BAD VALENTINE
SIMULIZI FUPI : BAD VALENTINE
Niliamka asubuhi sana, baada ya kuoga na kuvaa suruali yangu nyeusi na tshirt nyekundu yenye michirizi meusi mabegani, niliingia stoo na kuchukua jembe, jembe ambalo lilikuwa limeanza kuota kutu kwa kutotumiwa muda mrefu.
Nilitoka nje na jembe langu mkononi, nilitembea kwa miguu taratibu kuelekea Sinza makaburini. Makaburi ambayo hayakuwa mbali sana na nyumbani kwangu nilipokuwa nakaa, Sinza kwa Remmy.
Nilifika Sinza makaburini, sehemu ambako kulikuwa na makaburi mengi sana. Nikatafuta kaburi nililokuwa nalihitaji miongoni mwa makaburi yale mengi, nililiona. Lilikuwa kaburi ambalo halijasakafiwa vizuri, lakini jina la mtu aliyehifadhiwa katika kaburi lile lilisomeka vizuri. Lydia Michael.
Tarehe ya kuzaliwa; 15/4/1990 Tarehe ya kufariki; 14/2/ 2012
Niliweka jembe langu pembeni, nilipiga magoti mbele ya kaburi lile. Nilifumba macho nikiwa nimeangalia juu, na kuanza kuongea peke yangu.
"Lydia mpenzi, kwanini uliamua kuondoka mapema sana. Kwanini uliamua kuniacha peke yangu Lydia. Bado nazikumbuka ahadi zako Lydia. Uliniahidi tutakuwa mume na mke. Tutaanzisha familia na kuzaa watoto, Lydia.
Lydia ulikuwa mwanamke wa kipekee sana kwangu. Mwanamke uliyenipenda kwa dhati nikiwa sina chochote kile. Lydia mwanamke mwenye upendo usiomithilika.
Nakumbuka ulikubali kuishi na mimi nikiwa sina kitu kabisa. Nilikuwa sina kazi yoyote, ningepata vipi kazi ilhali sikuwa na elimu? Nilikuwa naelekea kuwa mtoto wa mtaani, baada ya wazazi wangu wote wawili kufariki kwa ugonjwa wa hatari wa Ukimwi. Ugonjwa
ulioondoka na roho za wazazi wangu wote wawili, ugonjwa ulioniletea uyatima nikiwa mdogo sana.
Kwa bahati mbaya zaidi ugonjwa huu ulikuja na kitu kibaya sana. Unyanyapaa!
Wakati dunia mzima ikinitenga kwa kudai eti nina maambukizi ya virusi vya Ukimwi, virusi nilivyoambukizwa na wazazi wangu, lakini Lydia hukunitenga mpenzi.
Usiku ambao ndugu zangu walinifukuza katika nyumba iliyojengwa kwa jasho la wazazi wangu, nd'o usiku niliokutana na wewe Lydia, ukiwa unatoka kuuza maandazi yako sokoni Kariakoo. Nilikueleza matatizo yangu huku machozi yakinitiririka mithili ya maji.
Nakumbuka uliniangalia usoni na kunijibu maneno
matatu tu..
"Tutaishi Pamoja Allen" Na ilikuwa hivyo, ulinikaribisha kwako Lydia.
Tuliishi pamoja katika kibanda dhaifu kilichopo pale Jangwani. Nakumbuka tuliishi maisha magumu sana!
Mara nyingi tulilala na njaa, mara nyingine tulinyeshewa na mvua, mara nyingi tulichomwa na jua, mara nyingi tulisumbuliwa na vibaka.
Lakini tulipambana!
Tuliendelea kuishi pamoja mpenzi ingawa kwa shida.
Siku moja asubuhi, nakumbuka nilikuaga asubuhi kuwa naenda kutafuta. Nilikupiga busu mwanana katikati ya paji lako la uso tukiwa tumesimama pale mlangoni, mlango wa gunia chakavu. Nikatamka.
