Wakimbizi kutoka Somalia, Syria na Eritrea ambao wameachiwa kutoka vizuizini nchini Libya wakifuata utaratibu wa kuondolewa kutoka kwa kituo cha kuondoka Tripoli, Libya
.
.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linahofia usalama wa mamia ya wakimbizi na waomba hifadhi waliokusanyika katika kituo cha makutano na kuondoka (GDF) kilichopo mjini Tripoli nchini Libya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na mkuu wa ofisi ya UNHCR nchini Libya Jean-Paul Cavalieri, hofu yao inatokana na taarifa kwamba kuna maroketi matatu yameanguka leo karibu na kituo hicho ingawa kwa bahati nzuri hakuna aliyekufa wala kujeruhiwa.
Kituo hicho kiko chini ya mamlaka ya wizara ya mambo ya ndani ya Libya na UNHCR na mshirika wake LibAid wameruhusiwa na serikali ya Libya kutoa huduma kwenye kituo hicho tangu kilipofunguliwa Desemba 2018.
Kituo hicho cha GDF kilianzishwa kwa lengo la kuhifadhi wakimbizi wanaosubiri kuondoka ambao tayari wamepatiwa suluhu ya kupelekwa nje ya Libya.
Kwa mujibu wa UNHCR kituo hicho ambacho kwa sasa kina watu karibu 1000 wakiwemo makundi ya watu karibu 900 walioingia wenyewe tangu Julai mwaka jana, kimefurika na hakifanyi kazi tena kama kituo cha mpito.
UNHCR imezitaka pande zote katika mzozo wa Libya kuwalinda raia na miundombinu yao
Comments
Post a Comment