KILICHONITOKEA BAADA YA KUBAKWA NA KAKA YANGU - 4
Simulizi : Kilichonitokea Baada Ya Kubakwa Na Kaka Yangu
Sehemu Ya Nne (4)
Nikiwa nahaha kujinasua alinibana kwa nguvu na bila kutegemea akanibaka jambo lililonipa maumivu makali sana ambayo nashindwa kuyaelezea, alipomaliza haja zake aliniachia na kunipa onyo kwamba ole wangu nimwambie mtu kuhusu alichonifanyia angeniua.
Wakati nalia, alitoa shuka lililokuwa limelowa damu, akatandika lingine lakini alisisitiza kwamba nikithubutu kumwambia mama au mtu yeyote, ninsingekuwa na maisha.
Hata hivyo, licha ya kaka Evance kunifanyia kitendo hicho cha kinyama ghafla alibadilika na kuwa mpole, akaanza kuniomba msamaha kwamba ni shetani alimpitia akajikuta akinifanyia vile.
Aliniomba msamaha na kunisihi nisimwambie mtu kwani mama yake akisikia itakuwa balaa na atagoma kumlipia ada ya chuoni, kisha akarudia kwamba pamoja na kuniomba msamaha siku nitakayotoa siri hiyo ataniua na kutoroka pale nyumbani.
Kutokana na kitisho hicho, nilitoka mle chumbani nikiwa nina maumivu makali nikaenda chumbani kwangu nikaanza kulia lakini baadaye nihisi kama mama angenikuta ninalia kwa vyovyote vile angeniuliza sababu ambapo nisingemficha kitu na matokeo yake Evance angeniua kama alivyoahidi.
Niliamua kunyamaza na kujipa huduma ya kwanza, hata hivyo sikuweza kufanya jambo lolote kwa maumivu niliyokuwanayo hadi mama aliporejea na aliponiuliza sababu za kuwa mnyonge nilimwambia kichwa kilikuwa kinauma.
Mama alinipa panadol, nilipomeza nikalala, usiku alipokuja kunijua hali nilimwambia nilijisikia nafuu na chakula kilipokuwa tayari nilikwenda mezani kwa kujikongoja kufuatia maumivu niliyopata.
Kwa kuwa sikujisikia vizuri, nilipomaliza kula nilikwenda chumbani kwangu na kuanza kutafakari kitendo cha kikatili ambacho Evance alinifanyia.
Nilijikuta najisemea moyoni kwamba kama mama angekuwa hai au baba angelikuwepo wala nisingefanyiwa ukatili ule, nikaanza kutitirikwa machozi.
Hata hivyo, kuhofia mama angeingia na kunikuta nalia nilinyamaza ambapo sikukaa muda mrefu nilipitiwa na usingizi hadi nilipozinduka kwenye saa saba.
Baada ya kuzinduka, nikaanza tena kufikiria mambo mengi niliyopitia tangu nikiwa mdogo mpaka tukio la kubakwa alilonifanyia kaka Evance niliyemuamini na kumchukulia kama kaka yangu wa damu.
Kutokana na mawazo hayo, sikuweza kupata usingizi kwa muda mrefu, nakumbuka nililala kwenye saa tisa kasoro nikashtuka kufuatia mama aliyeingia chumbani kwangu kuniita ili kujua hali yangu.
Ingawa nilihisi maumivu, nilimweleza niliendelea vizuri kisha alitoka na kwenda chumbani kwake nami nikabaki najigeuzageuza kitandani hadi saa kumi na mbili na nusu alfajiri.
Kwa kuwa bado nilihisi maumivu ya jeraha nililopata baada ya kubakwa, nilikwenda jikoni nilikochemsha maji ambayo nilijikanda kwa lengo kupunguza maumivu.
Ingawa muda huo kaka Evance alikuwa hakosekani nyumbani, nilipoamka sikumuona na sikufahamu alikwenda wapi hadi ilipofisa saa tano ndipo alirejea.
Aporejea alinikuta nimeketi sebuleni peke yangu, nilipomuona nilipatwa na hasira na kutamani kumvamia ili nimng’ate meno na kunyofoa ngozi au kiungo chochote cha mwilini mwake ili kila akiliona jeraha aukumbuke unyama alionifanyia.
Hata hivyo, nilijizuia kwa kuhofia angenifanyia kitendo kibaya kama alivyoniambia nikajikuta natiririkwa machozi na kwenda chumbani kwangu.
Kufuatia hasira nilizokuwanazo, Evance aligundua sikuwa sawa ingawa hakuwa akiingia mara kwa mara chumbani kwangu aliingia na kuniomba msamaha kwa kitendo alichonifanyia.
Aliniambia kwamba tangu aliponibaka alikosa amani ndiyo maana asuhubi aliondoka pale nyumbani kwani moyo ulimsuta sana, hivyo nimsamehe.
Nikiwa nina hasira nilimwambia kwa tukio alilofanya hakupitiwa na shetani isipokuwa alidhamiria kwa muda mrefu, akanipinga kwamba hakudhamiria.
Hata hivyo, kwa hasira nilimwambia sitamsamehe na kumweleza nitamfahamisha mama juu ya kitendo hicho.
Nilipomweleza hivyo, alinipiga mkwara kwamba siku nitakayothubutu kutoa siri hiyo ndiyo ungekuwa mwisho wangu na yeye angetoroka pale nyumbani.
