Watu kadhaa wanaosadikika kuwa ni Polisi wamevamia nyumba za wanachama wa CUF- Chama Cha Wananchi usiku wa jana kuamkia Leo huko Kibutuka Liwale na kupiga watu na kuwajeruhi vibaya baadhi yao, ambapo inaaminika mwanamke mmoja amefariki Dunia akiwa mikononi mwa Polisi baada ya mashambulizi hayo.
Kwa mujibu wa Taarifa za kuaminika kutoka Liwale, wanachama hao walivamiwa usiku baada ya mchana kushiriki kwenye Kikao Cha Ndani kilichoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bara Mheshimiwa Magdalena Sakaya ambaye yupo Mikoa ya Kusini kwa ajili ya Kukagua Uhai wa Chama.
Kwa mujibu wa Taarifa hizo, Polisi iliwakamata watu watano (5) huko Kibutuka na mmoja Liwale Mjini baada ya mashambulizi. Waliopigwa na kukamatwa ni Hussein Kwepu, Nassoro Pingili, Chande Uwangi, Aziza Kijumba( marehemu) na mume wa marehemu Mawazo Magumba, ambaye amejeruhiwa vibaya. Aliyekamatwa Liwale Mjini ni Salum Mtune.
CUF- Chama Cha Wananchi kinatoa pole kwa wafiwa na wote waliopatwa na mikasa hii ya ukandamizaji na kinamuombea marehemu Aziza Kijumba apate Mapumziko Mema.
CUF- Chama Cha Wananchi kinalaani mashambulizi haya na Ukiukaji wa Haki za Binadamu yanayoendelea Liwale tangu wakati wa Uchaguzi Mkuu uliovurugwa, ambapo watu kadhaa wameathiriwa na kadhaa wamebambikwa kesi mbaya na kufungiwa dhamana.
Tunatoa wito kwa Serikali na Vyombo vyake kukemea ukatili huu, kufanya Uchunguzi wa haraka na wa kina na kuchukua hatua stahiki kwa waliohusika na unyanyasaji na udhalilishaji huu unaolitukanisha Taifa.
HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!
Imetolewa leo Desemba 19, 2020 na:
Eng. MOHAMED NGULANGWA
Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF- Chama Cha Wananchi
Comments
Post a Comment