UKOMBOZI WA FIKRA KWA WATANZANIA

Siku moja mwanafalsafa Socrates aliwasha taa mchana kweupe na akaenda nayo kwenye soko la Athenes, kule Ugiriki. Pale sokoni wananchi wengi walimshangaa sana Socrates wakamuuliza; kwa nini amewasha taa sokoni wakati ni mchana na mwanga wa taa yake wala hauonekani kutokana na mwanga wa jua uliopo.


Socrates aliwajibu hivi, ‘’Pamoja na nuru hii ya jua lakini akili za watu wengi ziko kwenye giza nene’’.

Mamilioni ya Watanzania wako gizani. Uchumi wa Watanzania uko gizani. Elimu ya Watanzania iko gizani. Utalii wa Watanzania uko gizani. Kilimo cha Watanzania kiko gizani. Haki za Watanzania ziko gizani.

Maazimio ya Watanzania yako gizani. Watawala wako gizani. Watawaliwa wako gizani. Watanzania wako gizani. Wanatembea kwa kuona lakini hawatembei kwa dhati. Wanatembea kwa kuona lakini hawatembei kiuchumi. Wanatembea kwa kuona lakini hawatembei kielimu. Ni ajabu sana. Inasikitisha sana. Inatia huruma. Watanzania wamekaki kulalamika na kulaani. Siyo kosa lao.

Elimu aliyopata Mtanzania haijaweza kumkomboa kifikra. Bado Mtanzania yuko gizani katika mambo mengi sana. Mtanzania somo la falsafa limempita nyuma. Analisikilizia nyumba ya pili. Elimu yetu imewafanya baadhi ya Watanzania kuwa waoga wa kujenga hoja. Waoga wa kudadisi. Waoga wa kuhoji. Waoga wa kufikiria kwa muda mfupi na muda mrefu. Ukosefu wa fikra sahihi na bainifu kwa maisha ya mwanadamu yeyote yule ni ugonjwa. Ni ugonjwa usioonekana kwa vipimo vya kisayansi wala kienyeji lakini ni ugonjwa unaoua kwa haraka sana kuliko magonjwa mengine.

Ni ugonjwa unaoonekana kwa vitendo na kwa uamuzi mbalimbali. Watanzania tuko huru, lakini hatuko huru kwa upande wa kifikra. Ni katika mazingira haya tunaendelea kuzalisha kizazi kisichokuwa na maono ya kulijenga Taifa. Utafiti uliofanywa mwaka 2010 na asasi ya Marekani inayoitwa PEW Research Centre, ulibaini na kuonesha kwamba asilimia 93 ya Watanzania wanaamini katika ushirikina.

Akili za Watanzania ni kama mpira wa ngozi zinachezewachezewa. Haishangazi sana kila kona tunakopita tunakutana na vibao barabarani vya waganga wa kienyeji. Matangazo yao utaona yanasomeka hivi, “Dk. Bingwa kutoka Congo anatoa huduma zifuatazo: Kumrudisha mpenzi wa zamani, kuongeza nguvu za kiume, kuongeza akili za darasani, kumsahaulisha mdai wako, kuongeza mvuto kwa warembo, kupandishwa cheo kazini n.k.”

Kama kuna taifa lenye visa na mikasa basi Tanzania tunaongoza kwa visa na mikasa. Ama kweli Tanzania tumekuwa Taifa la kishirikina. Watawala wetu wanathamini ushirikina. Watawaliwa wanauthamini ushirikina. Tutainuka lini kiuchumi kama tunaamini katika ushirikina? Je, tutakaa tuliongoze Taifa letu kwa mbinu za kiushirikina? Tunawarithisha nini watoto wetu ambao ni Taifa la kesho? Kama vijana ni Taifa la kesho basi tunaandaa vijana watakaoliongoza Taifa hili kwa mbinu za kishirikina.

