Mfanyakazi wa serikali Souhayata Haidara anafurahia kuzungumza kuhusu maisha yake katika jamii ya mfumo-dume. Taaluma yake ni ushindi wa subira na ukakamavu, anaambia Afrika Upya akitabasamu na kupepesa.
Bi. Haidara, ambaye ni Mshauri Maalum wa Waziri ya Mazingira na Maendeleo Endelevu wa Mali, anasema kwamba alibahatika kutoolewa akiwa na miaka 14 kama wenzake. Baba yake alipinga shinikizo kutoka kwa waliokuja kumposa na aila yake na akasisitiza kwamba kijana huyo akubaliwe kuhitimisha elimu ya sekondari kabla ya kuolewa. “Katika utamaduni wetu, watu wanaamini kwamba elimu ni ya wavulana na kwamba sharti wanawake waolewa na kusalia nyumbani,” anasema.
“Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi umekitwa katika elimu,” asema Bi. Haidara, ambaye alituzwa shahada katika Sayansi ya Mazingira huko Marekani kwa msaada wa masomo kutoka kwa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa. “Singekuwa nilipo sasa bila elimu. Ninapata mapato. Niliwasomesha wanangu watatu — mvulana na wasichana wawili, ambao ni watu wazima sasa. Nina mjukuu wa kike wa miaka sita anayepata gredi nzuri darasani. Hilo linanifurahisha.”
Ila Brandilyn Yadeta, Mhabeshi wa miaka 32, hakupata elimu. “Nilimpata mtoto nikiwa na miaka 19 na babake akasafiri ng’ambo bila kunijuza. Tangu wakati huo ninapambana kumtunza mwanangu, ambaye ni muhimu sana kwangu kuliko elimu yangu.” Yeye ni mfanyabiashara mdogo.
Ikiwa baba atakataa kulipa pesa za kumtunza mwanawe, mwanamke ana chaguo lipi? “Ninaweza kufanya nini?” Bi Yadeta auliza kwa majuto na kutamauka.
Bi. Yadeta na wengine kama yeye barani Afrika ni mashujaa wasiotambuliwa — kwa kuitunza familia, kazi isiyothaminiwa na jamii zao. Kwa vipimo vya pesa, kazi isiyolipiwa ya wanawake hujumuisha kati ya 10% na 39% kwa mapato ya nchi, kulingana na Taasisi ya Uchunguzi wa Maendeleo ya Kijamii ya Umoja wa Mataifa, ambayo hutoa sera ya uchunguzi kuhusu masuala ya maendeleo.
Shirika la Kimataifa la Wafanyakazi lasema kuwa wanawake wamezongwa na jukumu kubwa la kutunza kusikolipiwa na kazi za nyumbani. Linaonyesha hili ili kushadidia haja ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, ambayo ndiyo mada muhimu sasa katika maandishi kuhusu maendeleo.
Mataifa ya Afrika yaliyo chini ya Jangwa la Sahara yaongoza katika mageuzi
Ripoti ya Benki ya Dunia yenye mada Wanawake, Biashara na Sheria 2019: Mwongo wa Mageuzi yaeleza kwamba mataifa yaliyo chini ya Jangwa la Afrika, “yalishuhudia mageuzi mengi kukuza usawa wa kijinsia [kuliko maeneo mengine yote].” Kwa kweli sita kati ya nchi 10 zinazofanya mageuzi ziko eneo hilo — Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Gine, Malawi, Morisi, Saotome na Prinsipe, na Zambia.
Licha ya mgogoro wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliimarika zaidi kufuatia “mageuzi yanayowakubalia wanawake kusajili biashara, kufungua akaunti za benki, kutia sahihi mikataba, kupata ajira na kuchagua pa kuishi kama wanaume,” ripoti hiyo ilisema.
Morisi ilianzisha tiba za kiraia kwa dhuluma za kimapenzi kazini na ikaharamisha ubaguzi wa kijinsia kwa mikopo. Tiba za kiraia zinajumuisha kuzuia waajiri kumdhulumu mfanyakazi au mtafuta kazi ilhali mfanyakazi hastahili kumdhulumu mwenzake. Morisi iliamrisha malipo sawa kwa wanaume na wanawake kwa kazi zenye hadhi sawa.
