KILICHONITOKEA BAADA YA KUBAKWA NA KAKA YANGU - 5

 

KILICHONITOKEA BAADA YA KUBAKWA NA KAKA YANGU - 5

 



Simulizi : Kilichonitokea Baada Ya Kubakwa Na Kaka Yangu

Sehemu Ya Tano (5)


Nilipomweleza hivyo akasema sawa na kuniuliza kama nilikuwa nasoma, nikamjibu ndiyo na kumdanganya kwamba nilikuwa naenda Mbeya kwenye msiba.


Nilipomwambia hivyo, alichomoa panga na kunikazia macho.


Alipochomoa panga, akauangalia na kuurudisha kwenye hala kisha akaniuliza nilikuwa naenda kwenye msiba wa nani, kwa hofu niliyokuwanayo awali kwamba jamaa huyo alitaka kunidhuru nilivuta pumzi na kuzishusha kwa nguvu.


Japo mama alifariki dunia muda mrefu nilimwambia msiba wa mama, alisikitika sana akachukua begi langu na kulifunga juu ya kiroba kilichokuwa nyuma ya baiskeli yake.


Alipohakikisha alilifunga vizuri akaniambia nipande kwenye bomba la baiskeli kisha nikashika usukani akaisuma kama mita mbili, akadandia na kuanza kuendesha..


Njiani, alinipa pole tena kwa msiba na kuniuliza mbona nilikuwa nasafari peke yangu nikamdanganya kwamba ndugu zangu wengine walitangulia.


Aliendesha baiskeli kwa kasi hadi sehemu tuliyokuwa tukisubiria magari, kutokana na kunionea huruma, yule bwana hakuondoka mpaka lilipokuja gari aina ya Toyota Land Cruiser ambapo dereva alisema anakwenda Nzega.


Kwa kuwa nilielewa kama ningechelewa kupanda basi huenda Emmy angeamka na kukuta ule ujumbe na kuamua kunifuata, nilipanda gari hilo ambalo ndani kulikuwa na wanawake wawili, mmoja wa makamo, kijana wa miaka 15 hivi, mtoto na dereva.


Nilijua huko mbele ningeunganisha na magari ya kwenda Mbeya, yule bwana aliyenipa lifti ya baiskeli kabla ya kuniaga alinipatia shilingi elfu tatu na kunitakia safari njema ndipo gari likaanza safari.


Gari likiwa limeanza kushika kasi, mama aliyekuwa na mtoto akanisalimia kwa kusema; “ Hujambo binti!”

Nikaitikia salamu yake na kumpa heshima yake akasema marahaba ndipo nikakumbuka kwamba wakati napanda garini hatukusalimaina.


Tukasalimiana wote na kuendelea na safari, hatukutembea umbali mrefu, yule mama akaniuliza nilikuwa nakwenda wapi, nikamwambia akasema wao walikuwa wakienda jijini Dar es Salaam lakini watasimama Nzega kwa siku moja kisha kuendelea na safari.


Nilimwambia nikifika Nzega nitaunganisha safari yangu na magari yanayokwenda Dodoma kisha huko ningepanda la Mbeya, akasema sawa.


Kama unavyojua watu mnaposafiri pamoja huzungumza mambo mbalimbali, yule mama aliniuliza jina langu na Shinyanga nilitoka kwa nani.


Aliponiuliza hivyo, sikumjibu kwa wakati akaniuliza mbona nilionekana sikuwa sawa nikamwambia sikuwa na tatizo, akanibishia na kusema alikuwa mtu mzima hivyo nisingeweza kumdanganya na kusisitiza kwa alivyonioa kuna jambo lilinitatiza.


Alipotoa kauli hiyo, dada aliyekuwemo kwenye lile gari akaniambia kama nilikuwa nina tatizo niwaambie kwa sababu kwa wakati ule nilikuwa kama ndugu yao na hata kama lingetokea tatizo wao ndiyo wangenipatia msaada.


Kama vile waliambiana, dereva naye aliniambia kama nilikuwa na tatizo niwaeleze, awali nilitaka kuwaficha lakini nilisikia sauti ikiniambia niwaeleze kila kitu kilichonitokea.


Niliwafahamisha kwamba kuna mambo yalinitatiza ndiyo yaliyonifanya niwe safarini kwenda Mbeya kwa mama mkubwa, yule mama akaniuliza ni mambo gani, nikawaeleza waelewe tu hivyo nilivyowaambia.


Yule mama na dada walibaini niliwaficha kitu wakanibana kwamba niwaeleze, nilipokumbuka mambo waliyonifanyia mama na Evance nikajikuta natiririkwa na machozi.


Jambo hilo liliwapa wakati mgumu ndipo wakaanza kunibembeleza ninyamaze na kuwasimulia kila kitu, nikaamua kuwaeleza mkasa wangu mwanzo hadi mwisho.


Nilipofika mwisho, yule mama alishindwa kujizuia kulia, yule dada akawa mpole na kuniuliza kama yote niliyowaeleza yalikuwa kweli, nikawaambia yalikuwa kweli, wakasikitika sana.


Yule kijana aliyekuwemo kwenye lile gari alisema mama wa Shinyanga pamoja na Evance walitakiwa kushtakiwa ili sheria ichukue mkondo wake, nikawaambia sikuwa na mpango huo Mungu angenilipia.





Wote walimuunga mkono yule kijana kwamba nikafungue mashtaka dhidi ya mama na Evance, nikawaambia niliwasamehe na sikuwa tayari kuwashtaki,nikaanza kulia.


Kufuatia kulia, wote wakaanza kunisihi ninyamaze nikawaambia ingawa sikupenda kuwafungulia kesi na kumuacha Mungu, kitendo walichonifanyia kiliniumiza sana.


“Hata sisi tumeguswa na unyama uliofanyiwa ndiyo maana tunakushauri ukawashtaki ili sheria ichukue mkondo wake,” dereva aliniambia.


Nilimwambia sawa lakini siku moja Mungu angewahuku kwa sababu yeyote anayewafanyia wengine ubaya, malipo yake yapo hapa hapa duniani.


Walipoona sikukubaliana na ushauri wao,waliniacha tukaendelea na safari huku kila mmoja akiwa ananionea huruma, kabla ya kufika Nzega yule mama aliniita jina langu na kunipa pole kwa yote yaliyotokea na kuwalaani mama na Evance.


Mama huyo ambaye tayari alijua hata Mbeya kwa mama mkubwa nilikokuwa nakwenda hakukuwa kwa ndugu zangu wa damu, aliniomba kama sitajali niongozane naye kwenda nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.


