Coronavirus: Hatua zinazochukuliwa na Afrika mashariki dhidi ya virusi vya corona

tANZANIA CORONA
Nchi za Afrika mashariki zimekumbwa na virusi vya Corona na kumekuwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa ili kupambana na hali hiyo.
Ni Burundi pekee ndio haijatangaza kuwa na maambukizi ya Corona.
Taarifa hii inaangazia ni namna gani nchi hizo zinavyopambana kuzuia kasi ya maambukizi ya Corona.

Uganda

Uwanja wa ndege wa UgandaHakiAFP
Mamlaka ya Uganda imetangaza mtu wa kwanza kukutwa na maambukizi ya virusi vya Corona na sasa nchi hiyo inawafuatilia abiria 84 ambao waliwasili na ndege ya shirika la ndege la Ethiopian.
Mwanaume mwenye umri wa miaka 36 aliyekwenda Dubai kwa shughuli za biashara Machi 17 ndio raia kwanza wa Uganda kubainika rasmi kuwa mwathirika wa Corona.
Wamewataka abiria wote waliosafiri naye warudi kupima .
Siku ya jumamosi , waziri wa afya, Ruth Jane Aceng alisema kuwa wote wako karantini kwa ajili ya uangalizi wa karibu.
Hata hivyo abiria hao wametakiwa wajitenge.
Wakati haya yakijiri, rais Yoweri Museveni ametoa agizo mipaka yote ifungwe kwa watu wote wanaoingia au kutoka. Agizo hilo lilitakiwa kuanza kutekelezwa saa sita mchana siku ya Jumapili.
Abiria waliopanga kuja au kuondoka Uganda wamejikuta mashakani. Hapo awali raia wa Uganda na Kenya waliruhusiwa kuvuka mipaka ya nchi hizo mbili, vivyo hivyo kwa wale waliokuwa wakitokea Tanzania.
Ila raia wengine wa kigeni hawakuruhusiwa lakini kwa sasa hakuna mtu anaruhusiwa kuvuka iwe kwa miguu, ndege au vyombo vya majini.
Mawakala wa mabasi yanayosafirisha watu Afrika Mashariki wame lazimika kusimasisha shughuli zao.

Vyombo vyote vya dola nchini Uganda vimeagizwa kuhakikisha kuwa maagizo ya kukabiliana na COVID-19 yanazingatiwa na wananchi.
Miongoni mwa hayo ni kutoshiriki katika mikusanyiko ya ibada, sherehe na maziko.
Agizo hilo lilianza kutekelezwa mara moja na maafisa wa wilaya mipakani , abiria kadhaa ikiwemo raia wa Congo na Burundi walikuwa wamekwama kwenye mpaka kati ya Uganda na Rwanda.
Kutokana na maagizo hayo, mapadre wawili nchini Uganda ambao waliokutwa wanaongoza misa wamekamatwa kwa kosa ya kukutanisha mikusanyiko ya watu wakati imekatazwa.
Padre mmoja wa kanisa Katoliki amesema kuwa alirekodi kwenye televisheni tu hakukuwa na misa lakini mashaidi wanasema kuwa kulikuwa na mikusanyiko ya watu.
Hata hivyo kundi moja la raia wa kigeni ikiwemo Wachina waliojaribu kukwepa hatua hiyo wamekamatwa na kuzuiliwa tena.

Rwanda

Rwanda
Rwanda imefunga mipaka yote ya nchi hiyo na watu kuamrishwa kusalia majumbani mwao katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Hatua zingine zilizochukuliwa ni pamoja na watumishi wote wa serikali na wa kibinafsi kufanyia kazi nyumbani na safari za kwenda mikoani kusitishwa kwa wiki mbili kukiwa na uwezekano wa muda huo kuongezwa.
Vilabu vya pombe na, maduka yasio ya chakula pia yamefungwa huku usafiri wa bodabobda ukisitishwa.
Hatua hiyo inajiri siku moja baada ya wizara ya afya ya Rwanda siku ya Jumamosi kutangaza kuwa watu wengine sita wameambukizwa virusi vya corona miongoni mwao mtoto mchanga wa miezi 10.
Maambukizi hayo yanaifanya Rwanda kuwa na idadi ya visa 17 vya maambukizi ya virusi vya Corona.
Wananchi waliokuwa na hofu wameonekana wakinunua bidhaa za chakula huku baadhi yao wakihofia hali itakuaje.
Hatua zilizochukuliwa na Rwanda kudhibiti virusi vya Corona ni kufungwa kwa shule zote za umma na za kibinafsi, maeneo ya kuabudu na sehemu zote za umma.
Matukio kama vile mikusanyiko ya watu katika maeneo ya michezo na harusini vimeahirishwa na wale waliopoteza wapendwa wao watazikwa kwa namna ya kipekee.
Shirikisho la Soka la Rwanda(FERWAFA), pia limetangaza kwamba michuano yote kwa sasa itafanyika bila kuhudhuriwa na mashabiki katika viwanja vya michezo, huku shirikisho la mpira wa mkono nchini humo likiahirisha michezo yake yote.
Maeneo ya umma na maeneo yote ya utoaji wa huduma yameagizwa kuweka vitakasa mikono kwa ajili ya umma unaotembelea maeneo hayo.
Raia wamehimizwa kukaa nyumbani na kuepuka matembezi yasiyo ya maaana na kunawa mikono mara kwa mara kwa muda wa sekunde 20.
Hakuna abiria atakayeruhusiwa kusimama na kutoa wito kwa watu wa eneo na vikosi vya usalama kusaidia kuhakikisha hatua hizo zinatekelezwa.

