NI SHERIA UNAWEZA KUMSHAKI MCHUMBA WA AKURUDISHIE ZAWADI ZA KAMA MMEACHANA

 Una mahusiano na mwanaume au mwanamke  ambaye kimsingi mpo katika uchumba. Unampa zawadi nyingi naye anakupa zawadi.  Mnayo ahadi ya kufunga ndoa na kuishi kama mme na mke . Na kwasababu hiyo unajitoa sana kimatumizi kwa mtu huyo.

Lakini katika mazingira usiyoyaelewa unaona sasa mambo hayaendi vizuri. Hayaendi vizuri katika kiwango ambacho sasa mahusiano yamevunjika kabisa. Hakuna tena mahusiano. Au bado yapo lakini kwa mambo unayofanyiwa unaona kabisa hutakiwi tena.


Kumbuka huko nyuma umegharamia sana. Umegharamia kwa fedha na mali. Swali ni je vitu hivi haviwezi kurudishwa ?. Vitu hivi haviwezi kufidiwa ?. Na je sheria imeongelea kuhusu jambo hili ?.

Majibu ya maswali haya yote ni ndiyo. Ni ndiyo, na gharama pamoja nazo zawadi zinaweza kurejeshwa. Unaweza kushangaa kuona sheria imeongelea hata mambo ya uchumba lakini ndio ukweli.
Wengi tunaijua sheria katika kuongelea wizi, dhamana, mikataba, mirathi, ndoa, na mengine. Lakini ni vyema tukajua kuwa sheria ni pana na imeongelea mambo mengi mno. Hili la uchumba nalo ni sehemu ya yaliyoongelewa.

1 KUVUNJA UCHUMBA
.
Kifungu cha 69( 1 ) cha Sheria ya Ndoa iliyofanyiwa marekebisho 2010 kinasema kuwa mtu anaweza kufungua shauri na kudai fidia baada ya uchumba kuvunjwa.

Kwa haraka utaona kuwa tafsiri ya kifungu hiki sio kufungua shauri ili kumlazimisha mtu akurudie, hapana. Mahakama haiwezi kutoa maamuzi kuwa fulani lazima amrudie fulani. Isipokuwa lengo lake ni kumtaka yule aliyeumizwa katika hili kudai fidia kutokana na maumivu aliyoyapata. Hapa hatujaongelea kurudisha zawadi.

Kudai fidia na kurudisha zawadi ni vitu viwili tofauti. Fidia inahusu kulipwa maumivu uliyoyapata kutokana na tukio hilo la kuachwa pamoja na muda uliopoteza na huyo mtu. Wakati zawadi ni kurejesha kile ulichotoa. Kwahiyo la zawadi tutaliona baadae.

Aidha masharti ya kufungua shauri la kudai fidia ni kuwa , moja anayefungua shauri awe ni yule aliyeumizwa, pili ahadi ya kuoana lazima iwe ilikuwa imefanyika Tanzania, tatu wakati mnaingia kwenye mahusiano iwe mlikuwa nyote mmetimiza miaka 18 .

2. KURUDISHA ZAWADI.

Kifungu cha 71 cha Sheria ya ndoa kinasema kuwa mtu anayo haki ya kufungua shauri kudai kurejeshewa zawadi ambazo alizitoa kwa mtu ambaye alikuwa ana ahadi ya kufunga naye ndoa lakini ndoa haikufungwa.

Zawadi ni pamoja na fedha, nyumba, magari, nguo na kila kitu chenye thamani(valuable). Haijalishi mali hiyo ipo kwenye jina la nani suala la msingi ni kuthibitisha kuwa wewe ndiye uliyetoa hiyo zawadi.

Shauri la namna hiyo unaweza kulifungua mahakama yoyote ya mwanzo, ya wilaya, ya hakimu mkazi au hata mahakama kuu. Itategemea na thamani ya kiwango cha mali unazodai.

Kama mali hizo zitakuwa zimekwishatumika au hazipo tena pengine zimeuzwa au kutolewa zawadi kwa mtu mwingine basi itatakiwa kulipwa fedha zinazolingana na mali hizo au mali hizo zikanunuliwe tena kwingine ili kumrudishia anayedai.
Ukishindwa kabisa kurudisha basi mali zako binafsi ambazo hazikuwa sehemu ya zawadi zitauzwa ili kupata kiwango kinachodaiwa na kama huna mali yoyote ya kuuza utatakiwa kwenda jela kama mfungwa wa madai.

Kwa hiyo watu wanatakiwa waelewe kuwa uchumba na ahadi za kuoana si jambo jepesi kama wanavyolitamka na kuliahidi .

Comments