Sumbawanga. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania,
Japhet Hasunga ameagiza kukamatwa kaimu mrajisi wa vyama vya ushirika
mkoa wa Rukwa, Anyosisye Mbetwa kwa tuhuma ya kushirikiana mmoja wa
mawakala wa pembejeo za kilimo kutapeli vyama vya ushirika zaidi ya
Sh277 milioni.
Ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Desemba
27, 2019 wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika (Amcos)
mkoa wa Rukwa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa mkoa huo
Sumbawanga Mjini.
Pamoja na mrajisi huyo, pia ameagiza
kukamatwa kwa wakala Elias Ndomba mkurugenzi wa kampuni ya Eli Agrovet
Co ambao waliahidi kufikishia mbolea wakulima hao kupitia vyama vyao vya
ushirika.
Waziri Hasunga amesema mrajisi huyo ambaye
ni ofisa ushirika wa mkoa huo kwa makusudi amekiuka sheria, kanuni na
taratibu za vyama vya ushirika hivyo amemshusha cheo hicho na sio ofisa
ushirika tena.
Amesema ofisa ushirika huyo amepoteza
sifa ya kuendelea kuwapo katika nafasi hiyo kwa kula badala ya
kuwasaidia wanaushirika yeye anashiriki kuwahujumu.
"Naagiza
hawa wote wakamatwe mara moja kwa kuwa wamewatapeli sana ushirika kwa
kuchukua fedha zao pasipo kuleta mbolea, labda wakileta mbolea hapa
ndiyo waachiwe tofauti na hivyo wafunguliwe mashtaka ya kuhujumu
uchumi," amesema Waziri Hasunga
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha Ufipa,
Anastela Malaji akizungumza kwa niaba ya Amcos 49 kiliingia mkataba na
kampuni ya Eli Agrovet ya kusambaziwa mbolea kwa bei elekezi iliyotolewa
na serikali amedai mrajisi aliwataka watoe fedha asilimia 30 ya mbolea
waliokuwa wakihitaji.
Amesema makubaliano ilikuwa
kampuni hiyo iongeze fedha asilimia 70 kisha kununua mbolea na
kuwafikishia wakulima lakini baadaye iligundulika haikuwa na mtaji huo
hivyo kuchukua fedha hizo za kwao kununua mbolea kiduchu aina ya Dap na
kuwapelekea kinyume na makubaliano yao.
Imeelezwa
makubaliano baina ya chama hicho na kampuni hiyo ilikuwa inunue mbolea
ya Dap, Urea na Can na kusambaza kwa wakulima ili waweze kuzalisha mazao
yao kwa tija
Comments
Post a Comment