“Mwanangu, mkasa wako umenigusa sana, kama hautajali naomba twende tukaishi wote nyumbani kwangu Dar es Salaam, nitakutafutia shule ili uendelee na masomo na utakuwa miongoni mwa watoto wangu,” Dorcas anasema yule mama alimwambia.


Kwa kuwa nilijua hakuna kitu kitakachonikomboa maishani mwangu kama elimu, nilifurahi sana kupata nafasi hiyo adimu ambayo nilikuwa naamini ilipotea, nikamkubalia yule mama.


“Nashukuru sana mwanangu kukubali kwenda kuishi nami, hata mume wangu nikimwambia habari zako atasikitika na kukupokea bila kinyongo,” Dorcas anasema yule mama alimwambia.


Nilimshukuru sana kwa ukarimu wake huo, hata yule dada alimuunga mkono tukaendelea kuzungumza na huku safari ikiendelea na kuwasili Nzega mapema.


Tulipofika tukaenda nyumbani kwa ndugu yao, katika maongezi yao waliambiwa mama aliyekuwa mwenyeji hakuwepo nalikuwa amekwenda Igunga.


Kufuatia taarifa hiyo, tuliondoka Nzega kwenda Igunga kwa ndugu yao mwingine ambako tulimkuta yule mama, baada ya maongezi waliamua kuelekea Dar.


Njiani tulikuwa tukizungumza mambo mengi utafikiri tulifahamiana muda mrefu, yule dada niliyemkuta mle kwenye gari kumbe naye alikuwa abiria.


Katika maongezi alitusimulia mateso aliyowahi kupata kutoka kwa mama yake wa kambo namna alivyokuwa akilala bila kula huku akiwa amefanya kazi kutwa nzima.


Alitueleza kuwa kila alipomweleza marehemu baba yake mambo ambayo alifanyiwa na yule mama, alimgeuzia kibao na kumchapa na kumtuhumu alikuwa muongo.


Mkasa wake ulituhuzunisha sana ambapo aliniambia nisihuzunike sana kwani kila kinachotkea katika maisha yetu kinakuwa na sababu.


Alisisitiza kama nitarudi shuleni nisome kwa bidii kwani ni elimu pekee ndiyo ingeweza kunikomboa na kunifanya nisahau yote yaliyonitokea, akaniambia nimshukuru sana yule mama aliyeamua kunichukua niende kwake Dar kwa ajili ya kusoma.


Nilimshukuru yule dada kwa kunipa moyo, tulipofika Singida alituaga kwani alikuwa amefika, kwa jinsi tulivyozoeana tulihuzunika lakini hatukuwa na la kufanya zaidi ya kutakiana heri.


Baada ya yule dada kuteremka, yule mama ambaye mpaka muda huo sikuelewa kama lile gari lilikuwa lake au la nani alimwambia dereva akipata abiria amchukue ili tupate pesa ya matumizi njiani.


Dereva aliondoa gari hadi maeneo ya stendi kuu ya Singida akawaeleza akina mama f’lani kwamba alikuwa akielekea Dar na kulikuwa na nafasi ya mtu mmoja.


Mama mmoja mwenye asili ya Kiarabu aliyekuwa na pochi alichangamka akaingia kwenye gari, safari ikaanza huku kila mmoja akiwa kimya hadi dereva alipoyumbisha gari wakati akiwakwepa mbuzi waliokatiza barabarani.


Kufuatia kuyumba huko kwa gari, yule mama wa kiarabu alipata mshtuko akaangukia upande wa kulia wa kiti alichokuwa ameketi na kupoteza fahamu.

Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni nicheki kupitia namba hizo hapo juu.


Kitendo cha yule mama kupoteza fahamu kilitukosesha raha, dereva alisimamisha gari pembeni ya barabara tukaanza kumpepea kwa kutumia gazeti lakini hakuzinduka.


“Huyu atakuwa na tatizo la presha, sasa sijui tufanyeje?” dereva alimwuliza mama.


Kwa kuwa mama alikuwa na uzoefu wa mamboya tiba alishauri tutafute sehemu iliyokuwa na kimvuli tuegeshe gari kisha akipigwa na upepo angezinduka.


Alipotoa ushauri huo, dereva alilipeleka gari chini ya mti wenye kimvuli ambapo palikuwa na hewa ya kutosha akafungua milango yote ya gari.


Mama hakuacha kumpepea ghafla yule mama akafumbua macho na kuanza kuangaza huku na huko,hali iliyotupa matumaini, mama akamwuliza alijisikiaje!

Yule mama wa Kiarabu hakujibu badala yake aliendelea kuangaza tu macho yake,mama akasema tumuache kama dakika kumi au zaidi angezinduka kabisa.


Kwelikama alivyosema, baada ya kupita kama dakika kumi na tano, yule mama aligeuza shingo upande aliokuwa mama na kumuuliza tulikuwa wapi.

“Tupo safari tunaenda Dar es Salaam,” mama alimjibu.


Alipoambiwa hivyo, alishangaa na kuuliza; “Tunakwenda Dar es Salaam kwa nani?”

Kufuatia swalilake tulijikuta tukiangua kicheko ndipo mama alimwambia tulikuwa safarini lakini kwa bahati mbaya tulipata tatizo lililomfanya we katika hali ile.


Mama alimwuliza kama hakukumbuka chochote,yule Mwarabu alitulia kwa muda na kuuliza begi lake lilikuwa wapi, mama akamuonesha, alipoliona alitabasamu.


Baada ya kufanya hivyo, aliinuka kisha kuuliza kwa nini dereva aliegesha gari chini ya mti,mama akamsimulia kilakitu kuhusu tulivyonusurika katika jail.


Alipoambiwa hivyo, alimshukuru Mungu ndipo alituambia alikuwa na tatizo la presha ambalo lilimfanya anaposhtuliwa na jambo f’lani alikuwa akipoteza fahamu.


Mama huyo, alifungua begi lake akatoa vidonge akameza viwili na kushushia na maji, akasema alikuwa sawa hivyo tuendelee na safari.


Maongezi yaliyojiri yalikuwa kumlaani mmiliki wa wale mbuzi kufuatia kitendo chake cha kuwaacha wakirandaranda hovyo barabani bila uangalizi.


Dereva aliendesha gari hilo kwa kasi hadi tulipofika Dodoma, tukaenda kula kisha safari ya Dar ikaendelea.