"Ubaki salama mpenzi wangu Lydia"
Nilienda kutafuta Lydia, ndio...nilienda kutafuta, lakini sikupata!.
Saa sita mchana nilikuwa narudi nyumbani nikiwa nimechoka sana, nimechoka kwa uchovu wa kutembea kwa miguu, nimechoka kwa kukosa hata shilingi mia tano. Nikiwa nimeweka mikono yangu nyuma, huku upepo mkali ukipeperusha shati langu dhaifu lililochanika kwa nyuma. Halikuwa shati, ilikuwa bendera.
Karibu na manzese darajani niliokota kitu, kipande cha gazeti. Niliokota kipande kile bila kujua kwanini nakiokota, kipande kile cha gazeti kilichorejesha furaha yangu. Katika kipande kile cha gazeti la Dumizi kulikuwa na jina langu, ilikuwa ni orodha ya watu walioitwa kazini kufanya kazi ya kuchora vibonzo katika gazeti hilo maarufu nchini Tanzania. Niliwehuka..
Nilikimbia mbio kuelekea nyumbani kwetu, kwa wewe mpenzi wangu Lydia. Nilikuwa na furaha isiyo na kifani, nilikimbia njiani huku watu wote wakiamini nilikuwa chizi. Sikujali mshangao wao, sikujali macho yao, sikujali zomea na makelele yao, nilichojali ni kwenda kushea furaha yangu na wewe mpenzi wangu Lydia.
Nilifika nyumbani, nilikukuta umesimama mlangoni Lydia. Nilikurukia kwa furaha, tukadondoka mpaka chini. Tulichafuka vumbi tupu.
Nakumbuka uliniuliza kwa upole kilichonifurahisha kiasi kile, nilikujibu nimepata kazi mpenzi katika gazeti la Dumizi. Hukuamini!
Sijui ni kwanini hukuamini Lydia, ni wewe ndiye uliyenambia nina kipaji kikubwa sana cha kuchora. Ni wewe ndiye uliyenishauri nishiriki katika mashindano yale yaliyoandaliwa na gazeti la Dumizi, na kila siku ulikuwa unaniambia ni mimi ndiye nitakayeibuka mshindi. Sasa Kwanini hukuamini Lydia nilivyokwambia kuwa nimepata kazi katika gazeti la Dumizi.
Nakumbuka usiku wa manane uliamka Lydia. Ulinipapasa mgongoni taratibu, kwa sauti ya upendo ulinambia.
"Allen mpenzi, umepata kazi. Siyo kwamba siamini kama umepata kazi, naamini sana, una kipaji kikubwa sana cha kuchora vibonzo, na siku zote niliamini wewe
ndiye utakayeibuka mshindi. Hakuna anayekufikia kwa kuchora katika nchi hii. Hakuna kabisa!
Lakini mpenzi wangu nina hofu, hofu ya kuachwa. Unaniahidi hutonitesa baada ya kupata kazi?.
Unaniahidi hutonisaliti?, unaniahidi Allen?.
Nilikuwa nimechoka sana, hivyo nilikujibu kwa kifupi, nikiwa nimekereka kwa kukatishwa usingizi..
"Siwezi kukusaliti Lydia!" Niligeuka upande wa pili na kulala.
Na ilikuwa kweli, niliajiriwa katika gazeti la Dumizi, kama mchora vibonzo. Tukahama kwenye kila kibanda dhaifu pale Jangwani, na kuhamia kwenye nyumba ya kisasa, Sinza kwa Remy.
Tuliendelea kuishi pamoja na wewe Lydia mpenzi wangu. Lakini sasa sikuwa nakuangalia kwa jicho la mke tena, nilikuwa nakuangalia kwa jicho kama mfanyakazi wangu wa ndani.
Wiki moja tu ilitosha kunambia kwamba Lydia haukuwa wa hadhi yangu. Ulikuwa mshamba sana, ulikuwa huna mvuto wa kuishi na mtu maarufu kama mimi. Pesa inabadilisha tabia ya mtu, pesa ni kitu kibaya sana hasa ukikipata katika umri mdogo tena bila kutarajia. Pesa ilinibadilisha.