Nikiwa binadamu niliyependa kuendelea kuishi, kauli yake ilininyong’nyesha nikaamua kukaa kimya na maumivu yangu kwani nilijua hata kama ningemwambia mama asingekubali kuwa upande wangu na kumuacha mwanaye.
Baada ya Evance kunitishia hivyo, alitoka mle chumbani hata nilipotoka nje sikumuona hadi aliporejea jioni ambapo hatukuchangamkiana kama ilivyokuwa kawaida yetu.
Wakati huo wa jioni kidogo nilipata nafuu, ambapo nilijumuika na wanafamilia kufanya kazi ndogo ndogo hadi usiku ambapo tulikula na kwenda kulala.
Siku iliyofuata, maumivu hayakuwa makali sana tukaendelea na maisha kama kawaida lakini siku kama kumi hivi mama akiwa kasafiri nilianza kuhisi kuchoka na kupenda kulala muda mwingi.
Hali hiyo ilikwenda sambamba na kukerwa na harufu ya baadhi ya vyakula hasa samaki, maharage na nilipenda sana kunywa soda aina ya Pepsi tabia ambayo sikuwa nayo.
Kadiri siku zilivyokwenda nikawa najisikia ovyoovyo sana na hata tarehe ambazo nilikuwa napata hedhi zilipofika sikupa siku zangu, kwa kuwa sikuwa na ufahamu wa masuala ya uzazi sikuelewa kama nilikuwa nina mimba.
Wakati huo pale nyumbani hakuwepo mtu mkubwa zaidi ya kaka Evance, Emmy, mimi na msichana mwingine mtoto wa mjomba wao hivyo hakuna aliyejua kama nilikuwa nina ujauzito.
Kufuatia kutapika na kuchagua chakula nilijua nilikuwa nasumbuliwa na malaria nikawa nakunywa panadol badala ya kwenda hospitali kwa sababu nilikuwa naogopa sana kuchomwa sindano na kumeza vidonge.
Ingawa mama aliposafiri alikuwa hakai muda mrefu, safari hiyo alikaa mwezi mmoja kama na wiki mbili kwani alikwenda Mwanza hadi Bukoba.
Siku aliyorejea aliponiona alinitazama na kuniuliza mbona nilikuwa nimependeza sana, nikaishia kucheka kwani sikujua alimaanisha nini, kwa kuwa alikuja na samaki wabichi aina ya sato aliniambia niwaandae kwa ajili ya kitoweo.
Kitendo cha kukumbana na harufu ya samaki, nilichafua nyongo nilitapika sana mpaka mama akashangaa ambapo aliniuliza nilikuwa naumwa nini nikamwambia sikuelewa ila sikupenda tu harufu ya samaki.
Kumbe wakati huo mama alishahisi nilikuwa nina ujauzito lakini hakutaka kuniendea haraka, aliendelea kunichangamkia huku akihesabu pepsi nilizokunywa tangu alipofika ambazo zilifika nne tena za baridi sana.
Kutokana kutopenda harufu ya samaki, chakula kilipokuwa tayari sikula badala yake nilitengeneza kachumbali ambayo niliweka ndimu nyingi nikala na ugali.
Kwa ujumla kila nilipolamba ndimu nilijisikia raha sana na mara kwa mara nikiwa chumbani kwangu nilikuwa nafanya hivyo na nikimaliza mabaki ya ndimu niliyatupia chini ya kitanda.
Nakumbuka ilipofika saa tisa alasiri nikiwa nimelala, mama mkubwa aliingia chumbani kwangu akaniamsha na kuniuliza nilikuwa nasumbuliwa na kitu gani, kumbe alinitega.
Kwa kuwa nilikuwa sifahamu kitu chochote nilimwambia kuna wakati sikujisikia vizuri tu na kupenda kulala, akaniangalia kwa kunikazia macho nikayakwepesha yangu.
“Dorcas!” Mama aliniita.
Nilipoitika akaniuliza kama nilianza kufanya mapenzi nikakaa kimya, akaniuliza mbona nilikaa kimya nikamwambia hata hayo mapenzi sikuyafahamu.
Baada ya kumwambia hivyo, akakunja sura na kuniambia nisijifanye mjanja kwani alikuwa anaelewa nilianza kufanya mapenzi na tayari nilikuwa mjamzito.
Aliponimbia hivyo, nilimuuliza kwa kuhamaki; “Mimi nina mimba?”
Kufuatia kumuuliza hivyo, mama aliyeona namletea mzaha alinizaba kibao ambacho kilinifanya niangukie kitandani nikaanza kulia.
“Yaani unajua kabisa una mimba nakuuliza unajifanya hujui, sasa leo utanitambua na utanieleza huyo mbwa aliyekupatia hiyo mimba ili nikakukabidhi kwake aulee mzigo wake,” mama aliyekuwa na hasira aliniambia.
Nikiwa nalia aliniinua na kuniuliza tena kama nilikuwa nina mimba nikamwambia mama sikufahamu chochote ndipo alinihakikisha kwamba nilikuwa katika hali hiyo kwani nilikuwa nina dalili zote.
Mama aliniuliza ulikuwa ujauzito wa nani na lini nilianza mapenzi, licha ya kaka Evance kuniambia kama ningetoa siri hiyo angeniua niliamua lolote litakalotokea katika maisha yangu litakuwa sawa kwani sikuwa na furaha ya kuendelea kuishi kwa sababu sikuwa na wazazi wala ndugu yeyote wa damu.