Kenya

KenyaHakiGETTY IMAGES
Kenya ikiwa imefikisha idadi ya watu 15 walioambukizwa virusi hivyo hatari vya Corona.
Kuanzia sasa maduka makubwa yameagizwa kudhibiti idadi ya wateja, kipaumbele kikipewa wanawake wajawazito, wazee na walemavu.
Maeneo ya burudani kufungwa ifikapo saa moja na nusu usiku kuanzia leo Jumatatu awali maeneo ya burudani yaliruhusiwa kuhudumu hadi saa tano usiku.
Hatua nyingine za dharura zilizochukuliwa kuanzia jumapili ni wenye hoteli wataruhusiwa kuuza chakula cha kwenda kula nyumbani.
Huduma za ibada makanisani na misikitini zimesitishwa huku mazishi yakiruhusiwa kuhudhuriwa na familia ya marehemu pekee.
Sherehe za harusi pia zimepigwa marufuku.
Masharti mengine ya kuzuia maambukizi Kenya ni pamoja na ndege za kimataifa zitasitishwa kuanzia Jumatano Machi 25 isipokuwa ile ya kubeba mizigo.
Wageni wote wanaongia nchini kutoka mataifa yaliyoathiriwa watalazimika kujitenga binafsi kwa gharama zao.
Wakenya katika mataifa ya kigeni wametakiwa kufuata muongozo wa nchi husika na atakayekiuka maagizo ya karantini atakamatwa.

Tanzania

tANZANIA
Wakati kwa upande wa Tanzania , juhudi za kudhibiti kuenea kwa maaambukizi Rais Magufuli amesema kuanzia Jumatatu, wageni wote watakaoingia nchini humo kutoka mataifa yaliyo na visa vya ugonjwa huo watatengwa kwa siku 14 kwa gharama zao.
Agizo hilo linawajumuisha Watanzania wanaorejea nyumbani kutoka nchi zingine.
Hatua nyingine zilizochukuliwa kudhibiti maambukizi ni kufungwa kwa shule zote pamoja na vyuo kwa siku 30 ikiwa ni hatua ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya corona nchini humo.
Pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ya watu wengi yakiwemo matamasha ya muziki, mikutano ya hadhara mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.
Aidha Tanzania imekuwa tofauti kidogo baada ya rais kusema kuwa hatofunga makanisa wala misikiti.
''Nimeanza kuwa na wasiwasi kwamba imefika mahali hata watu wanamsahau Mungu kwamba Mungu ndiye mponyaji wa kweli katika maisha yetu, ile tuweze kushinda hili balaa lakini pia tunachukua tahadhari.'' aliongezea kusema.
Aidha Bw. Magufuli alisema kuwa ana matumaini kuwa janga hilo litapita.
''Tuchape kazi, tuendelee kumuomba Mungu. Tusitishane, tusiogopeshana. Natoa wito kwa ndugu zangu wanaoandika mitandaoni kwa sababu kila mmoja amekuwa akiandika lake. Mengine wanapeleka kama mzaha. Huu ugonjwa sio wa kufanyiwa mzaha.''

Tanzania pia haijachukua hatua katika upande wa idadi ya abiria wa usafiri wa umma wala kufunga mipaka.
Ingawa kwa upande wa visiwa vya Zanzibar, baadhi ya ndege za moja kwa moja za barani ulaya zimesitishwa.

Comments