottfried Hirnschall, amesema ili kuweza kutokomeza kabisa homa ya Ini kutahitajika ubunifu mkubwa, dawa bora na huduma bora za afya.
Siku ya homa ya ini itaadhimishwa kimataifa mwaka huu nchini Mongolia taifa ambalo lina idadi kubwa ya wagonjwa wa homa hiyo duniani.
Zaidi ya asilimia 10 ya watu milioni 3 wa Mongilia wanaishi na viini vya homa ya Ini. Taifa hilo lilianza mpango wa kitaifa kukabiliana na ugonjwa wa homa ya ini mwaka 2017 kwa lengo la kuutokomeza kabisa ungojwa huo ifikapo mwaka 2020 .
Taifa hilo linalenga kutoa huduma ya upimaji wa homa ya ini aina B na C kwa asilimia 60 hadi 80 ya watu wake na kutoa tiba ya homa ya Ini aina ya C kwa asilimia 80 ya watu wanaoihitaji.
WHO inasema eneo la Pasifiki ya magharibi ndilo linaongoza kwa kuwa na watu wengi zaidiwaishio na vidudu vinavyosababisha homa ya Ini katika maeneo sita yaliyoathirika zaidi na homa hiyo duniani.
Hadi mwishoni mwa mwaka 2015, takriban watu milioni14, walikuwa wanaishi na vidudu vya homa ya ini aina ya C huku wengine milioni 155 waliambukizwa aina ya B, na kila siku watu 1,200 wa eneo hilo hufariki dunia kwa kukosa matibabu ya homa ya ini.
Comments
Post a Comment