“Wewe kinyago si nimekuuliza nani amekupa huo ujauzito?” mama aliniuliza kwa hasira.
Huku nikiwa nalia na hasira zikiwa zimenipanda, nilimwambia mama kama kweli nilikuwa na mimba mhusika ni kaka Evance.
“Unasema mhusika ni nani nani?” mama aliniuliza kwa kuhamaki.
Sikuona sababu ya kumficha, nilimsimulia kila kitu alichonifanyia, ghafla mama alinywea nikamuona machozi yanamlengalenga machoni.
Akiwa katika hali hiyo aliniomba msamaha kwa kunipiga na kunitolea lugha kali, akanipa pole na kuniambia nilale akatoka mle chumbani na kuanza kumuita Evance.
Kumbe wakati mama ananihoji, kijana wake huyo alikuwa amesimama nje ya dirisha la chumba tulichokuwemo akisikiliza kila kitu na alipojua ambacho kingefuatia, alitoweka pale nyumbani.
Wakati mama akiendelea kumwita alitokea Emmy aliyemweleza alimuona kaka yake akielekea mitaa ya sokoni, akamuuliza alikuwa na nani akamfahamisha kwamba alikuwa peke yake.
Mama hakuwa na la kufanya akarudi tena chumbani kwangu akiwa amepoa ambapo alinikuta nimejilaza, akaniuliza kama nilihitaji kula au kunywa chochote nikamwambia soda niliyokuwa napenda kunywa, akatabasamu na kutoka mle chumbani.
Hakuchukua hata dakika moja alirejea akiwa na soda hiyo pamoja na glasi akaifungua na kuniambia nikae nianze kunywa, nikafanya hivyo naye akiwa pembeni.
Yaani upendo ambao mama alinionesha ulikuwa wa hali ya juu, wakati napata kiburudisho hicho alinifahamisha kwamba kitendo alichonifanyia Evance kilikuwa cha hatari kwa sababu nilikuwa mwanafunzi.
Aliniomba nisimwambie mtu yeyote wakiwemo rafiki zangu na kwamba wakati akifikiria afanye nini aliniomba niwe nakaa ndani ambapo kila kitu ningehudumiwa bila kutoka nje.
Kwa kuwa nilikuwa mtoto nilikubaliana na kauli ya mama, kabla ya kutoka mle chumbani aliniambia nikipenda kula au kunywa chochote nimwambie kwani alikuwa anajua mwanamke anapokuwa mjamzito anapenda kuchagua vitu, nikamwambia sawa.
Jambo la kushangaza hadi ilipofika saa moja usiku kaka Evance ambaye hakuwa na kawaida ya kuchelewa kurudi nyumbani, hakutokea mama akaanza kuingiwa na wasiwasi.
Hata hivyo, nilimtoa hofu kwamba tuendelee kumsubiri angerudi lakini hadi ilipofika saa tatu hakutokea ndipo mama akaanza kuhaha kumtafuta.
Kwa kuwa alihisi huenda alikuwa kwa rafiki yake kipenzi aliyeitwa Kazimiri, alikwenda kwako ambapo alimkuta akiwa kalala, wazazi wa Kazimiri ambao aliwadanganya kwamba walipishana kauli na mama walipomuuliza sababu aliwaambia ni kweli lakini yaliisha.
Baada ya kuamshwa, kaka na mama waliongozana hadi nyumbani, sikusikia mama akimfokea kijana wake kwani nahisi alifikiri kama angefanya hivyo angeweza kutoroka au siri ingetoka nje.
Kuhofia watu kugundua nilikuwa nina mimba, mama alifanya jambo hilo kuwa siri kwani Emmy hakujua zaidi ya kuelewa nilikuwa naumwa, nafikiri kwa mtu mkubwa aliyekuwa akifahamu alikuwa mama mdogo aliyekuja pale nyumbani akitokea kijijini.
Tuliendelea kuishi huku nikiwa onyoonyo kiafya kwa sababu mara kwa mara nilipokula nilitapika na kupenda kulala sana na maziwa yangu kuongezeka ukubwa na kuniuma.
Niliendelea kuwa katika hali hiyo huku nikiwa namchukia sana Evance ambaye kila tulipokutanisha macho alikwepesha yake, hata ilipofika Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya nilikuwa ndani na wengi walijua nilikuwa nimesafiri.
Kabla ya kufungua shule mama aliniambia kwamba kutokana na hali niliyokuwanayo itabidi anichukulie uhamisho kisha ningeenda kuishi kijijini kwa bibi yaani kwao akina mama.
Aliniambia kwamba nitakaa huko hadi nitakapojifungua kisha nitaendelea na masomo, kufuatia kauli hiyo nililia sana kwani nilikuwa napenda sana kusoma.
Mama alinipa pole na kusema hakukuwa na jinsi zaidi ya kwenda kuishi kijijini kwa sababu kama ningeendelea kuwa pale Evance angepata matatizo makubwa na yeye pia.
Alinieleza kwa upole kwamba hakuwa na nia mbaya zaidi ya kutaka kunisaidia na alinitoa wasiwasi kwamba kule kijijini nitaishi vizuri na atanipatia huduma zote.
Kwa kuwa sikuwa na namna ya kufanya, nilikubaliana na mama na shule ilipofunguliwa alifanya taratibu zote za uhamisho na kufanikiwa ndipo niliondoka pale nyumbani na mama mdogo tukaelekea kijijini ambako ni mbali sana.
