SHERIA YA MADHARA: MAELEZO NA UFAFANUZI

SHERIA YA MADHARA: MAELEZO NA UFAFANUZI


Na Wakili Laurencia F. Mayila.
Madhara ni matokeo hasi yanayompata mtu au kitu au mali kutokana na kitendo kilichofanywa
na mtu mwingine au kilichotokea kutokana na mtu Fulani kushindwa kutimiza wajibu na
kutokana na madhara hayo mtu aliyepata madhara anastahili kupata fidia.
Ili kupata fidia kutokana na madhara tajwa hapo juu, inampasa mtu aliyepata madhara hayo
kufungua shauri la madai katika mahakama yenye mamlaka ili mahakama iweze kupima
madhara yaliyotokea na kuamuru mtu aliyepata madhara kulipwa fidia au kutolipwa au kulipwa
kiasi kidogo au zaidi ya kile alichoomba kufidiwa.
Ili kufanikiwa katika shauri la kudai fidia kutokana na madhara yaliyosababishwa na mtu
mwingine au mtu mwingine kushindwa kutimiza wajibu wake mambo yafuatayo inabidi
yathibitishwe mbele ya mahakama.
i. Kuwe na wajibu wa kujali au wajibu wa kisheria upande wa mdaiwa fidia
ii. Wajibu huo uwe umevunjwa na mdaiwa fidia
iii. Uvunjwaji wa wajibu huo usiwe umechangiwa na anayedai fidia
iv. Na, kuwe na madhara yanayotokana na uvunjwaji wa wajibu upande wa mdai fidia.
Mojawapo ya sheria zinazosimamia madhara inatoka katika Sura ya 310 ya sheria za Tanzania
kama ilivyorejewa mwaka 2002 (The Law Reforms (Fatal Accidents and Miscellaneous
Provisions) Act)
Kuna namna mbalimbali ambazo mtu akishindwa kutimiza wajibu wake anaweza kusababisha
madhara kwa wengine na kupelekea mtu kudai fidia. Namna hizo ni kama zifuatazo;

1. Wajibu wa mwenyeji kuhakikisha kuwa wanaoingia na kutoka kwenye eneo lake
kwa halali hawadhuriki.

Mwenyeji ana wajibu wa kuhakikisha kuwa wote wanaoingia na kutoka katika eneo lake kihalali
hawapati madhara. Akishidwa kutimiza wajibu huo na madhara yakatokea, mtu aliyedhurika
anaweza kudai fidia. Baadhi mifano ya mambo yanayoweza kupelekea madhara kutokea na
mtu kudai fidia chini ya wajibu huu ni pale ambapo mtu amekwenda kwenye nyumba ya mtu au
taasisi na kukuta sakafu inateleza kutokana na kupiga deki au asili ya sakafu bila kuwa na ilani
(tahadhari) kuhusiana na hali ya sakafu hiyo na mtu akateleza/ akaanguka na kuumia au
endapo mtu amepanda gari la mtu mwingine na gari hilo likawa na viti vibovu na kupelekea mtu
kuumia au kupata ajali kutokana ubovu wa gari hilo.

2. Wajibu wa mtu kulinda hadhi na heshima ya mwingine;
Chini ya wajibu huu, kila mtu ana wajibu wa kulinda hadhi na heshima ya mwenzie. Iwapo mtu
atafanya lolote na kusababisha hadhi ya mwenzie kushuka, mtu aliyefanyiwa hayo anaweza
kudai fidia. Mfano wa uvunjifu wa wajibu huu ni pale ambapo mtu A amefanya tendo au
amesema maneno ambayo sio maoni halali juu ya mtu B mbele ya watu wengine na kwa maoni
ya hao watu wengine tendo lile au maneno yale yanashusha hadhi au yanamdhalilisha mtu B;
mtu B anaweza kwenda kudai fidia.


