Magdalena Sakaya: Mbunge wa kwanza kupongezwa na ccm



Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya 
  • Viongozi wa CCM Mkoa wa Tabora wamempongeza mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya kwa kufanya vyema majukumu yake ya ubunge

Tabora.  Viongozi wa CCM Mkoa wa Tabora wamempongeza mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya kwa kufanya vyema majukumu yake ya ubunge.
Kauli hiyo ilitolewa Jumapili Februari 24, 2019 na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani humo.
Amesema licha ya CUF kutokuwa na diwani hata mmoja katika jimbo hilo, lakini Sakaya anafanya kazi zake vyema.
Hata hivyo Sakaya hakuwepo katika mkutano huo na mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amesema amepata udhuru.
Wakasuvi amesema mbunge huyo anatumia fedha za mfuko wa jimbo kuwahudumia wana CCM na wengine wasio wa chama chake.

"Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni,” amesema mwenyekiti huyo.
Amesema katika uchaguzi wa mwaka 2015,  CCM walimsimamisha mgombea mzuri lakini alishindwa, kubainisha kuwa goli ni goli hata kama mpira utapita katikati ya miguu.
Mbunge wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu naye alimuombea udhuru Sakaya, akibainisha kuwa hakuwepo katika mkutano huo kwa kuwa yupo Nairobi, Kenya katika matibabu.
Katika uchaguzi wa mwaka 2015, Sakaya alipambana na mgombea wa CCM, Profesa Juma Kapuya na kuibuka mshindi.

Comments