Nilipofika kijijini kila kitu kilikuwa kipya yaani mazingira na watu, mbaya zaidi nyumba ya bibi ambaye alikuwa akiishi peke yake haikuwa nzuri sana ilikuwa na mabati yaliyochakaa, haikuwa na sakafu ya saruji na choo hakikuwa kizuri.
Baada ya salamu mama mdogo alinitambulisha kwa bibi ambaye alimuuliza kama mimi ndiye yule msichana aliyeelezwa na mama kwamba alikuwa akiishi na mimi na kwetu Mbeya, akamwambia ndiyo.
“Karibu sana mjukuu wangu, nimefurahi kukuona hapa ndiyo kijijini kwetu karibu sana,” Dorcas anasema yule bibi alimwambia.
Nilimshukuru kwa kunikaribisha ndipo aliingia katika chumba kingine akatoka na karanga alizoziweka katika ungo mdogo na kutuletea akatukaribisha tule.
Kwa kuwa sikuwa napenda kula karanga mbichi, nilimshukuru lakini ni mama mdogo pekee ndiye alianza kutafuna karanga, bibi alipoona sili kama vile alijua kuna watu siyo wapenzi wa karanga mbichi akaniuliza anikaangie nikamwambia sawa.
Bibi aliyekuwa akipikia nje alitoka na kwenda kukaanga karanga ndipo mama mdogo akaniambia kwamba siku iliyofuata angerudi mjini kwa sababu ya majukumu yake.
Aliponiambia hivyo nilijisikia unyonge kwa sababu ya ugeni niliokuwanao nikawa najiuliza nitaishi vipi katika mazingira yale mageni ya kijijini!.
Nikiwa nawaza hivyo, bibi alirudi akiwa na karanga zilizokaangwa akanikaribisha ndipo mama mdogo akamuomba bibi wakaongee jambo f’lani, wakatoka nje.
Walipotoka nilijua mama mdogo alitaka kumweleza bibi masaibu yangu na lengo la mimi kwenda kule kijijini, baada ya dakika kama arobaini waliingia.
Bibi alinipa pole kwa yote yaliyotokea na kuniambia nisiwe na kinyongo na Evance kwani alifanya hivyo kwa sababu ya ujana na kwamba niwe na amani moyoni.
Kauli ya bibi iliniumiza sana kwani nilijua alisema vile kwa sababu aliyenibaka alikuwa mjukuu wake ambapo nilijiuliza kama angefanyiwa binti yao Emmy wangethubutu kusema aliyemfanyia hivyo alifanya kwa bahati mbaya.
Kutokana na uchungu nilioupata, kwanza wa kushindwa kuendelea kusoma, kubakwa na kupewa mimba nilijikuta nikitiririkwa na machozi.
Bibi aliyegundua niliumizwa sana na jambo hilo alianza kunibebembeleza ninyamaze na nivumilie na kwamba atanipa uangalizi mzuri mpaka nitakapojifungua kisha nirudi shuleni.
Kwa kuwa sikuwa na la kufanya, nililazimika kuwa mpole na kuendelea kumkumbuka marehemu mama na kujisemea kama angekuwa hai yote yaliyonitokea yasingetokea.
“Dorcas, nakuomba usiwaze sana jambo lililotokea, kwa kuwa upo na bibi naamini hautapungiwa na kitu na msamehe Evance hayo ni mambo ya vijana, naamini ipo siku atakusaidia kwani hata yeye anajutia kosa lake,” Dorcas anasema mama mdogo alimwambia.
Tukiwa tunaongea huku nikiwa sina furaha zaidi ya kusumbuliwa na msongo wa mawazo, alikuja mama mmoja ambaye nilitambulishwa kwamba alikuwa na undugu na mama.
Tuliposalimiana, bibi alimtambulisha kwamba nimetokea mjini nitakuwepo pale kijijini kwa muda mrefu, yule mama akamwuliza nitakuwa nasoma kule?
Kufuatia kuulizwa hivyo, bibi alimwambia hapana nilikwishahitimu darasa la saba hivyo nitakuwepo kule kijijini kwa muda mrefu bila kumwambia kama nilikuwa mjamzito.
Kwa kuwa tangu tulipofika tulikuwa tunapiga stori, yule mama alinikaribisha kule kijijini kisha akaaga na kwenda kwake ndipo bibi alimwambia mama mdogo aandae mboga ya majani, usiku tulipokula ugali nikaoneshwa sehemu ya kulala.
Kutokana na mazingira yale kuwa mapya na jinsi nyumba ilivyokuwa, sikuweza kupata usingizi mapema, lakini baadaye nilipitiwa na usingizi.
Kulipokucha mama mdogo aliondoka nikaanza rasmi kuishi na bibi ambaye awali tulikuwa tukienda naye shambani lakini kadiri siku zilivyosonga mbele nikashindwa na kuwa mtu wa kushinda nyumbani.
Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba ujauzito wangu haukuniletea matatizo ya kuumwa kama inavyowatokea wanawake wengine, isipokuwa nilikuwa sipendi kula.
Kilichonishangaza zaidi ni kitendo cha mama aliyeahidi kunisaidia kwa kila jambo kukata mawasiliano nami, wala hakuja kunijulia hali na nilipomuuliza bibi aliniambia kwamba huenda alibanwa na biashara zake.
Hata mama mdogo aliyeniacha kule kijijini naye alikata mawasiliano kabisa, kwa ujumla kitendo cha mama kutokuja kuniona kilinihuzunisha sana.