Tanzania tumekuwa Taifa la majaribio. Akili zetu zinajaribiwa. Mitazamo yetu inajaribiwa. Malengo yetu yanajaribiwa, jambo lolote la kutisha likitokea katika Taifa letu hatutafakari katika jambo hilo. Badala yake utasikia, mkuu wa nchi analaani vikali, waziri mkuu analaani vikali. Mawaziri na wabunge wanalaani vikali.

Wanaharakati wanalaani vikali. Kila mtu analaani vikali. Laana imekuwa laana. Kama kuna kipindi ambacho Tanzania inahitaji malezi ya kifalsafa ni hiki. Falsafa ni somo pana lenye uwezo wa kujenga fikra mpya katika jamii. Kila mwanadamu ni mwanafalsafa ingawa si kwa kiwango kinachofanana.

Elimu ya ukombozi wa kifikra ni zao la falsafa. Jambo ambalo hatuwezi kupinga wala kukwepa ni falsafa, ukweli, haki na mwanga. Jamii yoyote ile ni lazima itembee katika ukweli, haki, maadili, mwanga na elimu. Hakuna jamii inayoweza kuendelea pasipo watu wala kuwa na akili tafakari na akili bainifu. Si lazima kufuata falsafa ya watu wengine.

Falsafa itatujengea fikra pevu. Watanzania tunahitaji ukombozi wa kifikra tumekwama katika mengi, tumedumaa katika mengi, tumenyanyapaliwa katika mengi. Hatushituki? Hatutafakari?

George Benard Shaw alipata kuandika haya; “Maendeleo hayawezekani bila mabadiliko ya fikra na wale ambao hawawezi kubadilika namna wanavyofikiri hawawezi kubadili chochote”. Falsafa itatusaidia kuwa na maarifa yatakayotusaidia kufanya uamuzi sahihi kwa kufahamu lipi lifanyike na kwa namna gani, na kwa wakati gani, na lipi tuliache, na kwa nini tuliache.

Falsafa itatusaidia sisi wenyewe na watoto wetu kuwa watu wa tafakari ya kina. Baada ya kufikiri kuwa umaskini tulionao ni mapenzi ya Mungu, tutafikiri umaskini kama matokeo ya kutotumia vyema fikra zetu kwa usahihi katika mipango yetu.

Alfred Montapert alipata kuandika hivi; “Ukichagua kuchezea muda huwezi kukwepa matokeo yake ambayo siku zote ni mabaya tu.”

Hii ni karne ya kuwekeza katika muda wa kitafiti za kisomi. Tuwatumie wasomi wachache tulio nao katika kulikwamua Taifa letu kutoka kwenye hii hatua ya kiulimbukeni.

Natumia neno “wasomi wachache kwa sababu wasomi wenye fikra sahihi katika Taifa letu ni wachache…” Lakini wasomi wenye vyeti ni wengi kupindukia kimtazamo, kifalsafa na kisomi ni kwamba wasomi wa vyeti hatuwezi kuwahesabu kama wasomi na hatuwezi kuwaweka kwenye kundi la watu wenye upeo wa kisomi.

Hoja yangu hapa siyo kuchambua aina ya wasomi tulio nao bali ni kuonesha kwamba Tanzania kama Taifa kuna mahali tulikosea. Huu ni wakati wa kuanza upya. Tuchukue ushauri wa Mchungaji Henry Knox Sherrill [1890-1980] unaosema, “Habari njema kuwa amefufuka haibadilishi ulimwengu wa sasa. Bado mbele yetu kuna kazi, nidhamu na sadaka. Lakini ukweli wa Pasaka unatupa nguvu ya kiroho kufanya kazi, kukubali nidhamu, na kutoa sadaka.”

