KWA MATOKEO MAZURI JIFUNZE NJIA ZA KITAALAMU ZA USAFIRISHAJI NA UPANDIKIZAJI WA VIFARANGA VYA SAMAKI
Godfrey, Christopher Sway
Mtaalamu wa samaki kutoka
Sokoine University of Agriculture
+255752799673 / 0655859810.
Mtaalamu wa samaki kutoka
Sokoine University of Agriculture
+255752799673 / 0655859810.
UTANGULIZI
Mbegu za samaki (vifaranga) ni vifaranga vya samaki ambavyo vinapatikana kwa njia tofauti tofauti kulingana na namna mkulima mwenyewe ataamua. Njia ya kwanza ni ile ya samaki kuzaliana wenyewe bwawani wanapofikia umri wa kuzaliana wenyewe kwa wenyewe. Samaki hawa (brooders) ambao wanakua ni madume na majike wanaweza kuzaliana bila ya mfugaji au mkulima kuhusika katika kuwaandalia samaki hawa mazingira ya kuzaliana. Kwenye njia hii pia mkulima anaweza kuhusika katika kuandaa mazingira mazuri ya samaki kuzaliana kwa kuwatenga kwenye mabwawa tofauti na wengine. Samaki wakubwa wanaotengwa kwa ajili ya uzalishaji wa vifaranga wanapaswa kuwa na maumbo makubwa wote (madume na majike) ili waweze kuzalisha vifaranga wenye maumbo makubwa na wanaokua haraka. Brooders hutengwa kwenye mabwawa tofauti na wengine kwa ajili ya kupata nafasi nzuri ya kuzaliana. Samaki hawa (brooders) wanawekwa bwawani kwa uwiano wa 1:2 yaani dume moja kwa majike mawili au uwiano wa 1:3 yaani dume moja kwa majike matatu. Njia nyingine ni ile ya kuchukua mayai ya samaki baada ya kua yamerutubiswa na kuyaweka kwenye chumba maalumu (incubator) ambacho kinakua na joto zuri maji ya kutosha yenye oxijeni kwa siku tano hadi saba ambapo mayai ya samaki yataanguliwa. Njia hizi mbili zinatumika hasa kwa samaki aina ya perege ambao wanazaliana sana kwenye babwawa. Njia ya tatu ni ile ya kutumia hormone ya pituitari ambayo inatumika kwenye uzalishaji wa samaki aina ya kambale ambao kwa kawaida yao hawazaliani kwenye mabwawa au maji yalioyotuama. Katika utangulizi huu nimeelezea uzalishaji wa vifaranga vya samaki ambao asili yake wanafugwa kwa kiasi kikubwa kwenye maji ya baridi kama vile mito, maziwa, chemichemi, mabwawa, hapas, RAS, au kwenye vizimba (cages).
USAFIRISHAJI WA VIFARANGA VYA SAMAKI
Wafugaji wengi hasa wale wanaoanza mradi wa ufugaji samaki hua wanajiuliza maswali mengi sana kama vile ni wapi watapata vifaranga wazuri kwa ajili ya mbegu, na je ni namna gani nzuri ya kuweza kuwasafirisha toka eneo wanapo zalishwa hadi wanapoenda kupandikizwa (bwawani au shambani) Kwa wapenzi wasomaji wa makala zetu, leo tutafahamu namna nzuri na ya kitaalamu ya usafirishaji na upandikizaji wa vifaranga bwawani nakuweza kujibu maswali na changamoto unazopitia wakati unapowaza jinsi ya kuweza kusafirisha vifaranga wa samaki.
Upatapo vifaranga, visafirishe wakati wa asubuhi au jioni kabisa muda ambao joto linakua chini kwa kutumia ndoo ya plastiki, chungu, maplastiki makubwa (majaba). Pia kwa safari ndefu unashauriwa kubebea vifaranga ndani ya mifuko ya plastic ambayo utapatiwa na wauzaji wa vifaranga kama sehemu ya package kisha ndani ya mfuko huo kunaongezwa hewa ya oxijeni kuhakikisha uwepo wa oxijeni yakutosha kwenye maji kisha mfuko wa plastiki (transparent) unawekwa ndani ya ndoo au jaba.
Weka kiasi cha vifaranga 200 hadi 300 katika ndoo moja ya lita 20. Kiasi hiki cha vifaranga kwenye ndoo ya lita ishirini (20) huwa na nafasi yakutosha kabisa kwa kila kifaranga cha samaki kuweza kusafirishwa salama bila mshtuko (stress) hadi kwenye eneo lako.