Mbaya zaidi sikuwa na fedha za akiba ambazo ningezitumia kama nauli ya kwenda mjini, kufuatia hali hiyo nikawa sina namna ya kufanya.
Maisha ya kule kijijini yaliniweka katika wakati mgumu sana kwani nilimkumbuka marehemu mama na mama mkubwa wa Mbeya ambao walinilea kwa upendo.
Nilikuwa najiuliza kwa nini mimi pekee nilikuwa naandamwa na mikosi, wa kwanza kutomfahamu baba yangu, kusumbuliwa na wachawi nilipokuwa Mbeya, kifo cha mama, kubakwa na kupewa ujauzito, kukatishwa masomo kisha kwenda kutelekezwa kijijini!
Mambo hayo yaliniumiza sana, kuna wakati bibi akiwa hayupo nyumbani nilijikuta nalia peke yangu na kuiona dunia haikuwa rafiki yangu hata kidogo.
Wakati nikiwa kule kijijini nilikuwa nakwenda katika zahanati moja ambapo zilitolewa huduma za kliniki, kila nilipopimwa niliambiwa mtoto alikuwa akiendelea vizuri na kupewa maelekezo mengine yaliyohusiana na masuala ya uzazi.
Hata hivyo, kitendo cha kutelekezwa na mama kule kijijini kilinifanya muda mwingi kuwa katika msongo wa mawazo na kujiuliza ilikuwaje mama aliyenishauri nikakae kule na aliyefahamu hali niliyokuwanayo anifanyie vile?
Kutokana na msongo wa mawazo niliokuwanao, yule mama wa kwanza kufika pale nyumbani kwa bibi alinigundua mara kwa mara nikawa nakwenda kwake kwa ajili ya mazungumzo nk.
Licha ya kufanya hivyo, aliponiuliza kuhusu mwanaume aliyenipatia ujauzito sikuthubutu kumtaja Evance kama mama alivyoniomba nisimtaje kuhofia mwanaye kupata matatizo ya kisheria.
****
Niliishi kule kijijini hadi ujauzito wangu ulipofika miezi tisa bila mama wala mdogo wake kuja kuniona, usiku nilipatwa na uchungu lakini kwa kuwa kituo kikubwa cha afya ambacho kinatoa huduma za uzazi kuwa mbali chupa ya uzazi ilipasuka.
Baada ya tukio hilo sikukaa muda mrefu kwa msaada wa bibi na jirani zake wawili nilijifungua mtoto wa kiume, kama inavyokuwa karibu kwa wanawake wote, licha maumivu kitendo cha kupata mtoto kilinifurahisha sana.
Akina bibi walinihudumia vizuri na kulipokucha tuliondoka pale kijijini kwa usafiri baiskeli mbili nikapelekwa katika kituo cha afya kilichotoa huduma ya uzazi.
Kwa kuwa nilijifungulia nyumbani, nilifanyiwa uchunguzi kama nilipata maambukizo yoyote lakini ilibainika nilikuwa salama mimi na mwanangu.
Hata hivyo, nilikaa pale hospitali kwa muda wa siku tatu ndipo niliruhusiawa kurudi nyumbani, bibi aliyekuwa akifuga kuku alinihudumia vizuri kama mazazi lakini tatizo sikuwa na nguo za kumvalisha mwanangu kwa sababu sikuwa na fedha.
Kutokana na hali hiyo, nilikuwa namfunga kanga zangu na za bibi, ila yule mama niliyekuwa napenda kwenda kwake aliniletea nguo kadhaa za mtoto.
Kwa kuwa nilihitaji sana kumuona mama na kuzungumza naye kuhusu hatima yangu ya masomo, nilimuuliza bibi kama alimtumia ujumbe kwamba nilijifungua, alisema alifanya hivyo na angefika muda wowote.
Hata hivyo, nilikaa majuma matatu, si mama wala mama mdogo aliyetokea nikaendelea kuishi katika mazingira magumu na mwanangu hadi nilipomaliza mwezi.
Kwa kuwa afya ya mwanangu na yangu zilikuwa nzuri, nilizungumza na yule mama jirani wa bibi anikopeshe fedha ili niweze kwenda mjini ambazo angerudishiwa na mama.
Mama huyo aliyekuwa akitegemea kupata fedha kwa kuuza mazao wakati wa minada, akaniambia nisubiri kama angezipata angenipatia tena bila kunikopesha kwa sababu alikuwa ananionea huruma maisha niliyoishi kule kijijini na mwanangu.
Hata kabla ya kunipatia fedha hizo, nilimshukuru kwa ukarimu wake nikamwambia nitamsubiri mpaka atakapozipata, maisha yakaendelea.
Niliendelea kuishi huku nikisubiri kupewa nauli na yule mama na kufikisha mwezi mmoja na nusu, siku moja usiku mwanangu alipatwa na homa kali pamoja na ugonjwa wa Inimonia akawa anashindwa kupumua vizuri.
Kwa kuwa ilikuwa usiku ilituwia vigumu kutoka tukaamua kusubiri kukuche ndipo tumpeleke zahanati lakini ilipofika saa tisa kuelekea saa kumi mwanangu alifariki dunia.
Awali sikufahamu kama mwanangu alifariki hadi bibi alipokwenda kuwaamsha majirani ambapo alikuja babu mmoja na mkewe, bwana mmoja aliyekuwa akipenda kuniita mjomba na Yule mama aliyeniahidi kunipatia nauli ya kwenda mjini.
