Coronavirus: Wataalamu wanasema nini kuhusu wenye matatizo ya kiafya?


Watu walio na umri mkubwa wako hatarini kupata maambukizi

Virusi vya corona vinaweza kumuathiri yeyote,lakini watu wenye matatizo ya kiafya na wazee wanadhaniwa kuwa katika hatari ya kuathirika zaidi na dalili zake.
Ikiwa una ugonjwa wa muda mrefu unaweza kuwa na wasiwasi, hivyo basi huu ndio ushauri wa wataalamu.
Ni nani hasa aliye hatarini?
Kuwa na tatizo la kiafya haikufanyi wewe kuwa mtu anayeweza kupata maambukizi ya coronavirus kuliko mtu mwingine yeyote.
Lakini inaonekana watu wenye umri mkubwa zaidi (wazee), wale ambao mfumo wao wa kinga ya mwili umedhoofika na watu wenye magonjwa ya kudumu ukiwemo moyo, kisukari, au pumu wana hatari zaidi ya kuathiriwa.
Watu wengi huanza kupona haraka coronavirus baada ya kupumzika kwa siku kadhaa. Kwa baadhi ya watu , inaweza kuwasababishia kuugua sana na wengine hata kutishia maisha yao. Dalili zake ni sawa na za magonjwa mengine ambayo ni ya kawaida, kama vile mafua na homa:
  • kikohozi
  • joto la juu ya mwili
  • kushindwa kupumua
Watu walio katika hatari kubwa ni pamoja na wale wenye umri wa zaidi ya miaka 70, iwe wana ugonjwa wa kudumu au la, na watu wenye chini ya miaka 70 wenye maradhi ya muda mrefu.
  • Maradhi ya kudumu ya mfumo wa kupumua, kama vile pumu
  • Ugonjwa wa moyo wa kudumu kama vile, kiharusi
  • Ugonjwa wa kudumu wa figo
  • Ugonjwa wa kudumu wa ini
  • Ugonjwa wa kudumu wa neva, kama Parkinson , na mengine
  • Seli mundu
  • Mfumo dhaifu wa kinga ya mwili kutokana na maradhi kama HIV na Ukimwi, na wakati unapotumia tiba kama tembe za steroid au tiba ya mionzi
  • Unapokua na uzito wa mwili wa kupindukia
  • Wale wenye ujauzito
Kila mtu anaambiwa kufuata hatua za kutosogeleana na mtu mwingine ili kusaidia kupunguza uwezekano wa kuambukizwa na kusambaza coronavirus.
Watu walio katika hatari kubwa wanashauriwa kufuata ushauri huu kikamilifu.
Takriban watu milioni 1.5 wenye matatizo makubwa, kama vile wagonjwa wanaopokea tiba ya saratani au watu wanaoongezewa kinga ya mwili,wanaombwa kujitenga nyumbani kwa wiki walau 12 ili kujilinda na maambukizi nchini Uingereza.
Nina maradhi ya pumu, ninapaswa kufanyanini?
Wagonjwa wa pumu wanashauriwa kutumia inhaler ya kuzuia (ambayo kwa kawaida ina rangi nyekundu ) kila siku kama walivyoagizwa na daktari. Hii itakusaidia kupunguza hatari ya shambulio la pumu linaloweza kusababishwa na virusi vya aina yoyote vinavyoweza kushambulia mfumo wa kupumua , vikiwemo coronavirus.

Watu walio na maradhi ya pumu wametakiwa kuwa makini kuepuka maambukiziHakiGETTY IMAGES
ImageWatu walio na maradhi ya pumu wametakiwa kuwa makini kuepuka maambukizi

Tembea na inhaler yako ya rangi ya bluu kila wakati, ili utakaposikia dalili ya shambulio la pumu uitumie mara moja. Kama pumu yako itakuwa mbaya zaidi inaweza kua una coronavirus, na hivyo basi unatakiwa kupiga simu kwenye namba za huduma za tiba ya coronavirus katika nchi yako ili upate ushauri zaidi wa kitaalamu.
Mimi ni mzee, je ninapaswa kujitenga binafsi?
Kila mtu bila kujali umri -anapaswa sasa kuepuka mikusanyiko au kukaribina na mtu mwingine bila sababu ili kusaidia kuzuia kusambaa kwa virusi na kuwalinda walio katika hatari zaidi ya kupata maambukizi. Hiyo ina maana kwamba epuka kukutana na marafiki na familia pamoja na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.
Hii ni muhimu hasa kwa watu wenye umri wa miaka zaidi ya 70 na wale wenye magonjwa ya kudumu kwasababu wako katika hatari kubwa ya kupata dalili mbaya iwapo watapatwa na maambukizi ya coronavirus .

