Fahamu sababu zinazopelekea mashirika ya ndege barani Afrika kupata hasara


ndege

Hivi karibuni kumeibuka kwa maneno mengi kutoka kwa wananchi wa nchi za Afrika zinazomiliki ndege za kibiashara kutokana na hasara zinazopatikana kakutokana na sekta ya mashirika ya ndege yaliyopo kwenye mataifa yao.

Mpaka hivi sasa wasomi na wananchi wameenda mbali nakuhoji kama nchi zao mfano Kenya, Tanzania, Afrika kusini na Ethiopia kulikuwa na ulazima kuwekeza fedha nyingi za walipa kodi katika kununua ndege nyingi kwaajili ya kufanya biashara wakati bado mashirika hayo yalikuwa hayajajipanga vyakutosha katika kusimamia na kuendesha biashara za aina hii kulingana na ushindani uliopo hivi sasa.

Pamoja na kuwa upatikanaji wa huduma za usafiri wa anga ni muhimu katika ukuaji wa uchumi kwani husaidia katika ukuaji wa sekta za utalii, ajira na kuvutia wawekezaji wa nje kuwekeza.

Lakini tujiulize Je, kwa hali ya kiuchumi katika nchi zetu hasa kwa kuangalia vipato vya mwananchi mmoja mmoja kulikuwa na ulazima wa serikali za nchi hizi za Afrika kuzamisha fedha nyingi kiasi hiki kwenye kufufua mashirika haya ya ndege?

Au serikali zingepaswa kualika makampuni ya kibiashara kuweza kuja na kuwekeza katika sekta hii na kuokoa mabilioni haya ya fedha za kodi za wananchi ambao bado hali zao za kiuchumi bado si zakuridhisha?

Mashirika ya ndege mfano Air Tanzania, namna ambavyo lilifufuliwa lilileta maswali mengi kwa wasomi hasa wanauchumi pamoja na wananchi kwa kuwa mchakato wake haukuwa wa wazi kiasi kilichopelekea wabunge wengi wanasiasa kama Tundu Lissu, Zitto Zuberi Kabwe na wengine kulalamikia serikali kwa kuihoji maswali mengi ili kuweza kujua ni mchakato gani ulitumiwa katika kufufua shirika hili la ndege ili kuweza kupata uhalali wake kisheria hasa kwa kuzingatia sheria za manunuzi zilizopitishwa na bunge lakini walibezwa na hawakupata kujibiwa maswali yao.

Wanasiasa hawa walikuwa wakitaka kujua fedha hizi zilitolewa wapi?

Kwanini fedha hizi ambazo hazikupitishwa na bunge la Tanzania na wala hakuna mchakato wowote uliopata kuletwa kwenye bunge wala kutolewa na serikali kwa wananchi ilikuweza kutambua na kufahamu namna ndege hizo ziliweza kununuliwa?

Maswali haya na mengineyo mengi hayajapata kujibiwa mpaka hivi leo zaidi ya kupokea taarifa za shirika kujiendesha kwa hasara.

Mashirika mengi ya ndege hivi sasa Afrika yanaendeshwa kwa hasara kubwa sana jambo ambalo linapelekea fedha nyingi ambazo zingetumika katika shughuli nyingi za kimaendeleo kuchukuliwa na kuingizwa katika kuokoa mashirika haya ambayo hayafanyi vizuri tokea kuanzishwa kwake, na hivyo kupelekea shughuli nyingi za kimaendeleo kusuasua na kufanya hali za wananchi kuwa ngumu na wakati mwingine kupelekea mzunguko wa fedha kuwa mdogo katika mataifa haya yanayomiliki ndege za kibiashara Afrika.

Mfano; Kwa mwaka 2019/2020 peke yake mkaguzi wa hesabu za serikali Tanzania Charles Edward Kichere (CAG) anasema shirika la ndege la Tanzania limepata hasara ya zaidi ya bilioni 60 kwa maana hiyo mpaka hivi sasa shirika la ndege la Tanzania bado linaendeshwa kwa hasara tena hasara kubwa ambayo haijawekwa wazi vya kutosheleza.

Kwa mwaka 2015/2016 shirika lilipata hasara ya bilioni 94.3, mwaka 2016/2017 shirika la ndege Tanzania lilipata hasara ya bilioni 109.3 na mwaka 2017/2018 shirika lilipata hasara ya zaidi ya bilioni 113.8.