Baada ya kuzungumza na bibi ndipo Yule mama aliniambia mwanangu alifariki dunia hivyo niwe jasiri kwa sababu ilikuwa bahati mbaya.
Taarifa hiyo ilinihuzunisha nikaanza kulia kwani licha ya changamoto nilizopitia nilimpenda sana mwanangu na sikuhitaji kumpoteza, akina bibi waliendelea kunibembeleza.
Hata hivyo, nilimchikia sana mama pamoja na Evance kwa vitendo walivyonifanyia, mama kunipeleka kijijini na kunitelekeza na kijana wakle kunibaka na kunipa ujauzito.
Pamoja na chuki niliyokuwanayo, sikutaka kumuonesha mtu yeyote hali hiyo zaidi ya kusema ipo siku Mungu angenilipia kwa ukatili niliofanyiwa, nilipomkumbuka mama maumivu yalizidi kuwa makali nikajikuta nalia kwa sauti.
Tangu muda alipofariki mwanangu, hatukulala tena hadi kulipokucha ambapo watu walikusanyika na kujadiliana namna ya kumpumzisha mwanangu.
Kulipokucha na majirani kukusanyika, yule bwana aliyekuwa anapenda kuniita mjomba, alishauri mama atumiwe taarifa kuhusiana na msiba wa mwanangu.
Hata hivyo, akina babu wawili walisema ni sawa lakini walishauri mwanangu azikwe siku ileile kwa sababu alikuwa bado mdogo kwa sababu hakukuwa na ulazima wa kumsubiri mama.
Pilikapilika za mazishi ziliendelea na ilipofika saa sita, alikuja mtumishi wa Mungu ikafanyika ibada ya mazishi
Baada ya msiba baadhi ya akina mama waliniuliza historia yangu lakini sikutaka kuwaambia ukweli zaidi ya kuwafahamisha kwamba mama yangu alifariki dunia na kwamba alikuwa rafiki wa mama wa Shinyanga.
Waliponiuliza kuhusu baba wa mtoto wangu, niliwadanganya kwamba kulikuwa na kijana alinirubuni na kunipa ujauzito kisha kutoweka ndipo mama akaamua kunipeleka kule kijiji nikae kwa bibi.
Akina mama hao walihuzunishwa na taarifa niliyowapa ambapo yule mama niliyekuwa napenda kwenda kwake alinipa moyo kwamba kila binadamu hukumbana na mitihani hivyo nisihuzunike sana.
Mama huyo aliongeza kuniambia, kikubwa ni kujifunza baada ya kukosea awali ili nisirudie tena kosa.
Alipotoa kauli hiyo niliumia sana moyoni kwa sababu tangu nilipojitambua nilikuwa makini ila Evance ndiye aliyeniingiza kwenye matatizo baada ya kunibaka.
Hata hivyo, sikuwa na jinsi zaidi kumshukuru Mungu na kupanga kuondoka kule kijijini kwa njia yoyote na kurudi mjini ambapo pia nilipanga nisingekaa ningeenda Mbeya kwa mama mkubwa.
Kila nilipokumbuka maisha ya upendo niliyoishi nilipokuwa na marehemu mama na mama mkubwa wa Mbeya, nilijuta kwa nini nilikubali kwenda kuishi Shinyanga.
“Kama ningekuwa Mbeya kwa mama mkubwa, wala nisingebakwa na kupata mimba na kutelekezwa huku kijijini kama vile sina thamani,” nilijikuta nikiwaza moyoni.
Wiki moja baada ya msiba wa mwenzangu sikuona sababu ya kuendelea kuishi kule kijijini, siku moja usiku nikiwa nimeketi na bibi nilimwambia anipatie nauli ili nirudi mjini.
Bibi aliniambia kwamba nisubiri mpaka mama atakapokuja, kauli yake ilinitibua nikamweleza kwa kitendo cha mama kunitelekeza kule bila msaada wowote sikuwa na sababu ya kumsubiri.
Licha ya umri wangu mdogo, nilimwambia bibi mwanaye alikuwa mtu mbaya sana na kumwuliza kama mjukuu wake Emmy ndiye angekuwa alipewa mimba angefanya kama alivyonifanyia.
Kumtetea mwanaye, bibi aliambia kwa anavyomfahamu mama akufanya vile kwa makusudi isipokuwa alihisi kuna jambo lilimbana hivyo nisimuwazie vibaya.
Nilimweleza hata kama angekuwa kabanwa hakunitendea haki kunipeleka kijijini huku akijua nilikuwa mjamzito afadhali hata kama angemtuma mama mdogo aje kuniangalia lakini wote hawakufanya hivyo.
Baada ya kuzungumza mengi na bibi, nilimwomba anitafutie nauli hata kwa kukopa kwa majira zake ili niende mjini, akaniambia nisubiri kukicha atanipa jibu.
Asubuhi bibi aliniaga kwamba anatoka kidogo ambapo alirejea kwenye saa tatu hivi akanimbia alizungumza na mtu mmoja aliyemuahidi kumpatia fedha jioni ya siku hiyo.
Taarifa hiyo ilinifurahisha, nilimsaidia bibi kazi mbalimbali na jioni ilipofika bibi aliondoka aliporejea aliniambia nijiandae kwa safari ya mjini siku iliyofuata.
Nilimshuru bibi, usiku huo niliweka nguo na vitu vyangu kwenye begi tayari kwa alfajiri kuanza safari, bibi aliponiuliza kama ningeweza kufika mwenyewe nikamwambia ningefika.