Mungu jalia tulifika Dar, salama salimini na kupokelewa na watoto wa yule mama, yule kaka aliyekuwa akiendesha gari ambaye mpaka muda huo sikufahamu walikuwa na uhusiano gani alituaga na kuondoka na yule kijana mwingine.


Baada kuweka mizigo na mabegi sehemu husika, yule mama alinikaribisha kwa kuniambia pale palikuwa nyumbani kwake hivyo niwe huru kwa kila jambo.


Aliniambia kwamba mumewe hakuwepo na kwamba angerudi usiku ndipo alinitambulisha kwa binti mmoja ambaye alisema ni dada yaani binti wa kazi, akasema anaitwa Tabu.




Aliniambia kwamba mumewe hakuwepo na kwamba angerudi usiku ndipo alinitambulisha kwa binti mmoja ambaye alisema ni dada yaani binti wa kazi, akasema anaitwa Tabu.


Alinitambulisha pia kwa binti mwingine ambaye alionekana kama alisoma darasa la sita au la saba, akaniambia anaitwa Beatrice ambaye alizoeleka zaidi kwa jina la Bite.


Wakati ananitambulisha akafika dada mwingine ambaye alinipita kidogo umri, akasema alikuwa akiitwa Monica na kwamba ndiye alikuwa bintiye mkubwa.


Akiwa anaendelea na zoezi la utambulisho, nilimuona kijana akitokea kwenye korido akija sebuleni,umri wake haukuwa tofauti na wa Monica na walionekana kufanana.


Mama akamwita kwa jina la Barton, alipoitika akamwambia walipata mgeni yaani mimi ndipo akanitambulisha kwamba Barton na Bite walikuwa mapacha,nikasalimiana naye.


Baada ya salamu kijana huyo alimuaga mama yake kwamba anakwenda kwa rafiki yake kisha akaondoka, kwa kuwa tayari usiku ulianza kuingia mama alimsihi asichelewe kurudi, akamwambia sawa.


Muda mfupi baadaye Tabu aliniambia maji ya kuoga yalikuwa tayari, tuliongozana hadi chumbani walikokuwa wakilala mabinti nikabadili nguo kisha kwenda kuoga.


Nilipomaliza zoezi hilo nilirejea sebuleni na kukuta chakula kimeandaliwa, kama unavyoelewa taratibu za watu wa mjini kula pamoja, tuliokuwepo tulikusanyika mezani isipokuwa Barton na baba.


Wakati tukiendelea kula,Barton alirejea na kujumuika mezani tukawa tunapiga stori za hapa na pale huku tukipata mlo lakini cha kushangaza kijana huyo alikuwa akinitupia macho kijanja.


Tukiwa tunaendelea kula, baba wa familia hiyo ambaye alikuwa na umri wa utu uzima alifika, alifurahi sana kumuona mkewe, wakasalimiana na kuulizana habari za safari.


Baada ya salamu, alinisabahi nami nikamuamkia ndipo mkewe alinawa ili waongozane kwenda chumbani lakini akamzuia kwamba amalizie kula.


Mama hakukubali, alinawa na kumfuata mumewe nahisi ni kwa vile alimkumbuka, hata hivyo hawakukaa muda mrefu walirejea pale sebuleni na kukuta tumemaliza kula.


Kwa kuwa nilizoea kuwa bize na kazi za nyumbani, wakati Tabu anakusanya vyombo tulivyolia chakula nami niliungana naye lakini mama akanizuia.


“Mwanangu Dorcas hebu pumzika, muache Tabu afanye kazi hiyo yaani umefika leo tu hata kupumzika bado unataka kuwa bize?” mama aliniambia.


Nilimweleza asijali kwa sababu mwanamke huwa hana mapumziko, akacheka na kuniambia nipumzike kama ni kazi nitafanya siku nyingine, nikasema asante.


Tulipomaliza kuzungumza na mama na kurejea kuketi kwenye sofa, baba alinikaribisha Dar na kuniambia niwe huru kwa wenzangu na kwao,nikamshukuru.


Siku hiyo nyumba ilichangamka kwa furaha kwani tulikaa pale sebuleni tukiangalia runinga huku tukizungumza hadi muda wa kulala ulipofika,mama na baba walikwenda kulala.


Kwa kuwa nilikuwa nimechoka kwa safari, Tabu aliniambia twende tukalale na kuwaacha Bite,Monica na kaka yao Barton ambao nilivyowasoma kwa muda mfupi niliokaa nao nilibaini walipenda sana kuangalia tamthiliya na muziki.


“Karibu sana Dorcas,mimi na wewe tutalala kitanda hiki na akina Bite watalala hapa,” Tabu alinifahamisha.

Tukiwa tumejilaza kitandani, baada ya kuzungumza mawili matatu kuhusu Jiji la Dar lilivyokuwa na joto nilipitiwa na usingizi hata akina Bite walipoingia kulala sikuwasikia.


Kulipokucha, Tabu alipoamka nami niliamka kwa ajili ya kusaidiana kazi za nyumbani, licha ya kunisihi nimuache aendelee na jukumu hilo lakini sikumuelewa.


Kutokana na msimamo wangu, nilimuuliza karo la kuoshea vyombo lilikuwa wapi akanionesha, nilitoa vyombo vichafu na kuanza kuviosha.


Wakati nafanya kazihiyo, Tabu alikuwa akipiga deki ndani na kupanga vitu,muda huo Bite na Monica walikuwa wamelala lakini sikutaka kumuuliza.


Kama unavyojua kazi inapofanyika kwa ushirikiano inakwisha haraka, Tabu alimaliza kupiga deki akachukua fagio la nje na kuanza kufagia.


Kwa kuwa nyumba hiyo ilikuwa na eneo kubwa,nilimuuliza kama kulikuwa na ufagio mwingine ili nimsaidie. Tabu aliyekuwa kafurahia ‘kampani’ yangu alinipatia aliokuwa akiutumia na kwenda stoo akachukua mwingine.


Tukiwa tuna furaha tulifagia uwanja wote kisha tulirejea jikoni ambapo nilimuuliza kuhusu maandalizi ya chai akaniambia pale huwa wanapenda sana kunywa uji wa ulezi asubuhi ndipo vyakula vingine hufuatia.


Tabu aliwasha jiko la mkaa, wakati tunasubiri moto ukolee aliamka Barton na kuja moja kwa moja jikoni akatusalimia kisha alifungua chupa iliyokuwa na maji ya moto akayapoza kidogo kwa kuchangana nay a baridi na kunywa lita moja.