Saotome na Prinsipe ilisawazisha umri wa lazima wa kustaafu na miaka ya wanaume na wanawake kupata malipo yote ya uzeeni—hatua iliyoimarisha ushiriki wa huduma za wanawake katika nchi hiyo kwa 1.75%.
Ripoti ya Benki ya Dunia haipendekezi kwa vyovyote kwamba hali ni nzuri kwa wanawake katika nchi hizi. Ripoti hiyo inaonyesha tu ongezeko la mabadiliko chanya ambayo mataifa yanafanya.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa mfano, yaweza kuwa imetekeleza baadhi ya mageuzi ya kuwawezesha wanawake, lakini wanawake katika nchi hiyo hawana haki za kurithi shamba, kulingana na shirika la misaada la Global Fund for Women.
Theodosia Muhulo Nshala, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake, shirika la misaada Tanzania aliambia Afrika Upya kwamba “wanaume na wanawake [nchini Tanzania] wana haki sawa kumiliki shamba kulingana na Sheria ya Kijiji kuhusu Shamba 1999; hata hivyo, kuna sheria za kimila zinazowazuia wanawake na wasichana kurithi shamba kutoka kwa waume zao na baba zao.”
Ingawaje ushiriki wa wanawake katika nguvukazi (hasa katika sekta zisizo rasmi) ni wa kiwango cha juu katika mataifa mengi chini ya Jangwa la Sahara—86% nchini Rwanda, 77% Uhabeshi na 70% Tanzania — ni katika nchi nane pekee (Gabon, Ghana, Kenya, Libya, Namibia, Afrika Kusini, Uganda na Zimbabwe) ambako 50% ya wanawake wanamiliki akaunti za benki, kulingana na Global Financial Inclusion Database, ambalo huchapisha vigezo vya kitaifa vya ujumuishi wa kifedha mara kwa mara.
Si shughuli isiyo na manufaa
Kuwawezesha wanawake kiuchumi si shughuli isiyo na manufaa ambapo wanawake hufaidika huku wanaume wakihasirika, yasema Urban Institute, jumuiya ya washauri mabingwa kuhusu sera katika Washington, D.C. Badala yake, kuendeleza usawa wa wanawake, ukuaji wa mapato ya kimataifa ya kila mwaka waweza kupigwa jeki kwa trilioni $12 au 11% kufikia 2025, kulingana na kampuni ya ushauri kuhusu usimamizi iliyoko Marekani ya Mckinsey Global Institute.
Na Kitengo cha Masuala ya Wanawake cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kinasema: “Kuwekeza katika kuwawezesha wanawake kiuchumi huelekeza moja kwa moja kwa usawa wa kijinsia, kuuangamiza umaskini na ukuaji jumuishi wa uchumi.”
“Kwa upande mwingine, tangu 2014 chumi za Afrika chini ya Jangwa la Afrika zimepoteza takribani bilioni $95 kila mwaka kwa sababu ya pengo la kijinsia katika soko la huduma,” asema Ahunna Eziakonwa, Mkurugenzi wa Ofisi ya Kieneo Afrika ya Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP). “Kwa hivyo, fikiria ikiwa utawachilia uwezo, talanta na ushupavu wa wanawake.”
Wataalamu wanaamini kwamba uwezeshaji wanawake kiuchumi ndio njia ya kutimiza Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika, mfumo wa bara zima wa mabadiliko ya kiuchumi na kijamii barani, pamoja na malengo mengine katika Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa. Hayo yanajumuisha Lengo la 1, kuangamiza umaskini; Lengo la 2, kutimiza usalama wa chakula; Lengo la 3, kuhakikisha afya; Lengo la 5, kutimiza usawa wa kijinsia; Lengo la 8, kuendeleza ajira kamilifu na zenye manufaa pamoja na kazi za heshima kwa wote; na Lengo la 10, kupunguza ukosefu wa usawa.