Kulipokucha, bibi alinisindikiza hadi sehemu ya kupandia magari tukakuta canter moja ikiwa imejaza watu na mizigo, nami nikapanda ambapo hatukukaa sana safari ikaanza.
Tulisafiri kwa muda mrefu ndipo tuliingia Shinyanga mjini, kwa kuwa nilikuwa mwenyeji niliposhuka kwenye gari nikabeba begi langu na kuanza kuelekea nyumbani.
Njiani watu waliokuwa wakinifahamu walinishangaa na kuniuliza mbona nilibadilika sana, badala ya kuwajibu nilianza kulia.
“Dorcas umepatwa na tatizo gani linalokufanya ulie?” dada aitwaye Jasmini alimwuliza.
“Nyie niacheni tu,” Dorcas aliwaambia.
Licha ya kuwaambia wamuache tu, Jasmini aliyehisi huenda Dorcas alikuwa na tatizo kubwa akazidi kumbana ili amwambie kilichomliza ndipo aliwadanganya kwamba alimkumbuka marehemu mama yake.
“Ooh jamani kumbe umefiwa na mama yako?” Jasmini alimwuliza.
Dorcas aliwajibu ndiyo ndipo wakazidi kumpa pole na kumwambia alikuwa na sababu ya kudhoofu kwani kufiwa na mama lilikuwa tatizo kubwa.
“Ndiyo hivyo, yaani kila ninapomkumbuka mama naumia sana,” Dorcas aliwaambia bila kujua kama kilichomliza ni kitendo cha kikatili alichofanyiwa na Evance pamoja na mama yake aliyemtelekeza kijijini.
Kwa kuwa wakati nazungumza na dada Jasmini na mwenzake ambaye sikumfahamu tulikuwa tumesimama, niliagana nao na kuelekea nyumbani.
Nilipokaribia kufika, rafiki zangu Ester na Kalunde waliponiona walinikimbilia wakanilaki kwa furaha kisha kunipokea begi, tukaongozana kwenda nyumbani.
Marafiki zangu hao, kama alivyofanya dada Jasmini, waliniuliza kama nilikuwa naumwa kwa sababu nilikuwa nimekonda na kubadilika tofauti na nilivyokuwa awali kabla sijaondoka.
Pia walinilaumu kufuatia kuondoka bila kuwaaga, niliwaambia niliondoka ghafla na kwamba hali ya hewa ya nilikokuwa ilinikataa kwani mara kwa mara nilikuwa naugua malaria.
Tulipofika nyumbani, Ester ndiye alibisha hodi na hatukukaa muda mrefu pale mlango Emmy alifungua mlango, aliponiona alinirukia kwa furaha!
Emmy ambaye naye hakufahamu jambo lililoniondoa pale nyumbani alifurahi sana na kunieleza alikuwa kanimisi sana, alibeba begi langu na kulipeleka chumbani.
Tukiwa tumeketi sebuleni nilimuuliza alikokuwa mama akaniambia alikwenda Mwanza kwenye shughuli zake za biashara, nilipomuuliza pia kuhusu mama mdogo akaniambia alikwenda Tabora kwa mzazi mwenzake.
Emmy alinifahamisha kwamba pale nyumbani alibaki na mama yake mkubwa, Edina na dada wa kazi ambaye wakati huo alikuwa ametoka.
Wakati tukizungumza, alikuja mama mmoja ambaye sikumfahamu kutokea kwenye korido ya kwenda vyumbani, mimi na akina Ester tulimwamkia.
“Dada Dorcas huyu hapa ni mama mkubwa anaishia Bariadi, mama mkubwa huyu ni dada Dorcas amefika muda mfupi uliopita,” Emmy alitoa utambulisho.
Mama huyo alinipa pole kwa safari na kunikaribisha lakini kwa nilihisi kama alikuwa anataka kuuliza jambo fulani akasita, baada ya muda akina Ester waliaga.
Kutokana na uchovu wa safari sikuwasindikiza badala yake Emmy alifanya zoezi hilo, tukiwa tumebaki na mama mkubwa aliniuliza mtoto wangu alikuwa wapi!
Kufuatia swali hilo nilijua alikuwa kaelezwa kila kitu na mama, swali lake lilinikumbusha mwanangu na ukatili niliofanyiwa, nikaanza kulia.
Mama mkubwa aliponiuliza sababu za kulia, nilimfahamisha kuwa mwanangu alifariki dunia siku chache zilizopita, taarifa hiyo ilimhuzunisha akanipa pole.
Nilimuuliza kama hawakupata taarifa ya msiba, akaniambia hakufahamu chochote, nikamwambia hivyo ndivyo ilivyotokea, akanipa pole tena.
Wakati tunaendelea kuzungumza na mama huyo, Emmy alifika ndipo tulisitisha maongezi yaliyohusiana na kifo cha mwanangu, Emmy aliyekuwa akinipenda aliniandalia maji ya kuoga nikaenda chumbani nikabadili nguo na kwenda bafuni.
Niliporejea sebuleni, nilikuta Emmy kaniandalia chakula na wakati napata mlo dada wa kazi alirejea tulisabahiana na Emmy akanitambulisha kwake.
Usiku nikiwa chumbani na Emmy, aliniuliza mbona nilirejea nyumbani kabla ya shule kufungwa, nilimdanganya kwamba nilikuwa naumwa hivyo niliomba ruhusa, akanipa pole.