Ufikapo bwawani, weka juu ya maji ya bwawa chombo ulichotumia kusafirishia samaki kwa dakika 15 -30 kisha inamisha ndoo ili maji ya kwenye ndoo yaingiliane na yale ya bwawani.
Hii ni kuruhusu joto la maji na mazingira ya maji yaingiliane na yale yaliotumika kusafirishia vifaranga na kuwa sawa.
Waruhusu samaki watoke bwawani wenyewe bila ya kuwamwaga. Itachukuwa muda kabla ya vifaranga wote kuingia bwawani. Kwa kufanya hivyo, samaki hawatapata mshituko ambao wanaweza kupata kama watamwagwa. Mshituko wa ghafla huweza kusababisha vifo.
UPANDAJI WA VIFARANGA VYA SAMAKI.
Ubora wa samaki utakao wafuga utategemea sana ubora wa vifaranga utakaokuwa umepanda bwawani. Hiki ni kiashiria kwamba mwanzo mzuri ndio utakupa matokeo mazuri sambamba kabisa na kutumia ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu walio bobea.
Chanzo chako cha vifaranga ni bora kiwe na vifaranga wenye umri mdogo na ambao hawajadumaa. Vifaranga wanapo dumaa huwa wanachukua muda mrefu sana kukua na mara nyingi inapelekea hasara kwa mfugaji kwani atakua anawalisha chakula kingi bila matokeo mazuri ya ukuaji hali ambayo itapelekea kuchukua muda mrefu kufikia saizi inayohitajika sokoni au mara nyingine kutofikia kabisa.
Kwa samaki aina ya Perege, panda vifaranga wanne (4) hadi watano (5) kwa kila mita moja ya mraba.
Aina ya samaki wanaofugwa kwenye maji ya baridi kwa kiasi kikubwa hapa Tanzania ni sato/perege na kambale.
Kwa sasa, samaki aina ya Perege ndio wanaofugwa na wafugaji wengi hapa nchini. Kwani aina hii ya samaki hupendwa sana na watu wengi na nyama yake ni laini pia samaki aina ya perege ni rahisi sana kuwaandaa kwa ajili ya kitoweo ukilinganisha na samaki wa aina nyingine kama vile kambale.
Kambale huweza kufugwa na mkulima mzoefu kwani huduma yake huitaji mtaji mkubwa katika
kuwalisha na Utaalam katika kuzalisha vifaranga vyake kwani samaki aina ya kambale hawazaliani wenyewewe kwenye mabwawa.
ULISHAJI WA SAMAKI.
- Samaki, Kama walivyo wanyama wengine, wanahitaji kula.
- Chakula cha samaki huweza kugawanywa katika makundi mawili:-
- Cha asili kipatikanacho ndani ya bwawa kama vile vijimea, vijidudu na samaki wadogo.
- Chakula cha ziada ambacho huongezwa bwawani na mkulima.
- Ili chakula cha asili kipatikane bwawani, ni vema bwawa liwe limerutubishwa vizuri, kwani vijimea vinavyotarajiwa humea palipo na rutuba.
- Chakula cha ziada huwekwa bwawani na mkulima mwenyewe. Aina ya chakula cha ziada hutegemea upatikanaji wake, gharama na aina ya ukubwa wa samaki. Baadhi ya chakula cha ziada ni kama: pumba za mahindi, za mpunga, mashudu ya pamba na karanga, mashudu ya alizeti, mahindi parazwa, dagaa sagwa, damu. soya bean, na mifupa kwa ajili ya madini na vitamini. machicha ya pombe, ugali na masazo ya jikoni, baadhi ya majani pori, majani yatokayo bustanini.
- Inashauriwa mfugaji alishe kila siku, kwa muda ule ule, saa ile ile na sehemu ile ile. Tabia hii hujenga mazoea ya samaki kula zaidi na kupunguza wingi wa chakula kinachopotea.
- Usilishe chakula kingi zaidi ya mahitaji ya samaki kwa siku hiyo. Mfano, usiweke debe zima la pumba kwa mara moja na kuacha kulisha kwa wiki nzima! Sehemu ya chakula kitakachosalia, kitaoza na baadhi ya siku samaki hawatakuwa na chakula, mwisho kupelekea maji ya bwawa kuchafuka kutokana na kuoza kwa chakula
Comments
Post a Comment