Kwa mtiririko huo ni wazi kuwa shirika la ndege la Tanzania linajiendesha kwa hasara kubwa ambapo wataalam wa masuala ya anga na uchumi wanadai bado kuna uwezekano kukawa na hasara kubwa zaidi lakini ukweli haujawekwa bayana kutokana na sababu nyingi hasa za kisiasa.

Kenya

Shirika la ndege la Kenya (Kenya Airways) lilitangaza hasara ya dola milioni 83 kwa mwaka 2020. Na kulingana na Mwenyekiti wa shirika hilo la ndege alieleza bayana ya kuwa hakuna ukuaji wa sekta hiyo kwa hivi sasa labda mpaka ifikapo mwaka 2024/2025.

Shirika la ndege Kenya linakabiliwa na madeni mengi makubwa.

Madeni haya ya Shirika la ndege la Kenya ni kielelezo tosha kuwa Shirika hili linaendeshwa kwa hasara kubwa.

Hapo awali wamepata kubadilisha watendaji wakuu watatu kwa kudhania yakuwa utendaji wao ni mbovu lakini bado hali katika shirika hilo siyo shwari na hivyo bado linaendeshwa kwa hasara.

Hivi sasa Serikali ya Kenya inapanga kurejesha pesa za wamiliki wa hisa nyingi ikiwemo shirika la Air France - KLM inayomiliki asilimia 7.8 ya hisa.

Shirika la ndege la Ethiopia (Ethiopia Airways) nalo linaendeshwa kwa hasara kubwa sana. Kwa mwaka 2020 pekee yake shirika hili limeripoti hasara ya zaidi ya dola milioni 500.

Na mpaka hivi sasa shirika la ndege la Ethiopia inakabiliwa na changamoto yakulipa madeni linayodaiwa shirika hilo kutokana na kuzuia baadhi ya safari zake sababu ya changamoto za ugonjwa wa COVID 19.

ethiopia

Shirika la ndege la Afrika Kusini (South Afrika Airways) nalo linajiendesha kwa hasara kubwa kwani kwa mwaka 2020 limepata hasara ya zaidi ya R.33 bilioni.

Na kama unavyojua kutokana na hasara shirika hili inalozipata watu mbalimbali wamekuwa wakishinikiza serikali kulibinafsisha shirika hilo kwani kwa sasa shirika hilo ni hasara na mzigo kwa watu wa Afrika Kusini.

Tatizo kubwa la mashirika hayo ya ndege za Afrika kutokufanya vizuri zipo nyingi japo hivi sasa mashirika haya yanajificha katika kivuli cha Corona (COVID -19) lakini ukweli utaendeelea kubakia kuwa hata kabla ya COVID -19 bado mashirika hayo yalikuwa yakijiendesha kwa hasara kubwa tofauti na ilivyodhaniwa katika kuanzishwa kwake.

Yapo mashirika yanayofanya vizuri kibiashara pamoja na janga la COVID-19.

d

Mfano Mashirika ya ndege ambayo pamoja na corona yameendelea kufanya vizuri kutokana na kujidhatiti kibiashara ni pamoja na;

Shirika la Emirates ambalo pamoja na corona janga la corona kwa mwaka 2020 lilitengeneza faida ya dola milioni 456 ($ 456) . Shirika la ndege la Singapore Airlines likitengeneza faida ya 59.1 bilioni Singapore dola.

Shirika la ndege Etihad Airline likitengeneza faida ya dola bilioni 1.7 ($ 1.7) wakati mwaka 2019 likitengeneza faida ya dola 2.7.

Kuweza kuokoa mashirika ya ndege ya nchi za Afrika hatua za kimakusudi za kibiashara lazima zichukuliwe tofauti na hatua zinazochukuliwa hivi sasa ambazo ni za kisiasa tu na siyo za kitaalamu ambazo zinazingatia ufanye wa biashara za ndege.

Vinginevyo mashirika haya yataendelea kuwa hasara na mzigo kwa Serikali na wananchi na hivyo kupelekea kurudi nyuma zaidi kimaendeleo kwani fedha nyingi badala ya kupelekwa kwenye maendeleo ya wananchi zitakuwa zikipelekwa kwenye kuokoa mashirika haya kutokana na hasara mashirika haya yanazozipata.

Serikali ya nchi za Afrika ili kuweza kufanikiwa katika aina hii ya biashara lazima wakubali kujifunza zaidi kutoka kwenye mashirika yanayofanya vizuri kwenye uwanda huu ilikujipatia uzoefu na mbinu za namna za kuendesha mashirika haya kwa faida zaidi. Mfano wa mashirika hayo ni pamoja na Air Canada, Delta Airlines, American Airlines na Singapore Airlines

Comments