Baada ya kupiga stori za hapa na pale, Emmy alipitiwa na usingizi lakini kwa upande wangu sikupata hata tone la usingizi badala yake nilisongwa na mawazo kuhusiana na kitendo nilichofanyiwa na watu wawili, mama na Evance.
Kutokana na kuwaza kwa muda mrefu nikapatwa na hasira nikaanza kulia, wakati huo Emmy alikuwa akiuchapa usingizi wa pono nikaamua kuchukua uamuzi mzito.
Licha ya kwamba sikuwa na fedha, nilipanga kukicha kuondoka Shinyanga na kwenda Mbeya kwa mama mkubwa ambaye niliamini ndiye aliyechukua nafasi ya marehemu mama.
Usiku huo Emmy akiwa amelala, nilikumbuka mama alikuwa akipenda kumuachia fedha za kutosha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na dharura zingine, nikaamka na kufungua kabati.
Baada ya kufanya hivyo, niliiona pochi ambayo Emmy alikuwa akihifadhia vitu nikahisi ilikuwa na fedha alizoachiwa na mama, nilipoifungua nikaona ilikuwa na noti za shilingi elfu kumi ambazo sikujua idadi yake.
Baada ya kufanya hivyo, niliiona pochi ambayo Emmy alikuwa akihifadhia vitu nikahisi ilikuwa na fedha alizoachiwa na mama, nilipoifungua nikaona ilikuwa na noti za shilingi elfu kumi ambazo sikujua idadi yake.
Kwa kuwa lengo langu lilikuwa kuchukua kiasi cha fedha kwa ajili ya nauli ya kwenda Mbeya, nilizihesabu na kubaini ilikuwa shilingi hamsini na nne elfu, nikachukua elfu thelathini.
Kiasi hicho cha fedha niliamini kingenifikisha Mbeya bila matatizo, sikupenda kuchua fedha zote kuhofia ningewapa usumbufu wa kukosa fedha za matumizi wakati sikujua mama angerudi lini.
Baada ya kufanya hivyo, nilizihifadhi kwenye moja ya mifuko ya siketi yangu kisha nilichukua karatasi na kuandika ujumbe ambao hadi leo naukumbuka vizuri.
Ujumbe huo niliandika maneno haya: Emmy mimi Dorcas siyo mwizi na sitakuja kufanya kitendo hicho katika maisha yangu hata kama nitakumbana na wakati mgumu kiasi gani.
Kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wangu nimefungua kabati na kukuta pochi yako ambayo ndani ilikuwa na shilingi hamsini na nne elfu, nimechukua shilingi elfu thelathini.
Najua nitakuwa nimeharibu bajeti yenu wakati huu mama akiwa hayupo lakini naomba mnisamehe kwa sababu sina jinsi nimeamua kuchukua fedha hizo ili nifanye nauli ya kwenda kwa mama mkubwa Mbeya.
Naomba Mungu unisamehe kwa kosa nililofanya kwa sababu sina jinsi, naomba mbaki salama na kwa amani kama Mungu akipenda tuonane tutaonana na asipopenda ipo siku tutaonana mbinguni, nakupenda sana Emmy kuliko mama na Evance.
Niombee nifike salama huko niendako, mimi Dorcas.
Nilipoandika ujumbe huo niliuweka ndani ya pocho niliyochukua zile fedha, nikaweka magauni yangu mawili ndani ya begi nikapanda kitandani kusubiri kuche ili nianze safari ya kwenda Mbeya.
Nikiwa macho, Emmy alijitikisa nikajifanya nakoroma ili asijue kama tangu niliponda kitandani sikupata usingizi, akajigeuza na kuangalia ukutani na kuendelea kuuchapa usingizi.
Alfajiri na mapema wote wakiwa wamelala, niliamka nikaoga kisha nikachukua begi langu, nikafungua mlango wa nyumba kubwa nikatoka kisha nikaufunga kwa funguo na kuziingiza ndani kupitia uwazi wa chini ya mlango.
Nilipofanya hivyo, nikafungua geti la kutokea nje kwa uangalifu bila kushtukiwa na kulifunga nikashika njia ya kwenda stendi, kwa kuwa bado kulikuwa na giza nilikuwa na hofu ya kukutana na vibaka.
Nikiwa natembea nikawa namuomba Mungu anipe ulinzi ili niweze kufika salama kwani sikutka kabisa kuendelea kuishi kwa mama ambaye hakuwa na upendo kwangu.
Wakati nikitembea ghafla nikasikia kengele ya baiskeli ile nageuka ikasimama pembeni yangu, moyo ukapiga pa!
Kijana aliyekuwa akiendesha kwa sauti nzito akanisalimia kwa Kiswahili chenye lafundhi ya Kisukuma; “Wewe msichana hujambo?”
Huku nikumuomba Mungu anilinde nikaitikia salamu yake na kumwamkia, akasema marahaba kisha akashuka kabisa kwenye baiskeli ambayo nyuma alifunga kiroba na kuchomeka panga kwenye mkanda wa kaptura kubwa aliyovaa.
“Unatoka wapi na unakwenda wapi usiku wote huu?” Dorcas anasema yule bwana alimwuliza.
Nilimweleza nilikuwa natoka nyumbani naenda kupanda basi kwani nilikuwa nasafiri kwenda Mbeya, akaniuliza nilikuwa natoka nyumbani wapi, nikamwelekeza mtaa ambao ulipakana na alioishi mama.
ITAENDELEA
Comments
Post a Comment