Kubadilishwa na fedha siyo tatizo, tatizo ilinitoa mwangani na kunisukumia gizani. Ilinitoa kuwa mwanaume mpole, mstaarabu na mwenye busara, na kunipeleka kuwa mwanaume mkorofi, kiburi na mlevi. Nilianzisha tabia mpya, tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani. Tabia iliyochochewa na pombe, tabia iliyochochewa na mabaamedi. Tabia mbaya kabisa ambayo sikuwa nayo kabla. Lakini yote hayo ulivumilia Lydia.
Ikapita miezi, ikaja saa baada ya kupita siku kadhaa, saa mbaya zaidi katika maisha yako. Saa ambayo nilithubutu kuingiza mwanamke katika nyumba yetu, niliingiza mwanamke wakati wewe ulikuwepo.
Tulikukuta upo sebuleni unasali, tulikusonya kwa
pamoja, hatukujali ulichokuwa unachokifanya. Tulikaa pale sofani, tulianza kushikanashikana wakati wewe unasali.
Ulimaliza kusali, kwa hekima kubwa uliondoka bila kusema chochote, bila kufanya chochote, sikuwa najua kabisa kiasi gani ulikuwa unaumia, nilikuwa naona sawa tu kwa kila nilichokuwa nakifanya.
Siku ile tulilala sebuleni na yule changudoa niliyomchukua Kona baa, bila wasiwasi wowote. Lakini mimi sikukoma!
Siku ya pili nilikuja tena na mwanamke mwengine. Nakumbuka nilikukuta umelala chumbani. Nilikufukuza kama mbwa huku nikikutukana matusi makubwa sana. Nilikutukana matusi bila sababu maalumu. Lakini hukubisha Lydia. Ulinyanyuka taratibu pale kitandani na kwenda sebuleni. Ulilala sebuleni siku ile ilhali mimi nikilala chumbani, tena na changudoa!
Ulikuwa mwanamke wa ajabu sana Lydia, pamoja na yote hayo haukuonesha dharau kabisa kwangu, ulinijali, na mbaya zaidi ulizidi kunipenda!
Ni mwanamke gani duniani mwenye moyo kama wako, mwanamke anayeweza kuvumilia visivyoweza kuvumilika kama nikivyokufanyia wewe. Ni mwanamke gani?
Nakumbuka siku moja, siku iliyoanza kwa manyunyu ya mvua, sikumbuki ilikuwa juma ngapi, aahhhh leo nimekumbuka, ilikuwa jumamosi, ndiyo...kulikuwa na disco katika ukumbi wa Ambiance pale Sinza Africa sana.
Mimi nilienda, wewe nilikuacha umelala.
Nilirudi saa kumi usiku, kama kawaida yangu nilirudi na mwanamke, naye alikuwa changudoa. Changudoa mbaya zaidi katika maisha yangu! Tuligonga sana mlango pale nje, ilitunyeshea sana mvua pale nje.
Hukuja kufungua mapema. Labda ulilala sana kwa ajili
ya mvua, au labda ulikuwa umechoka kwa kazi nzito ulizofanya mchana, au yote hayo kwa pamoja.
Lakini baadae ulitufungulia, baada ya kuita sana. Ulitutizama mimi na yule mwanamke, changudoa niliyemuokota tu njiani. Sijui nimlaumu nani, eti nilijifanya nampenda sana mwanamke yule kuliko wewe. Labda nilikuwa nimerogwa! Yule mwanamke naye alifanya jambo la ajabu sana pale mlangoni.
Alikupiga kofi la nguvu sana usoni, eti akidai
umechelewa kutufungulia mlango. Nilitegemea labda utafanya kitu kikubwa sana. Lakini haikuwa hivyo kwako Lydia. Ulitoa maneno yaliyonishangaza sana.
"Naomba mnisamehe, sikusikia mlivyokuwa mnaniamsha"
Tuliingia ndani tukikokotana na yule mwanamke, mwanamke nisiyemjua, mwanamke asiyenijua.
