MOYO WA KUPENDA

 

MOYO WA KUPENDA



SIMULIZI FUPI: MOYO WA KUPENDA
MAALUMU KWA SIKU YA WAPENDANAO!!

AJALI mbaya ya gari iliyotokea maeneo ya sabasaba nje kidogo ya mji wa Musoma iliwashangaza watu sio tu kwa jinsi ilivyokuwa ajali ya mbaya sana lakini kwa namna gani wahusika waliweza kutoka wakiwa bado wanavuta pumzi.
Hayakuwa makosa ya dereva bali makosa ya wakandarasi waliokuwa wakitengeneza daraja. Hawakuweka alama zinazoonekana vyema kwa madereva juu ya ukarabati uliokuwa ukiendelea mbele.
Bwana Johnson pasi na kujua akiwa na mkewe ndani ya gari mwendo wa kawaida tu wa kilomita 65 kwa saa walifikia eneo lile wakitambua wazi kuwa mbele palikuwa na njia.
La haula! Palikuwa na shimo kubwa sana na refu kuelekea chini!!
Gari ikaenda hewani.
Linapokuja suala la ajali ndugu zangu ni vigumu sana kujikinga.
Walishasema wazee wetu. Ajali haina kinga!!
Johnson alijitazama yeye kivyake huku mkewe naye akijitazama kivyake. Huyu alipiga kelele za kuita mama huyu naye akashindwa cha kufanya na kubaki mdomo wazi.
Baada ya sekunde kadhaa gari likajipigiza chini katika lile shimo kisha kujiviringisha zaidi ya mara mbili kabla ya kutulia tena.
Amini kuwa hakuna aliyepoteza maisha lakini Jesca mkewe Johnson alivunjika kiuno na pia kuvunjika baadhi ya mbavu,. Alikutwa amepoteza fahamu.
Johnson hakuumia zaidi ya kupata michubuko!!
Hakuna jitihada alizofanya ili kuepuka kuumia. Kwa pamoja huwa tunasema ni kudra za mwenyezi Mungu tu!!
Upesi Jesca alikimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Musoma. Lakini hakudumu sana pale akaandikiwa kufikishwa Bugando jijini Mwanza, hali ikawa tata zaidi na kuamuriwa kuwa ni Muhimbili pekee ambapo anaweza kufanyiwa upasuaji.
Johnson hakuwa tajiri sana lakini kwa msaada wa ndugu na marafiki wakafanikisha Jesca akafikishwa Muhimbili kitengo cha mifupa (MOI) huko akafanyiwa upasuaji.
Ilikuwa inaumiza na kusikitisha sana, mfupa mmoja katika nyonga yake ulikuwa umenyofoka vibaya na kukichoma kizazi chake.
Haikuwa lazima uwe daktari ama uonyeshwe kwa vitendo ili ujue ni maumivu kiasi gani alikuwa anapitia dada yule.
Na wakati huo ndoa yao ikiwa na mwaka mmoja tu!!
Madaktari walifanya jitihada sana kiutulivu.
Jesca alilala kitandani miezi ipatayo sita!!
Johnson akaona si vyema kuendelea kukaa hospitali basi yeye akarejea Mwanza ambapo ndo alikuwa na shughuli zake akaendelea kufanya kazi ili kuweza kukidhi haja!!
Lakini huo ndio ukawa mwanzo mbaya!!
Hatimaye Jesca akatoka hospitali.
Wakaendelea kuishi pamoja, na hapa ndipo tofauti ikaanza kujionyesha Jesca hakuwa na uwezo ule wa kumfurahisha Johnson kitandani, angeweza vipi kukukuruka ilhali alivunjika vibaya na ilikuwa bahati sana kuendelea kutembea.
Angeweza vipi jiulize??
Johnson hakujali hayo akaanza kujisikia fadhaa, huenda alimpenda Jesca kwa sababu ya utundu wake kitandani. Tutajuaje??
Licha ya kushindwa kumpa Johson atakavyo bado pia hakuweza kuhimili uzito wa Johnson kwa walau dakika 15. Jesca akawa anachoka upesi sana.
Naam! Johnson akajisahau kabisa kuwa ni yeye alikuwa dereva siku ile ambayo wanapata ajali na mkewe, akasahau kabisa kuwa alikuwa ni mkewe wa ndoa na aliapa kutomsaliti kwa shida yoyote ile.
Johnson akathubutu kwenda kuionja ladha ya nje.
Akatafuta binti ambaye hajavunjika kiuno wala hajawahi kupata ajali!!
Very stupid in did!!
Johnson akaanza kulala nje, Jesca akiuliza anajibiwa kuwa kazi zimekuwa nyingi sana eti alivyokuwa amelazwa alikopa sana hivyo anafanya kazi mara tatu zaidi ili aweze kulipa madeni.
Ikawa usiku ikawa mchana. Jesca akawa anaumia sana moyoni, akamuuliza Mungu ni kwanini aliruhusu ajali ile itokee ikiwa hata hajapata mtoto mmoja. Ikiwa hata hajayafurahia maisha ya ndoa ambayo aliyasubiri kwa muda mrefu!!
Jesca akawa mtu wa kutokwa machozi tu!! Alitamani sana kumjua mwanamke yeyote yule ambaye amekuwa tayari kushiriki mapenzi na Johnson na kumsahaulisha kabisa kuwa yu katika ndoa!!
Jesca alifanya hatua zake taratibu sana. Mafaniko yalikuwa hafifu sana lakini aliamini kuwa yapo njiani yanakuja.
