Unaweza kusema Freeman Mbowe amebaki peke yake. Hii ni kutokana na viongozi wote wa juu wa Chadema alikuwa nao katika uongozi aliposhika uenyekiti wa chama hicho mwaka 2004, kutokuwapo tena kwenye chama hicho kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuhamia CCM.
Hiyo
inaelezwa kuwa ni moja ya sababu za wanachama kuendelea kumuhitaji Mbowe
kukiongoza chama hicho kwa miaka mingine mitano kwa sababu amekuwa na
msimamo thabiti wakati wote wa miaka 15 ya uongozi wake.
Uchambuzi
uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kwamba Mbowe alichaguliwa kuwa
mwenyekiti mwaka 2004 akichukua nafasi ya Bob Makani wakati makamu
mwenyekiti akiwa ni Dk Amani Kabourou na Katibu Mkuu akiwa ni Dk
Willibrod Slaa.
Makamu mwenyekiti wake kwa upande wa
Zanzibar wakati huo alikuwa Mzee Said Mzee ambaye baadaye nafasi yake
ilichukuliwa na Said Issa Mohamed ambaye yupo hadi sasa.
Naibu
Katibu Mkuu – Bara alikuwa ni Shaibu Akwilombe wakati Naibu Katibu Mkuu
wa Chadema – Zanzibar akiwa ni Hamad Mussa Yussuf ambaye sasa yuko
ACT-Wazalendo.
Mwaka 2006, Dk Kabourou alitangaza
kukihama chama chake na kujiunga na CCM ikiwa ni mwaka mmoja baada ya
kushindwa ubunge katika jimbo la Kigoma Mjini kwenye uchaguzi wa
Nafasi ya Dk Kabourou ilichukuliwa na Chacha Wangwe ambaye wakati huo alikuwa pia ni mbunge wa Tarime.
Mwaka
huohuo, Akwilombe naye alitangaza kujiunga na CCM na nafasi yake kama
Naibu Katibu Mkuu – Bara kuchukuliwa na Zitto Kabwe ambaye naye wakati
huo alikuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Mwaka 2008,
Wangwe alifariki dunia kwa ajali ya gari na nafasi yake kujazwa na Said
Arfi ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa Mpanda Mjini.
Uchaguzi
ulifanyika tena mwaka 2009 na 2014, Mbowe akachaguliwa kuwa mwenyekiti
huku safu yake ya uongozi ikibaki ile ile; Makamu Mwenyekiti akiwa ni
Said Arfi, Katibu Mkuu, Dk Slaa, Naibu Katibu Mkuu – Bara – Zitto.
Hata
hivyo, Julai 2015 Arfi alitangaza kujiuzulu wadhifa huo akipinga
kitendo cha kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo.
Nafasi ya Arfi ilichukuliwa na Profesa Abdallah Safari ambaye katika uchaguzi wa sasa hatagombea tena wadhifa huo.
Baadaye
Arfi alitangaza kujivua uanachama wa Chadema na kuhamia CCM wakati
Zitto naye akivuliwa uanachama na kwenda kuanzisha chama chake cha ACT
-Wazalendo ambacho anakiongoza mpaka sasa. Nafasi ya Zitto ilichukuliwa
na John Mnyika ambaye yupo hadi sasa.
Mwaka huo huo, Dk
Slaa naye alijivua uanachama wa Chadema wakati chama hicho kikiwa
kwenye mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Miaka miwili
baadaye, Dk Slaa aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden.
Hamad
Yusuf Mussa aliyekuwa naibu katibu mkuu Zanzibar aliondolewa kwenye
uchaguzi wa mwaka 2014 na nafasi yake ilichukuliwa na Salumu Mwalimu
aliyepo hadi sasa.
Licha ya viongozi walioanza na Mbowe
kuachana na chama hicho, yeye ameendelea kuwa mwenyekiti wa chama na
hata sasa chama hicho kikiwa kwenye uchaguzi wa ndani, bado wanachama
wanamhitaji na tayari wamemchukulia fomu ili agombee nafasi hiyo. Hoja
hiyo pia inabebwa na wabaya washindani wake na wale wa chama kuwa amekaa
muda mrefu na anapaswa kuondoka.
Mkurugenzi wa
Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema
anasema moja ya sababu za wanachama kuvutiwa na uongozi wa Mbowe ni
msimamo wake thabiti usioyumbishwa.
Anasema sababu
nyingine ni mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 15 ya
uongozi wake ambayo yamekuwa ni kielelezo cha uongozi bora uliokijenga
chama hicho na kuwa chama kikuu cha upinzani.
“Wamepita
viongozi mbalimbali kwenye chama chetu lakini hatunao tena, lakini
wanachama bado wanamuhitaji Mbowe, kitu kikubwa wanachohitaji ni msimamo
wake thabiti na uongozi makini wa kukijenga chama,” alisema Mrema.
Katibu
Mkuu wa chama cha CCK, Renatus Muabhi anasema Chadema inamuhitaji Mbowe
sasa kuliko wakati wowote kwa sababu ndiye mtu anayeweza kuhimili
figisu, hila na changamoto zote ambazo chama hicho kinapitia katika
awamu h.
Alisema haoni mtu mwingine ndani ya chama
hicho ambaye anaweza kuwa mbadala wa Mbowe kwa sababu akiwekwa mtu
legelege chama hicho kitakufa kwa sababu si wote ni wavumilivu na mahiri
kama Mbowe.
“Mbowe anahitajika Chadema sasa kuliko
wakati wowote. Kwa hiyo, haijalishi ameongoza miaka mingapi, suala ni
amefanya nini kama kiongozi. Katika kipindi hiki watu wananunuliwa,
chama kinahitaji mtu ‘active’ ambaye atakabiliana na changamoto hizo,”
anasema.
Anasema Chadema inahitaji kiongozi ambaye
akitoa kauli inaonekana kweli imetoka kwa kiongozi na siyo kiongozi
ambaye hana ushawishi.
Muabhi anaamini Mbowe ni mtu makini mwenye uwezo, ndiyo maana wanachama wa Chadema bado wanamuhitaji.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa chama cha ADC, Doyo Hassan Doyo alisema
vyama vya upinzani hapa nchini havijawa imara kubadilishana uongozi kwa
sababu vinajengwa katika misingi ya kiitikadi.
Kwa
sababu hiyo, alisema Mbowe anastahili kuendelea kuongoza Chadema hasa
wakati huu ambao kuna siasa za rushwa na fedha kutumika kununua
viongozi. Alisema demokrasia ni mchakato ambao unakwenda na wakati wake.
“Sisi
tunachokiangalia ni usalama wa chama uko sawasawa? Haijalishi ameongoza
kwa miaka mingapi, tunaangalia mazingira ya kisiasa yaliyopo sasa,
huwezi kuondoka na kukiacha chama kwa kiongozi ambaye hana ideology
(itikadi) ya chama,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu
Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema Mbowe
amejipambanua kama kiongozi ambaye harubuniwi, kwa sababu hiyo anakiweka
chama katika hali ya usalama.
“Hebu fikiria inatokea
mwenyekiti wa chama kama Chadema anatangaza kujivua uanachama na kuhamia
CCM kama walivyofanya wengine, hicho chama si ndiyo kinakufa hivyo?
Nadhani wana hoja ya kumhitaji Mbowe,” alisema mwanazuoni huyo.
Comments
Post a Comment