Skip to main content

Kikundi cha watu kimezua taharuki katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam na kusababisha maduka mengi kufungwa huku wafanyabiashara wakitimua mbio.


kariakopic

Dar es Salaam. Kikundi cha watu kimezua taharuki katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam na kusababisha maduka mengi kufungwa huku wafanyabiashara wakitimua mbio.

Kikundi hicho ambacho bado dhamira yake haijafahamika kilikuwa kikipita kama watu wanaokimbizwa na kupaza sauti kikiwataka wafanyabiashara kufunga maduka wakidai kuna watu watawavamia na kuwapiga kwa kuwa wamefungua biashara zao leo Jumatatu Machi 22, 2021.

Tukio hilo limetokea leo saa 5 asubuhi na kudumu kwa takribani saa moja na nusu ambapo Mwananchi Digital ilifika eneo hilo na kushuhudia maduka mengi yakiwa yamefungwa huku watu wakikimbia ovyo.

“Mimi nilibaki nashangaa sikujua la kufanya nilikimbia kwa kuwa watu walikuwa wakikimbia kutoka mtaa mmoja kwenda mwingine. Baadaye nilijiuliza nakimbia biashara yangu namuachia nani, nilitulia nikarudi na kukaa,” amesema.

Kutokana na hali hiyo mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge alitembelea  soko hilo ili kuwatuliza wananchi huku akiwaambia hakuna agizo lililotolewa na Serikali

“Kama kuna mtu amefanya hivyo ni muhuni na tapeli, sisi tunaendelea kuchukua hatua kwa waliohusika, nawatamkia endeleeni na biashara zenu bila wasiwasi, wenye maduka fungueni biashara zenu na wenye biashara ndogondogo endeleeni na biashara zenu,” amesema Kunenge

Comments