_______
14.02 (SIKU YA WAPENDANAO)
Sebule ilikuwa imepambwa haswa, kila kitu kilikuwa chekundu.
Sarah alikuwa ameungana na rafiki zake wane, walikuwa wanakunywa bia huku muziki ukitoka katika sauti ya wastani.
Ilikuwa ni saa mbili na kwa pamoja walikuwa wakimngoja Johnson ambaye alikuwa ni hawara wake Sarah.
Sarah alimuomba sana waonane siku hiyo ya wapendanao ili aweze kufurahi naye pamoja.
Jesca pia alimuomba Johnson wawe pamoja usiku ule lakini Jonhson akadai kuwa kama ni sikukuu ya wapendanao wamesheherekea sana hivyo siku hiyo hakuwa na muda kwa ajili ya jambo hilo. Jesca akatikisa kichwa akajitazama kiuno chake.
“Ningekuwa kama zamani wala asingekataa!!!” akajisemea kisha akafunika kombe mwanaharamu apite!!
Majira ya saa mbili na nusu Johnson mwenye tabasamu pana kabisa alifika katika nyumba ambayo ilikuwa maskani yake ya pili. Alikuwa amempangia ile nyumba Sarah!!
Alipoingia akapokelewa na harufu nzuri ya marashi, akaingia na kukutana na mashemeji zake wa siku zote ambao kwa pamoja walitambua kuwa Johnson ameoa lakini bado yupo na Sarah. Hawakuwa na cha kujali kwa sababu Johnson alikuwa akiwasaidia shida zao ndogondogo!!
Wakamsalimia kwa kumkumbatia, ukafuata utani wa hapa na pale na hatimaye ukafika muda wa Johnson kupewa zawadi ambayo alikuwa ameandaliwa na huyo hawara!!
Akiwa mwenye tabasamu lake vilevile akaamuriwa kufumba macho kwa dakika moja.
Na aliporuhusiwa kufumbua almanusura apoteze fahamu.
Alikuwa akitazamana na mwanamke akiwa amevaa shera nyeupe sana. Hakuwa akitabasamu bali huzuni iliutawala uso wake.
“Johnson mume wangu!” ilikuwa sauti kavu kutoka kinywani mwa Jesca mkewe…
“Nipo mbele yako hapa mume wangu, kama ni vyema basi nioe mara ya pili. Nakupenda John na unalijua hilo, nd’o maana nilikuwa tayari kuacha kila kitu ili tu unioe na kuwa mume wangu!! Johnson unaniumiza sana mume wangu, unaniua polepole mume wangu, tazama hii ni shela ileile ya siku ile ya harusi yetu, angalia hainitoshi tena!! Inanipwaya, nimekonda sana John wangu, usinikondeshe zaidi ya hapa basi kwani moyo umekonda zaidi kwa sababu yako, nitakufa huku nikiwa nimesimama Johnson. Nina moyo wa nyama, siwezi kuyavumilia yote haya. Unaniacha mpweke Johnson, kisa tu siwezi tena kukufurahisha tukiwa sirini. Johnson mume wangu sikuwahi kuyapanga haya sikuwahi kupanga eti nipate ajali.
Muogope Mungu Johnson…….. twende nyumbani John nipeleke basi nyumbani ukanifanye unavyotaka hata nikifia kitandani basi nife nikiwa nakufurahisha wewe nipeleke nyumbani Johnson ” akasita akajifuta machozi kisha akamgeukia Sarah!!
“Sarah asante kwa kunipa nafasi hii ukiwa kama mwanamke uliyeguswa na magumu yaliyonitokea… asante kwa kunionyesha upendo katika siku hii ya wapendanano.. naomba nikukumbatie Sarah…. “ akamsogelea Sarah na kumkumbatia, lakini ajabu kumbatizi lile likawa la kushangaza. Sarah akampokea Jesca ambaye alikuwa yu katika kupoteza fahamu!!
Hekaheka zikaanzia pale wakampepea huku Johnson akiwa ametawaliwa na aibu kuu. Maneno ya Jesca mkewe yalikuwa yamemgusa sana moyo!!!
Baadaye Jesca alipatwa tena na fahamu zake. Johnson akamwongoza hadi katika gari, kabla hawajaingia garini Sarah akamkumbusha kitu.
“Licha ya kwamba gari hii imebadilishwa rangi kumbuka mara ya mwisho mimi kuingia katika gari hii nilikuwa natabasamu kabisa lakini huo ukawa mwisho wa tabasamu. Nakumbuka ulinibeba siku ile na kuniingiza garini. Hebu iwe kama siku ile!!” Jesca alimaliza.
Johnson akiwa anajilazimisha kutabasamu alimnyanyua mkewe akiwa katika vazi lake la shera. Akamwingiza katika gari kisha naye akaingia. Akawasha na kuondoka!!!
Naam! Jesca alisamehe kwa kila kitu na maisha yakaendelea tena upya!!
LILE KOVU KATIKA MOYO LIKAFUTIKA MAPENZI YALE YANACHANUA MPAKA SASA. HAKUNA MTOTO WALA HATAKUWEPO LAKINI WAMEAMUA KUWA MWILI MMOJA KWA KUMAANISHA!!!
UJUMBE!!
Mapenzi ni safari ambayo haijanyooka kuna mabonde na milima, mbebe vyema mwenza wako panapo milima na mabonde ili kwa pamoja mtabasamu inapokuja tambalale!!!

Comments