Maelezo zaidi

Nina ugonjwa wa kisukari, nifanye nini?
Wale wanaoishi na ugonjwa wa kisukari wa aina ya 1 au aina ya 2 wanaweza kuwa katika hatari kubwa ya kuugua sana. Dan Howarth mkuu wa kituo cha huduma kwa wagonjwa wa kisukari nchini Uingereza - Diabetes UK, anasema: "Coronavirus au Covid-19 inaweza kusababisha matatizo makubwa kwa wagonjwa wa kisukari.
"Kama una ugonjwa kisukari na una dalili kama vile kikohozi, joto la juu la mwili na unahisi unashindwa kupumua vizuri, unahitaji kufuatilia kwa karibu sukari yako mwilini."
Kama una dalili hizi unapaswa kukaa nyumbani kwa siku saba na uendelee kutumia dawa zako. Usiende kwa daktari wako, kwenye duka la dawa wala hospitali, hata kama ulipaswa kumuona daktari wako. Kama unahisi hali yako inaendelea kuwa mbaya na huwezi kuvumilia piga simu kwa taasisi inayoshughulikia coronavirus nchini mwako.
Kama hauna dalili zozote za coronavirus na unataka kuhudhuria kliniki ya kawaida ya kisukari, angalia ikiwa unaweza kufanya hilo kwa njia ya simu au mtandao badala ya kutembelea hospitali au kliniki mwenyewe ili kuepuka hatari ya maambukizi.
Je wanawake wajawazito wanasababu ya kuwa na hofu?
Hakuna ushahidi bado kwamba wanawake wajawazito na ( watoto wao wachanga) wako katika hatari kubwa iwapo watapatwa na coronavirus, lakini serikali inasema wakinamama wanapaswa kuwa waangalifu zaidi kwa sasa. Kama ilivyo kwa mtu mwingine yeyote yule ambaye anaweza kuwa katika hatari ya kuambukizwa , umesema ushauri rasmi.

Ninavuta sigara, je ninakabiliwa na hatari kubwa?
Deborah Arnott, mkurugenzi mkuu wa misaada ya kiafya nchini Uingereza, Ash, anashauri wale wanaovuta sana sigara wanapaswa kupunguza au kujaribu kuacha kabisa uvutaji wa sigara ili kupunguza hatari iwapo watapatwa na coronavirus.
"Wavutaji wa sigara wana uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya mfumo wa kupumua na wana uwezekano mkubwa mara mbili wa kupata maradhi ya mapafu- pneumonia kuliko wasiovuta sigara ," alisema.
Inashauriwa kuwa hata kama haujihisi vema iwapo una magonjwa ya kudumu uendelee kutumia dawa ulizopewa za matibabu pale unapopatwa na coronavirus. Kama unahitaji kuchukua dawa muombe rafiki yako au mtu wa familia yako akuchukulie.

Unachotakiwa kuzingatia
ImageUnachotakiwa kuzingatia

Je ninahitaji dawa ya kinga ya mafua?
Coronavirus ni tofauti kabisa na mafua ya kawaida, kwa hiyo dawa ya mafua haitakuzuia kupata maambukizi, lakini mafua pia yanaweza kukufanya uugue na yanaweza kuwa mabaya sana kwa baadhi ya watu.
Kwa hiyo ninawezaje kuwa salama?
Virusi vinasemekana kuwa husambazwa kwa kikohozi na kwa njia ya kugusa sakafu au vifaa vyenye virusi, kama vile vyuma vya kando ya ngazi katika nyumba za magorofa, na nyingine, na vitasa vya milango katika maeneo ya Umma.
Usafi mzuri unaweza kuzuia kusambaa kwa :
  • Funika pua yako na mdomo na tishu au sehemu ya juu ya mkono wako unapokohoa au kupiga chafya.
  • Weka tishu ulizotumia kwenye debe la takataka mara moja
  • Nawa mikono yako kwa sabuni na maji mara kwa mara-tumia vitakasa mikono (Sanitizer) wakati maji hayapo
  • Jaribu kuepuka kusogeleana na watu hasa wale ambao wanaumwa
  • Usiguse macho yako, pua au mdomo iwapo mikono yako sio misafi
  • Usijibweteke fanya mazoezi ya mwili ndani ya nyumba yako au katika bustani kama inawezekana

Comments