Kitendo hicho kilinishangaza sana kwani sikuwahi kumuona mtu akinywa maji mengi kiasi kile baada ya kuamka tu kabla ya kupiga mswaki.


“Vipi dada mgeni naona kama unashangaa?” Barton aliniuliza.

Nilimwambia alinishangaza alivyokunywa maji kiasi kile, kijana huyo ambaye mwili wake ulionekana wa mazoezi alicheka na kuniambia ilikuwa kawaida yake kufanya hivyo.


Aliponieleza hivyo, akamimina tena maji kwenye glasi na kunywa glasi mbili hivi, akiondoka akiwa anacheka kuelekea kwenye korido sehemu iliyokuwa na viatu akavaa raba.


Barton alipovaa raba,alichukuwa maji kwenye jagi akajongea uwanjani akanawa uso kisha alituaga kwamba anakwernda kwenye mazoezi.


“Hivi akitoka huko jambo la kwanza nikunywa uji yaani anaweza kumaliza hata ukijaa kwenye hii bakuli,” Tabu aliniambia.


Nilibaki kushangaa kwani kwa sikuamini, Tabu alinifahamisha kwamba kwa kuwa nilikuwa mwana familia ile ningeshuhudia kwa macho yangu.


Mama alipoamka na kukuta tumefanya usafi wa mazingira,kupiga deki, kuosha vyombo na kupika uji alifurahi sana na kusema wasichana ndiyo wanavyotakiwa kuwa.


Mama alimwuliza Tabu kama aliweka maji ya kuoga baba bafuni,ambapo alimweleza alikwishayaweka, akasema safi sana ndipo aliingia ndani. Hazikupita dakika nyingi baba alitoka na kutusalimia.

Aliniuliza kuhusu uchovu wa safari nikamwambia nilikuwa vizuri akasema asante kisha akaenda kuoga, alipomaliza mama naye aliingia bafu kwa ajili ya zoezi hilo.


Baba alipopata kifungua kinywa alikwenda kazini,tukiwa tumebaki na mama alituita sebuleni na kutuambiakwambia tulimfurahisha sana kwa jinsi tulivyofanya kazi za nyumbani.

Nilimwambia asijali kwa sababu jukumu hilo lilikuwa letu, tulipomaliza kunywa uji, wakati mimi naosha vyombo Tabu alitoa rundo la nguo chafu tayari kwa kuanza zoezi la kufua.


Kwa kuwa vyombo havikuwa vingi, nilimaliza haraka nikaungana na dada huyo wa kazi kufua nguo ndipo Bite na Monica walipoamka, tulisalimiana nao.

Nilishangazwa na kitendo cha wasichana hao kuamka karibu saa tatu kasoro kisha kupiga mswakina kwenda kunywa uji wakati wenzao tuliamka mapema na kufanya kazi karibu zote.


Tukiwa tunafu nilimwuliza Tabu kuhusu tabia hiyo, msichana huyo alitabasamu na kuniambia niachane nao kwani alikwisha wazoea.


Nilimwuliza kuwazoea kivipi, akaniambia huwa hawanyi kazi yoyote labda wakipenda tena zile ndogondogo lakini kazi zote za nyumbani akuanzia kufua, kupika, kuosha vyombo, usafi wa mazingira alikuwa akifanya yeye.


Hakuishia hapo, aliniambia hata kwenda sokoni kununua mahitaji ya jikoni na vitu vingine alikuwa akienda yeye na mama waowalifanya hivyo mara chache.




Tabu aliniambia niachane nao kwani kuna siku watakuja kuona athari za tabia hiyo ya kudeka na kutegemea kila kitu wafanyiwe na yeye, nikaishia kushangaa.


Nilikaa wiki nzima utaratibu wa kufanya kazi za nyumbani ukiwa kama nilivyoukuta, sikuwa na kinyongo kwani lengo langu kubwa lilikuwa kusoma ili niwe na elimu itakayonikomboa katikamaisha yangu.


Siku moja usiku nikiwa nipo chumbani na Tabu, aliniambia kwa Barton alikuwa muhuni sana kwani mara kwa mara alikuwa akimtongoza lakini alimkataa.

Aliponiambia hivyo, nikamwambia hata mimi amekuwa akiniangalia na kuna wakati ananikonyeza lakini nashindwa kumkalipia kuhofia kumkwaza mama yake.


Tabu akaniambia hiyo ndiyotabia yake na kuna wakati kama pale nyumbani wengine wanakuwa hawapo akijua Tabu yuko chumbani alikuwa akienda kuimgongea mlango lakini alikuwa hafungui.


Taarifa alizonipatia Tabu kuhusu Barton zilinikumbusha kitendo nilichofanyiwa na Evance,nikajikuta nalia na kujiuliza moyoni kwa nini kila ninapokuwa nakutana na majaribu?


Msichana huyo wa kazi ambaye kwa muda mfupi tulipatana sana, aliponiuliza sababu za kulia nilmdanganya kichwa kilikuwa kinauma kwani sikutaka kabisa kumweleza historia yangu.


Kwa upendo aliinuka nilipomuuliza alitaka kwenda wapi akaniambia kuchukua panadol,nilimwambia huwa nikinywa maji mengi kinapoa na kumsihi asimwambie mtu yeyote kama nilikuwa naumwa kichwa.

“Kwan nini hupendi niwafahamishe?” Tabu aliniuliza.


Nilimwambia aache tu, nikinywa maji kitapoa na kwamba huwa sipendi hata vitu vidogo kuwaambia watu, Tabu akanielewa na kwenda kuchukua maji ya kunywa.


Nilikunywa maji hayo kwa kumzuga tu Tabu ukweli nilikuwa naujua mwenyewe, nikajikuta naapa moyoni kwamba Barton asingeweza kunibaka kwani siku atakayojaribu kuniltea ujinga wake ndiyo angejua.


“Sitakubali tena kubakwa,siku atakayojaribu kuniletea ujinga wake nitamuua kama kwenda kufia jela nipo tayari,” nilijisemea moyoni.


Tukiwa tunapiga stori na Tabu, akina Bite na Monica walikuwa wakiangalia runinga waliingia chumbani,tukabadili mazungumzo ambapo haukupita muda mrefu tukapitiwa na usingizi.


Kulipokucha kama kawaida, mimi na Tabu tukawa bize na kazi na ilipofika saa tatu hivi alifika yule dereva tuliyetoka naye Shinyanga, akina Bite, Barton, Monica na Tabu walimchangamkia na kumwita mjomba.


