Kifo cha Magufuli: Watu watano wa familia moja wafariki wakimuaga Rais Magufuli

 

Kifo cha Magufuli: Watu watano wa familia moja wafariki wakimuaga Rais Magufuli

uwanja

Familia moja jijini Dar Es Salaam imepoteza watu watano katika mkanyagano uliotokea wakati maelfu ya wakaazi wa jiji hilo walipojitokeza kuuaga mwili wa Rais John Magufuli.

Dennis Mtuwa amepoteza mke wake, watoto wawili, na wapwa zake wawili. Walienda kumuaga aliyekuwa Rais wao jana Jumapili katika Uwanja wa Uhuru, lakini hawakurejea tena nyumbani.

Msichana wa kazi anayewasaidia kwa shughuli za nyumbani mpaka sasa hajulikani alipo.

Bwana Mtuwa alipokea simu kutoka kwa msamaria mwema mmoja ambaye aliokota pochi ya mke wake na kumtaarifu kuwa inafaa aende uwanjani ama polisi kumtafuta.

Alifanya hivyo kwa haraka na maumivu yake yakawa makubwa zaidi baada ya kuona miili ya wapendwa wake.

"Saa 24 zilizopita zimekuwa ngumu sana kwangu, napata faraja nikiwa nipo na watu, ila nikiwa peke yangu nakumbwa na huzuni ambayo haiwezi kuelezeka...watu watano wa familia yangu wameondoka, ni msiba wa ukoo, nimebaki na mtoto mmoja tu wa miaka miwili," anaeleza Bwana Mtuwa.

Na huku wanafamilia na marafiki wa karibu wakikaa na kusubiri miili ya ndugu zao ili waweze kuzika, wanapata tabu kuamini mtihani huu uliowakumba.

"Huu mtihani ni mgumu sana kwetu, ni kwa neema ya Mungu tu ndio tumeweza kufika hata hapa tulipo sasa," ameeleza Irene Mtuwa, ndugu wa familia.

Mamlaka nchini Tanzania bado hazijatoa idadi kamili ya watu waliokufa au waliojeruhiwa ila ripoti ambazo hazikuthibitishwa zinasema takriban watu 40 huenda wakawa wamefariki dunia.

Kamanda wa Polisi wa jiji la Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ameiambia BBC kuwa atalizungumzia suala hilo kesho Jumanne.

Tukio hilo limetokea wakati ambapo maelfu ya wakaazi wa jiji la Dar Es Salaam wakijitokeza katika mitaa na Uwanja wa Uhuru kuonesha hisia na majonzi yao kwa kiongozi wao aliyewaongoza kwa kipindi cha miaka 6.

Idadi hiyo kubwa ya waombolezaji iliumuaga rais huyo lakini idadi kubwa zaidi ilishindwa na hatimaye mamlaka kuamua kuuzungusha mwili huo mara tano kabla ya kuuondoa uwanjani kuelekea uwanja wa ndege ili kusafirishwa kwenda Dodoma.

Hata hivyo, idadi hiyo kubwa ya watu iliingia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kuuaga mwili huo ukiwa unapandishwa kwenye ndege.

Comments