Mwanamke aliyeingiwa na tamaa za mali zangu ghafla tu baada ya kuingia ndani, na kutamani kunimiliki kabisa, ili azimiliki mali zangu.
Baada ya nusu saa tu za kukaa chumbani aliniaga anaenda chooni, kumbe hakuwa anaenda chooni. Alikufata wewe pale sebuleni changudoa yule mwenye roho mbaya sana. Alikukuta umelala Lydia. Changudoa yule wa ajabu alikuziba mdomo na pua kwa mkono yake mipana. Ulikuwa dhaifu sana Lydia. Ulijitahidi kujitoa bila mafanikio.
Nikiwa kule chumbani nilisikia miguno yako, lakini sikujali kabisa, Lydia mpenzi ulifariki kifo kibaya sana wakati nilikuwa na uwezo mkubwa sana kukusaidia. Ulifariki siku kama ya leo, siku ya Valentine. Kwangu siku ya Valentine ni siku mbaya zaidi duniani.
Maana siku ile nilikuwa na uwezo wa kufanya kitu ili usiwawe, lakini sikufanya kitu chochote. Cha ajabu nilimpongeza yule mwanamke, nikimuona shujaa kwa kukuuwa wewe, mwanamke nikiyekuchukia sana tangu siku nilipoajiriwa na gazeti la Dumizi.
Baada ya ile ajira tu nilikuwa nasema hivi, katika vitu viwili nikivyovichukia zaidi duniani, ni wewe na shetani. Tuliificha ndani maiti yako usiku ule na mchana kutwa.
Usiku wa manane uliofuata tulienda kukufukia na yule baradhuli. Hatukukuzika Lydia, tulikufukia kama mnyama!
Lydia mpenzi, unafikiri mapenzi yetu yalidumu na yule mwanamke, wewe hukuwepo lakini malaika wako alikuwepo, hatukufikisha hata wiki na yule mwanamke.
Siku ya nne tu nikiwa na yule mwanamke, Nilikuja kugundua siri kubwa sana toka kwa yule mwanamke. Kumbe alikuwa anatumia dawa ya kurefusha maisha( ARVs), nilizozifuma katika mkoba wake. Ishara kwamba ameathirika na virusi hatari vya ugonjwa wa Ukimwi.
Sikumwambia.
Nami nikaenda kupima pale Angaza. Majibu yalipotoka, yalikuwa machungu mithili ya shubiri, na mimi nilikuwa nimeambukizwa virusi hatari vya ugonjwa wa Ukimwi. Ugonjwa uleule uliowauwa wazazi wangu wote wawili.
Nakubali nilistahili kupata adhabu hii, au pengine adhabu kubwa zaidi ya hii, kutokana na vitendo vibaya sana nilivyokufanyia mpenzi wangu Lydia. Leo nimekuja hapa kukwambia maneno haya.
"Nimegundua wewe ndiye mwanamke uliyenipenda, uliyenijali na kuniheshimu zaidi duniani. Natamani siku zirudi nyuma ili nikwambie haya, lakini siwezi, haiwezekani kurudisha siku nyuma. Naomba msamaha kwa yote niliyokufanyia Lydia, pesa na umaarufu vilinisukuma kwenye tamaa, tamaa mbaya! Pesa na umaarufu vimeniletea gonjwa hili lisilo na tiba.
Ningetulia na wewe nisingelia leo hii. Najiahidi sitokuwa na mwanamke mwengine tena hapa duniani mpaka nitakapokufuata Lydia ulipo, ili nije huko uliko tuishi wote Lydia. Nakuahidi nitaishi peke yangu katika maisha yangu yote yaliyobakia, ili nisiwaambukize watu wasio na hatia ugonjwa huu hatari, ili nilitunze penzi lako Lydia. NAKUPENDA SANA LYDIA.'
Nililimia kaburi la Lydia Michael, kisha nilirudi nyumbani.
Mwisho.
Halfani Sudy. 14/2/2015
Comments
Post a Comment