Kufuatia kumwita hivyo nilijua kumbe alikuwa kaka wa yule mama, baada ya salamu aliniuliza nilikuwa naendeleaje nikamwambia safi, wakati huo mama naye alikuwepo.


Mjomba huyo aliponiuliza kama nilianza shule nikamwambia bado, akauliza kwa nini nikamwambia bado mama hakunitafutia.


Kabla hajaendelea kuzungumza, mama alidakia na kumweleza kwamba tayari zoezi hilo lilianza na baba ndiye alikuwa akifuatilia, mjomba akasema hapo sawa.


Baada ya kuambiwa hivyo, mjomba alifurahi sana ndipo alimuuliza dada yake za tangu walipoachana siku ile tuliyotoka Shinganya akamwambia zilikuwa nzuri.

Mjomba aliyeonekana kuwa na haraka, kabla ya kuondoka alitoa pochi yake akachomoa noti mbili za shilingi elfu kumi na kumpatia mama na kusema atununulie nyama kisha akaaga na kuondoka.


Ingawa tangu nilipofika sikumsikia mama akizungumzia suala langu la shule, nilifurahishwa na upendo aliouonesha mjomba kwa kumuuliza mama jambo hilo.


“Huyu mjomba inaonekana anapenda sana mambo ya shule, maana alipofika tu hapa suala la kwanza kutaka kujua ni kama nimeanza kusoma,” niliwaza.

Nikiwa chumbani na Tabu baada ya mjomba kuondoka,mama ambaye tangu nilipofika sikuwahi kumuona akiwa bize kwa kazi yoyote alituiita.


Tulipokwenda kuitikia wito alituambia kwamba tuchukue mahindi, ulezi na karanga tuchambue kisha twende tukasage unga kwa ajili ya uji ambao ulipendwa sana na familia ile.


Wakati anatuambia hivyo, akina Bite na Monica walikuwa sebuleni wamewasha runinga wanaangalia muziku, kitendo hicho kilinikwaza nilipozungumza na Tabu akaniambia niachane nao.


“Dorcas usipende kuishi kwa kushindana, mimi hao nimewazoea kikubwa omba Mungu uanze kusoma kama mama alivyokuahidi,” Tabu aliniambia.


Nilimshukuru Tabu kwa ushauri wake, tulipomaliza kuchambua mahindi,karanga na ulezi mama alitupatia hela tukashika njia kwenda mashineni.


Tukiwa njiani Tabu alinisimulia historia ya maisha yake kwamba kwenye familia yao walizaliwa wawili na kaka yake ambaye wakatihuo alikuwa akitumikia kifungo kwa kesi ya kusingiziwa.


Alinifahamisha kwamba kiasili kwao ni Kigoma vijijini na kwamba wazazi wake walikufa kwa Ukimwi na kuwaacha wadogo, akasimama na kuanza kulia.

Kufuatia hali hiyo nilibaini alikumbuka jambo lililomuumiza nikamsihi anyamaze, akatulia na kusema;


“Hata hii kazi naifanya kwa sababu ya matatizo tu kwani naamini kama baba na mama wangekuwa hai licha ya kwamba walikuwa ni wakulima wa jembe la mkonona maskini, nisingezifanya zaidi ningesoma kwa bidii ili elimu inikomboe,” Tabu aliniambia.


Tabu alinifahamisha kwamba kaka yake aliyeitwa Samweli alikuwa gerezani akitumikia kifungo cha miaka miwilio baada ya kusingiziwa aliiba baiskeli.


Alisema tukio hilo lilimuumiza sana kwani kabla ya kufungwa alikuwa msaada sana kwake kwani fedha alizopata baada ya kufanya vibarua ziliwawezesha kupata mahitaji yao na walikuwa wanapenda sana.


“Kila nikimkumbuka kaka naumia kwani yupo gerezani anatumikia kifungo kisicho halali, kama kweli angekuwa ameiba ningesema alijitakia, kweli hii dunia wakati mwingine haina huruma,” Tabu aliniambia na kuanza kulia tena.


Kitendo cha Tabu kulia, kilinikumbusha mateso niliyopita kikiwemo kitendo cha kubakwa na Evance, nikajikuta name ninalia kitendo kilichowafanya akina mama wawili waliotuona tukiwa tumetua mfuko wa mahindi kutufuata na kutuuliza tulipatwa na masaibu gani.


Kwa kuwa sikupenda kuwaambia ukweli niliwadanganya kwamba tulipata taarifa ya msiba wa mdogo wetu huko Mbeya, walitupa pole na kutuambia tusilie turudi nyumbani.


Mama mmoja alipotueleza hivyo, tulitulia walipoendelea na mambo yao nasi tulibeba mfuko wetu na kuelekea mashineni, bahati mbaya tulipofikahuko tulikuta umeme umekatika.


Tukiwa tunasubiri Tabu aliniambia baada ya kaka yake kufungwa na maisha ya kijijini kuwa magumu alichukuliwa na dada mmoja na kumleta Dar kwa ajiliya kufanya kazi za ndani.


Aliongeza kuwa, alipokaa na dada huyo miezi sita alianza kumfanyia visa ndipo msichana mmoja rafiki yake alimshauri aache kazi ndipo alimtafutia kazi kwa mama Bite.


Tabu aliniambia hata kwa mama huyo alikuwa anavumilia mengi kwa sababu alikuwa mkali hata kwa mambo yasiyostahili na kuna wakati alipokesea jambo alikuwa akimchapa na kumtukana.

Aliponiambia hivyo na jinsi nilivyomuona mama huyo nilimwuliza kama aliyoyasema yalikuwa yana ukweli akanimbia kweli lakini sikuamini na kuhisi Tabu alikuwa na matatizo tu!






“Mama mwenye moyo wa upendo namna ile aliyeamua kunichukua na kuahidi kunisomesha awe na roho mbaya kama anavyosema huyu Tabu, sidhani hawezi bwana!” nilijisemea moyoni.


Kule mashineni tulizungumza mengi lakini moyoni niliamini mama Bite alikuwa mama mzuri sana na kuhisi Tabu alikuwa na mambo yake yaliyomfanya mama huyo kumuadhibu kama alivyoniambia.


Umeme uliporudi tulisaga na kurejea nyumbani, tulipofika mama alimwuliza Tabu tulichelewa wapi, akamwambia hakukuwa na umeme.


“Eti Dorcas mmechelewa kwa sababu hakukuwa na umeme au huyu mwenyeji wako alikuwa kwa wanaume zake, sema ukweli?” mama aliniuliza.