Tamanio la 6 la Ajenda 2063 linaazimia “Afrika ambayo maendeleo yake husukumwa na watu, yanayotegemea uwezo wa watu, hasa wanawake wake na vijana, na kuwatunza watoto.”
Kuchukua hatua
Mataifa yanaweza kufanya nini kuwawezesha wanawake kiuchumi?
Katika blogu kwa manufaa ya Benki ya Dunia, Waziri wa Fedha, Mipango na Utawala ya Umma wa Kapuvede Cristina Duarte na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia wa Miundomsingi Makhtar Diop hivi karibuni walihimiza “usaidizi (kwa) wanawake wachanga katika kipindi cha kuvunja ungo — awamu muhimu ya maisha yao.” Mpango wa Uwezeshaji na Riziki za Vijana katika Uganda, ambao “hutumia vilabu vya wasichana pekee kutoa mafunzo ya kiufundi na mafunzo ya ‘stadi za maisha’,” ni mfano bora, kulingana na Bi Duarte na Bwana Diop.
Benki ya Dunia inapendekeza, miongoni mwa hatua nyingine, upitishaji wa sheria zinazoendeleza ujumuishaji wa kiuchumi. Bi. Eziakonwa anaamini kwamba mataifa yanastahili kuondoa sheria ambazo ni vikwazo kwa wanawake, pamoja na zile zinazowazuia kumiliki shamba. Mwanahabari wa Afrika Kusini Lebo Matshego anawahimiza wanaharakati wa haki za wanawake kutumia mitandao ya kijamii kushawishi dhidi ya mila na tamaduni zinazovunja haki za wanawake.
Vera Songwe, mkuu wa Tume ya Kiuchumi kwa Afrika, mwanamke wa kwanza kuongoza shirika hilo, asema wanawake, hasa wa mashambani, wanahitaji mtandao ili waweze kunufaika na teknolojia mpya.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika ripoti yake ya CSW ya 2018 yenye mada: Changamoto na nafasi katika kutimiza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake wa mashambani na wasichana anahimiza mataifa “kubuni na kutekeleza sera za kifedha zinazoendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake wa mashambani na wasichana kwa kuwekeza katika miundomsingi muhimu (Teknohama, nishati endelevu, uchukuzi endelevu na usafi wa maji).”
Kulingana na Ellen Johnson Sirleaf, aliyekuwa Rais wa Liberia, azimio la usawa wa kijinsia ndio mwelekeo bora. Asema, “sasa ndio wakati wa kuwapendelea wanawake,” kama mapendeleo katika ajira na mikopo.
Kitengo cha Umoja wa Mataifa cha Masuala ya Wanawake kiliunga mkono mageuzi ya zabuni za ununuzi za umma nchini Kenya mwaka wa 2013, na sasa Kenya huwatengea wanawake angalau 30% ya matumizi ya kila mwaka ya serikali. Katika 2017, kupitia kwa Mpango wake wa Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi, Kitengo cha Umoja wa Mataifa cha Masuala ya Wanawake kiliripoti kuwapa mafunzo kwa ufanisi wachuuzi wa kike 1,500 Nairobi kushiriki na kunufaika na mfumo wa ugavi wa serikali. Huu ni mfano mmoja wa hatua zinazooana na pendekezo la Bi. Sirleaf.
“Ubora wa kazi wazifanyazo wanawake ni muhimu pia,” aandika Abigail Hunt, mtafiti wa jumuiya ya washauri mabingwa ipatikanayo Uingereza, Overseas Development Institute. “Uwezeshaji ni mdogo wakati wanawake wanapojiunga na soko la nguvukazii kwa malipo mabaya. Na hili linahusisha wanawake kuhusishwa katika kazi za unyonywaji, hatari na zilizonyayapaaishwa, kwa malipo madogo na ukosefu wa usalama wa kazi.” Kwa maneno mengine, wanawake wanahitaji ajira za malipo ya juu, salama na za kudumu.
“Safari ya kuelekea kwa uwezeshaji kiuchumi wa wanawake haiwezi kubadilishwa,” asisitiza Bi. Sirleaf, “inachukua muda mrefu, ila inakuja; hapana wa kuizuia.”
Comments
Post a Comment