Ni kweli bado mbele yetu kuna kazi tena ngumu ya kulijenga Taifa letu. Huu ni wakati wa kuyatafsiri maisha kama kipindi cha mpito cha kufanya kazi, kujituma na kusonga mbele. Tusiogope. Tusonge mbele. Baba wa kiroho, Sai Baba, alipata kunena maneno haya yenye busara tuyatafakari:

Maisha ni wimbo-uimbe,

Maisha ni mchezo-ucheze,

Maisha ni changamoto-ikabili,

Maisha ni ndoto-ielewe,

Maisha ni sadaka-itoe,

Maisha ni upendo-ufaidi,

Maisha ni lengo-liingie,

Maisha ni kengele-igonge,

Maisha ni barabara-ipite,

Maisha ni mti-upande’’.

Watanzania kwa pamoja tufanye kazi ya kulijenga Taifa letu. Tanzania itajengwa na Watanzania. Tanzania yenye heri na neema itajengwa na Watanzania. Tanzania yenye amani, umoja na undugu itajengwa na Watanzania.

Napoleon alijenga tabia ya kuwaambia wanafunzi wake maneno haya, “Kila saa unayopoteza ni fursa ya kuwa na balaa baadaye.” Hii ni karne ya kuwa na mipango endelevu. Vipaumbele vinatuagiza; kuhesabu visivyohesabika. Kuwekea muda kinachoishi milele. Kuwekea umbo kisichoweza kuumbika. Kutafuta thamani ya kisichopimika. Kuwekea mipaka kisichokuwa na mwisho. Kuwekea taswira kisichoweza kuwa na sura. Kuanzisha kisicho na mwanzo. Kuingia duniani bila ya kuwa na dunia.

Mwanasayansi Albert Einstein alipata kushauri hivi, “Ukifikiri mwaka mmoja ujao panda mbegu. Ukifikiri miaka 10 ijayo panda mti. Ukifikiri miaka 100 ijayo elemisha watu”.

Mwanasayansi huyu alikuwa na maana hii, kwa kupanda mbegu utavuna mara moja. Kwa kupanda mti utavuna mara kumi. Kwa kuelimisha watu utajenga kizazi kinachojitambua.

Naye mwanafalsafa Anselm Stolz alipata kufundisha hivi, “Ukimpa mtu samaki atamla mara moja, lakini ukimfundisha kuvua atakula samaki kila siku”.

Watanzania samaki tulioletewa kwa kwa ajili ya kula wametosha. Na sasa tufundishwe namna ya kuvua samaki. Ni kweli alivyopata kusema mwanahabari mkongwe, Jenerali Ulimwengu, kwamba, “Leo lazima iwe bora kuliko jana, na kesho kuliko leo, la sivyo kuna tatizo’’. Tunataka kujenga kizazi cha kuona mbele.

Tunataka kujenga kizazi chenye uwezo wa kufikiri kwa upana “Reasoning generation”. Tunataka kujenga kizazi cha kuwajibika na si kizazi cha kulalamika. Tunataka kujenga kizazi chenye uwezo wa kuwakosoa viongozi wavivu, viongozi wasio na maono kwa Taifa letu, viongozi wasio na uzalendo na Taifa lao.

Tunataka Watanzania, Waafrika na walimwengu wote wawe na fikra mpya katika kuelewa na kupambanua mambo kwa ufasaha. Tunahitaji fikra mpya katika mipango yetu. Fikra mpya katika mahusiano yetu. Fikra mpya katika kuujua ukweli na kuuishi ukweli ulivyo na uhalisia wake. Muda wa akili ndogo kuitawala akili kubwa ulikuwa jana. Muda wa akili kubwa kuitawala akili ndogo ulikuwa jana.

Muda tulio nao sasa ni akili kubwa kushirikiana na akili ndogo ili kuliletea Taifa letu maendeleo. Sisi sote ni watoto wa Mungu. Kumbuka kwamba; Ukiwa maskini bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukiwa kijana bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukiwa mzee bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukiwa tajiri bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukiwa machinga bado wewe ni mtoto wa Mungu.

Ukiwa mfupi bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukichelewa kuolewa ama kuoa bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukifukuzwa kazi bado wewe ni mtoto wa Mungu. Ukiwa mrefu bado wewe ni wa Mungu

Comments