Licha ya kumwambia umeme haukuwepo tuliamua kusubiri mama hakuelewa alisema alinifundisha niseme uongo kwa sababu pale nyumbani palikuwa na umeme.


Bila kufahamu kwamba eneo tulilokuwepo ilitokea hitilafu ya umeme,mama alimdaka Tabu na kuingia naye ndani, akaanza kumtandika huku akisema hataki wasichana malaya katika nyumba yake.

Licha ta Tabu kilia na kumwambia mama hakuwa kwa wanaume aamini maneno yetu hakumwelewa, alimtandika hadi fimbo aliyokuwa akiitumia ikawa vipandevipande.


“Dorcas, kwa kuwa nimeamua kuishi na wewe hapa sitaki uige mambo ya umalaya kama anayoyafanya huyu kinyago, anakufundisha uongo na wewe unakubali, ole wako mimi sitaki mambo ya ujinga na upuuzi,” Dorcas anasema mama Bite alimwambia.


Aliongeza kuwa hataona shida kunifukuza nyumbani kwake licha ya kuniahidi kutaka kunisomesha na kwamba hakutaka tuwafundishe watoto wake tabia mbaya.


Baada ya mama kumpa kichapo Tabu, alimwambia tukaendelee na kazi, japo wakati huo hatukuwa na kazi ikabidi tutafute cha kufanya,Tabu akaenda chumbani na kutoa nguo za akina Bite tukaanza kuzifua.


Wakati tunafanya kazihiyo, Tabu alikosa raha akawa anatiririkwa machozi kufuatia kitendo cha mama kumuadhibu bila kosa.


Nilimsihi awe na amani na avumilie lakini akaendelea kulia na kuniambia alikuwa amemvumilia sana mama na kufikia tamati na kwamba hata kama kwao walikuwa maskini atarudi kuliko kuendelea kuteseka.


Manenoya Tabu yalinihuzunisha sana kwani alichokiongea kilikuwa kweli tupu, hata hivyo nilimsihi asiwe na hasira akaniambia alichoshwa na manyanyaso.


Siku hiyo Tabu alishinda akiwa mnyonge, tukiwa chumbani kwetu alifungua begi lake na kutoa baadhi ya nguo zilizokuwa zinambana akanipatia kwa vile sikuwa na nguo nyingi.


Hakuishia hapo, alinipatiajozi mbili ya viatu,nilifurahi sana kwa upendo wake. Jioni ilipofika mimi na akina Bite tulikaa nje tukawa tunapiga stori na kumuacha Tabu chumbani.


Nyumba tuliyokuwa tunaishi ilikuwa na milango miwili mmoja wa kuingia nyumba kubwa na wa uani, wakati tunazungumza Tabu alitoka kwa kupitia mlango wa uani na kutoweka.


Aliyekuwa wa kwanza kubaini Tabu hakuwepo pale nyumbani alikuwa Bite, kwani chumbani kwetu hakukuwa na begi na vitu vyake vingine.


Tulipobaini hakuwepo tulitoka na kuwaliza majirani ndipo mama mmoja alisema alimuona akiwa kabeba begi na mfuko wa Rambo na alipomuuliza alikuwa akienda wapi alimwambia lilikuwa begi la mgeni wetu.


Kufuatia Tabu kutoroka, mama aliingia chumbani na kuuliza kama hakuchukua vitu visivyomhusu, ulipofanyika ukaguzi kila kitu kilikuwepo kasoro begi la Tabu na vitu vyake.


Bite alipoangalia ndani ya begi langu alikuta zile nguo nilizopewa na Tabu na viatu vilivyokuwa uvungu wa kitanda, akaniuliza nani aliziweka nikamwambia alikuwa amenipatia, akaenda kumwambia mama.


Mama aliingia chumbani na kuniuliza kuhusu nguo hizo nikamwambia nilipewa na Tabu, akaanza kunishambulia kwamba nilikuwa najua mpango wake wa kutoroka akanizaba kibao nikaangukia kitandani.

Alipoona nimeangukia kitandani, aliniinua huku akinitukana na kunipiga kibao kingine nikaanza kulia.


“Wewe kinyago leo utanitambua, unajifanya unashangaa Tabu kutoroka wakati unajua kila kitu, kwa nini hukuniambia mapema,” Dorcas anasema mama alimjia juu.


Nikiwa naendelea kujitetea kwamba sikuelewa chochote alimtuma Bite aende akamchukulie fimbo, mwanaye alikwenda uani na kurudi na fimbo ya mti wa muarobaini.


Mama alinitoa mle chumbani na kunipeleka sebuleni akaanza kunitandika hadi alipokuja mama wa jirani aliyesikia wakati nikilia na kuuliza sababu za kunichapa.


Mama alimfahamisha, yule mama alimsihi asiendelee kunichapa ndipo alisema ilikuwa bahati yangu nilipata mtetezi lakini siku ile ningemtambua.


Nakumbuka siku hiyo sikula chakula cha usiku, nikiwa chumbani kwangu nilikumbuka mengi nikalia sana na kumkumbuka marehemu mama yangu pamoja na mama mkubwa wa Mbeya.


Hata hivyo, sikuwa na la kufanya kwani kilichonifanya niwe nyumbani kwa mama Bite ni kusoma kama alivyoniahidi, nikaamua kuvumilia kwa sababu hapakuwa na mtu wa kunisaidia kupata elimu.


Usiku baba aliporejea alisimuliwa kila kitu kuhusu kutoweka kwa Tabu, baba alishauri kukicha mama akatoe taarifa polisi ili kama atapata tatizo wasije kuhusishwa.


Kulipokucha, kablaya baba kwenda kazini aliniita sebuleni na kuniuliza rafiki yangu Tabu aliniaga anakwenda wapi, nikamwambia sikuelewa chochote.

Licha ya kuniuliza mara kadhaa nami kusisitiza sikufahamu chochote aliridhika niliongea ukweli, akamwambia mama kwamba lakini mama hakukubaliana naye.


Baada ya baba kuelekea kazini, nikaanza kufanya usafi wa nyumba nzima, nilipomaliza niliosha vyombo na kuinjika uji. Wakati huo akina Bite na kaka yao Barton walikuwa wanauchapa usingizi.


Kwa upande wa mama, mumewe alipoondoka alirudi chumbani kwake, sikuelewa kama alikuwa amelala au alikuwa akifanya kitu gani.


Kwa kuwa tangu nilipoamka sikuwa nimefungua kinywa, nilichukua mkate ambao baba alikujanao pamoja na blue band nikamimina chai kwenye kikombe nikaanza kunywa.