3. Wajibu wa mtu kutoharibu raha na furaha ya mtu mwingine. 

Wajibu huu unamaanisha kwamba mtu hatakiwi kuwasumbua wengine walioko jirani naye.
Mfano wa uvunjifu wa wajibu huu ni pale ambapo mtu anasababisha karaha kwa kuweka mziki
kwa sauti ya juu bila kibali au bila kuzingatia masharti ya kibali, au kelele au kusababisha harufu
mbaya kiasi cha kuwakosesha raha au kuwasumbua wengine.

4. Wajibu wa mwenye mali au mwajiri kuhakikisha kuwa mawakala au wafanyakazi

au waajiriwa wake, katika kutimiza wajibu wao kwenye kazi au ajira
hawasababishi madhara kwa watu wengine.
Wajibu huu unamanisha kwamba, mwajiri au mwenye mali ana wajibu wa kuhakikisha kuwa
mawakala au waajiriwa wake hawasababishi madhara kwa wengine wakati wanatimiza
majukumu yao ya kazi. Mfano wa uvujifu wa wajibu huu ni pale ambapo mfanyakazi/ mwajiriwa
aliyeajiriwa na mtu au taasisi au wakala wa mtu au taasisi akifanya kitu chenye kukuletea
madhara kwa mtu mwingie au juu ya mali ya mtu mwingine wakati anatimiza majukumu ya ajira/
kazi yake. Hili likitokea mtu aliyepata madhara binafsi au mali yake anaweza kudai fidia kutoka
kwa mwajiri au mwenye mali. Mfano mwingine ni pale ambapo mtu amepanda basi/ gari na
akapata ajali au kuumia akiwa kwenye basi hilo na kapata madhara anaweza kudai fidia kutoka
kwa dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo pamoja na mmiliki wa gari/ basi hilo. Mara nyingi hii
ni pale ambapo basi/ gari lilikuwa ni la biashara mfano mabasi yanayosafirisha abiria.

5. Wajibu wa watawala/ viongozi kuhakikisha hawafanyi vitendo ambavyo
vitawaathiri wananchi wao.

Chini ya wajibu huu, viongozi au watawala wanapaswa kujali na kufanya mambo ambayo
hayaleti madhara kwa wananchi wanaowaongoza. Mfano na vitu vinavyoweza kupelekea
madhara na kusababisha watu au mtu kudai fidia ni pale ambapo kiongozi anaruhusu takataka
zitupwe kwenye eneo fulani ambalo lipo kwenye makazi watu.

6. Wajibu wa mtu kuhakikisha mwenzake hadhuriki wala hasumbuki kwa namna
yoyote ile.

Chini ya wajibu huu, kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha kuwa mwenzake hadhuriki wala
kusumbuka kwa namna yoyote ile kutokana na kitendo anachofanya au ambacho anaweza
kukizuia kisifanyike. Mfano wa uvunjifu wa wajibu huu ni kama mtu kuingia kwenye eneo / mali
ya mtu mwingine isivyo halali na kufanya mwenzie ashindwe kutumia, kuendeleza au kafanya
kazi katika eneo hilo; au mtu kusababisha uchafu kwenye eneo/ mazingira ya mtu mwingine au
kuwa na mali ambayo inaleta uchafu kwenye eneo la mtu mwingine; au mtu kupata madhara
binafsi au mali yake kutokana na mnyama/ mifugo ya mtu mwingine; au Ikiwa mtu amepata
hasara/ madhara binafsi au mali yake kutokana na uzembe wa mtu mwingine au Ikiwa mtu
alikuwa anasafisha shamba au eneo lake kwa kuchoma moto na moto ule ukasambaa hadi
kwenye eneo la mtu mwingine na kusababisha madhara kwenye eneo hilo.
Kitu cha kuzingatia kutokana na Makala hii ni kwamba kila mtu ana wajibu wa kujali na
kuhakikisha kuwa kitendo chochote anachofanya hakisababishi madhara hasi kwa mwenzake.
Tukutane katika Makala nyingine!!!


Comments