Nilifanya hivyo kwa sababu sikuwa mpenzi sana wa uji, nikiwa nimeketi sebuleni sehemu ya kulia chakula nakunywa chai, mama alitoka chumbani kwake.


Aliponiona alisimama na kujishika kiuno kisha kunikata jicho, kitendo cha mama kufanya hivyo kilisababisha moyo kupiga paa kwani nilielewa hakupenda ninywe chai!


“Hivi wewe kinyago nani kakuambia unywe chai tena kwa mkate wenye siagi, unajua huo mkate kaletewa nani?” Dorcas anasema mama Bite alimwuliza.

Aliponiuliza hivyo nilipata hofu nikashindwa kumjibu kwa sababu sikuona kama nilifanya kosa na sikuwa na nia ya kula mkate wote, alipoona nimekaa kimya aliniuliza;


“Wewe si nina kuuliza mbona umekaa kimya au ndiyo kiburi cha kwenu?”

Nikiwa bado nimepigwa na butwaa na kushindwa kumjibu, alinifuata akanishika mkono na kunivuta, niliteleza na kuanguka chini.


Licha ya kuanguka mama hakunionea huruma aliniinua na kunipiga kibao kabla sijakaa sawa akaniongezea kingine nikaona nyota zikitembea usoni.


Kwa maumivu niliyopta nilianza kulia na kumuomba msamaha mama kama nilikosea anisamehe hakuridhika akaendelea kunipiga na kunishambulia kwa matusi.


Wakati akinipiga huku akivuta sketi yangu ilinifuka nikabaki na nguo ya ndani pekee, nikiwa katika hali hiyo Barton aliyesikia nikilia aliamka na kuja sebuleni na kunikuta nikiwa na nguo ya ndani pekee.




Sikuelewa sababu ya Barton kuendelea kuniangalia badala ya kuondoka, nilijiuliza kama aliyekuwa akipigwa au kuwa katika hali ile angekuwa dada yake Bite au Monica angevumilia kuwaangalia.

Jambo la kushangaza, mama hakujali aliendelea kunishambulia mpaka Bite na Monica walipoamka na kuhoji sababu za kuadhibiwa namna ile.


“Huyu msichana ni jeuri sana, mimi namwuliza badala ya kunijibu ananikunjia sura, hivi hanijui eh?” mama aliwaambia mabinti zake.


Wakati akinizushia uongo huo nilifanikiwa kuvaa sketi yangu na kuzidi kumuomba msamaha mama japo sikuwa na kosa, lengo langu lilikuwa anisamehe ili aache kunishambulia.


“Bahati yako umelitambua kosa lako, ukirudia tena nitakufukuza hapa nyumbani kwangu,” mama aliniambia.

Nafsi yake iliporidhika, alimwambia Bite aende akachukue fedha za matumizi alizoziweka juu ya meza chumbani, zilipoletwa aliniambia niende sokoni nikanunue mboga na viungo.


“Muone kwanza, hebu kamalizie chai yako ila usirudie tena upuuzi wako wa kuamua kunywa chai bila kupewa maelezo na wenye nyumba,” Dorcas anasema yule mama alimwambia.


Nikiwa sina amani, licha ya kujongea pale mezani nilishindwa kunywa chai nikabaki nimejiinamia na kumkumbuka marehemu mama.


“Hivi kama mama na baba yangu wangekuwepo sidhani kama ningepitia mateso haya, hivi ni lini nitaishi kwa amani kama watu wengine, lini nami nitakuwa na furaha hapa duniani?” niliwaza.


Wakati nawaza hivyo, mama aliniambia kama sikuhitaji kunywa chai niende sokoni nikanunue mboga kisha nipike ili wasijechelewa kula.


Niliinuka na kuelekea chumbani kwa lengo la kubadili siketi na kujiweka sawa,nilipoingia niliwakuta Monica na Bite wakiwa wameketi kitandani ndipo Bite akaniambia nisimfanyie ujeuri mama yao.


“Dorcas,unaona huo ujeuri wako umesababisha mama akuchape makofi na kama hutajirekebisha anaweza hata kukufukuza hapa nyumbani,” Dorcas anasema Bite alimwambia bila kujua sababu ya mama yao kumchapa.


Aliponiambia hivyo, sikumjibu chochote,nilibadili nguo nikaenda jikoni nilikochukuwa kikapu na kuelekea sokoni.

Niliporejea nikatakata nyama na kuiinjika jikoni, wakati huo akina Bite walikuwa wanajiandaa ili waende mjini.


Walipokunywa chai waliacha vyombo walivyonywea mezani kisha wakaondoka.

Kwa kuwa niliwazoea,nilivikusanya na kwenda kuviosha huku nikiwa nina msongo wa mawazo. Kufuatia hali hiyo nilisahau kama nilikuwa nimeinjika nyama.


Aliyenishtua alikuwa Barton aliyenifuata na kuniambia ilikuwa ikiungua nikatoka mbio kwenda jikoni na kukuta sehemu kubwa ya kitoweo ikiwa imeungua na harufu ya kuungua ikiwa imetanda jiko zima.


Nilichofanya ni kuipua lakini kabla sijafanya chochote mama aliyesikia harufu ya nyama kuungua aliingia, kama alivyofanya asubuhi alijishika kiunoni na kuniuliza nilikuwa nimefanya nini!


Kwa hofu nilishindwa kumjibu ndipo akaniuliza nilifanya nini nikamwomba msamaha kwa kuunguza nyama kwa bahati mbaya, akatoka mle jikoni. Moja kwa moja nilijua anakwenda kufuata fimbo.


Kabla hata sijachukua hatua ya kutoka nje aliingia akiwa amefura kwa hasira, kabla hajaanza kunitandika nilipiga magoti na kumwomba msamaha kwamba nyama iliungua kwa bahati mbaya hakunielewa, alinitandika bakora ya mgongoni.


Baada ya kunitandika, alinyanyua tena fimbo ili anichape begani nikakinga mkono, hapo nikawa nimemuongeza hasira akanimbia kumbe nilikuwa najua kukinga fimbo yake!


Alipotoa kauli hiyo alinizaba kibao cha nguvu upande wa kushoto nilipojishika kufuatia maumivu niliyopata alinizaba tena kibao upande wa kulia, nikasikia masikio yakivuma.


Mama aliniambia hapendi kuishi na mtu jeuri akaitupa fimbo chini, akaniambia nitafute fedha zangu nikanunue nyama nyingine. Kwa kuwa sikuwa na fedha niliomuomba msamaha, akanisonya.


“Kumbe unajua kuunguza tu wakati huna hata hela mjinga wewe, hivi huko ulikotoka ulikuwa unakulanyama?” mama aliniambia kwa kebehi.


Wakati akiniambia hivyo, bado masikio yangu yalikuwa yakivuma, alichokifanya alimtuma biti akanunue nyama na kuniambia niipike na ole wangu iingue tena.


Siku hiyo nilikosa raha kwa maumivu na uchungu wa kupigwa bila sababu, nilipokula nilishindwa kabisa kufanya kazi yoyote nikaingia chumbani kulala. Kufuatia kipigo cha mama nilipoteza uwezo wa kusikia vizuri kutokana na makofi aliyonipiga masikioni.


Nilipomwambia mama akanieleza nimuondolee upuuzi wangu na kusema kama sikusikia vizuri yeye afanyeje.

Kauli hiyo iliniumiza sana, kulipokucha kabla hawajaamka nikaenda mtaa wa pili alipokuwa akiishi dada aitwaye Stellah niliyekuwa naelewana naye sana na alijua mambo yangu mengi.


Nilimwelezea suala zima la kupigwa na manyanyaso niliyopata na kumuomba anisaidie fedha ili niende Mbeya kwa mama, mkubwa.


Stellah aliyekuwa akifanya biashara alihuzunika sana, alinipatia shilingi 30,000 kisha alinifahamisha kwamba jioni ya siku hiyo angehamia kwenye nyumba yake huko Kimara, akasema kabla sijaenda Mbeya alitaka nikapafahamu.


Alinieleza kuwa sikutakiwa kabisa kuendelea kuishi kwa yule mama, akasema nikifika nyumbani nikusanye vitu vyangu halafu niende pale kwake kisha twende Kimara.


Nilifurahi sana, nilipofika nyumbani wote walikuwa wamelala, nilichukua begi langu na vitu vyangu vyote nikaenda kwa dada Stellah.


Kuhofia kuonekana tuliondoka na kuelekea Kimara, nilimpongeza kwa kujenga nyumba nzuri alishukuru kisha aliniacha kwa jirani yake hadi jioni alipohamia.


Alfajiri dada Stellah alinisindikiza Ubungo akanikatia tiketi ya kwenda Mbeya, nikiwa safarini niliwaza mambo mengi la kubwa ni kumsimulia mama mkubwa masaibu yaliyonikuta.


Safari yangu ilikuwa nzuri kwani niliwasili Mbeya saa 12.15 jioni, nilipoteremka Mwanjelwa nilipanda daladala za kwenda Soko Matola nikashuka Kituo cha Sido na kukatisha njia ya mkato kuelekea kwa mama mkubwa.


Nilipokaribia mtaa aliokuwa akikaa mama mkubwa mama wa kwanza kukutana naye alikuwa mama Ambokile, alishangaa aliponiona na kunipongeza kwa kuwa mkubwa.


Licha ya kuzungumza mawili matatu na mama huyo alionesha alikuwa na jambo moyoni mwake,nilipomuuliza mama mkubwa hajambo aliniambia hajambo.

Hata hivyo, alinifahamisha kwamba alihamia Usangu hivyo twende nikalale nyumbani kwake ili kukicha nianze safari ya kwenda Usangu alikohamia, nilipopewa taarifa hiyo nilikosa raha.


Tulipofika kwa mama huyo ambaye alipoongea name nilikuwa simsikii vizuri, aliniandalia maji ya kuoga pamoja na chakula, lakini moyo wangu ulikosa utulivu kabisa.


Usiku tukiwa tumekaa jikoni tukiota moto,mama huyo aliyekuwa mjane aliniambia kuna jambo alitaka kuniambia lakini niwe jasiri kwa sababu hakuona sababu ya kunificha.


Nikiwa mwenye shauku ya kujua jambo hilo alinifahamisha kwamba mama yangu mkubwa alifariki dunia kwa ajali ya kugongwa na gari miezi mitano iliyopita.

Taarifa hiyo ilinifanya nianze kulia kwani sikujua hatima ya maisha yangu ingekuwaje,mama alinipa pole.

Nilipomuuliza alizikwa wapi japo nikalione kaburi lake akaniambia alizikwa kijijini kwao Tukuyu.


Hakika niliona dunia imenitenga, nililia sana lakini hakuna kilichobadilika ukweli ulibaki mam mkubwa kipenzi cha mama yangu alifariki dunia. Nilikaa Mbeya siku tatu ndipo yule mama akanipa nauli nikarudi Dar kwa dada Stellah aliyenipokea kwa upendo.


Nikiwa naishi kwa dada Stellah aliyekuwa ananipenda sana na kuahidi kuishi name katika maisha yake yote, kadiri siku zilivyokwenda masikio yangu yalipoteza uwezo wa kusikia.


Baada ya kuhangaikia tiba bila mafanikio alinipeleka Muhimbili ambapo nilifanyiwa vipimoa kugundulika masikio yangu yalipata matatizo makubwa hivyo nisingweza kupona.


Siku hiyo nililia sana na kumuuliza Mungu kwa nini niliandamwa na matatizo katika maisha yangu, wakati nazungumza hivyo dada Stellah aliyenishawishi niandike kisa changu ili jamii ijifunze jambo alinisikia na kuniambia nisiseme hivyo kwa sababu misukosuko katika maisha ni jambo la kawaida.


Nilimwambia sikatai lakini kwangu ilikuwa imezidi akanimbia niwe na amani ipo siku nitapona na kusahau yote yaliyonitokea na nitakuja kushangaa siku nitakayokutana na baba pamoja na ndugu zangu.


Kutokana na msongo wa mawazo niliokuwa nao, licha ya kupata kila kitu kwa dada Stellah nilijikuta nashindwa kula na kupoteza kabisa uwezo wa kusikia yaani nikawa kiziwi nikawa nazungumza kwa ishara.


Jambo hilo liliniumiza nikajikuta nadhoofu kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele, siku moja nilipatwa na malaria kali nikapelekwa Hospitali ya Muhimbili ambapo iligundulika nilipungikiwa dawa na maji nikalazwa.


Mpenzi msomaji, taarifa mbaya ya kuumiza niliyopewa na dada Stellah aliyekuwa akiishi na Dorcas ni kwamba mpendwa wetu huyo alifariki dunia Desemba mwaka jana siku ya tano baada ya kufikishwa Muhimbili ambapo msiba huo ulikuwa nyumbani kwake.

Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.


*MWISHO.*

Comments