NIPE NAFASI NYINGINE

 

NIPE NAFASI NYINGINE



Niliolewa mwaka 1994, na kijana mmoja kutoka mkoani Kigoma. Huyu mwanaume kwakweli sikumpenda hata kidogo, kwani niliolewa naye kwa sababu ni chaguo la wazazi wangu. Mume wangu alijitahidi kunionesha ananipenda, na alinijali kwa kila kitu. Mume wangu, bwana Michael Kalinye, akijua kuwa sikumpenda, alitumia kila njia aliyoweza kunifanya nimpende. Alikuwa mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi. Ni kati ya wafanyabiashara wa zamani kidogo hivyo hali yake ya uchumi ilikuwa nzuri.

Kwangu niliwekewa wafanyakazi wa ndani wawili na mmoja nje wa usafi. Mume wangu alihakikisha ninaishi maisha mazuri. Sikupungukiwa na pesa, nguo wala chochote ambacho nilihitaji. Tuliishi Kigoma, lakini mara kadhaa tulisafiri kwenda Dar es Salaam, Arusha, na hata nje ya Tanzania kwa mapumziko. Mume wangu hakuwa muongeaji sana, na naweza sema alikuwa na asili ya upole, na hivyo hata kama ningemkosea, hangenisema wala kunilaumu. Mara chache sana aliniambia kwa upole mno kuwa hakupendezwa. Alijitahidi kutoniudhi, alijaribu kila namna kunifurahisha.

Tuliishi miaka mitatu bila kupata mtoto jambo ambalo mimi lilinisumbua sana akili. Mume wangu hakuonesha kujali kiasi kwamba hata nilipomgusia alionekana kuchukulia kirahisi sana akisema watoto ni zawadi tuu ya ndoa, hata tusipopata bado ndoa inaweza kuwa nzuri. Kwa upande wangu niliona ndoa hii na mwanaume nisiyempenda haitakuwa na faida kwangu kama sitakuwa na watoto. Nilianza kuhangaika kwa madaktari kutafuta mtoto. Nilimlazimisha Michael hivyo tukawa tukitembelea wataalam kadhaa kwa ushauri. Sikuonekana kuwa na tatizo lolote kila tulipopimwa. Hospitali ya kwanza tuliyotembelea sote tulionekana kuwa sawa baada ya vipimo, ambapo daktari alitupa ushauri tuu na kuahidi kwamba ningeweza kupata ujauzito. Lakini tulikaa tena zaidi ya miezi sita bila matokeo yoyote.

Nilianza kukata tamaa na kumlazimisha Michael twende kwa daktari mwingine. Mara hii tulienda lakini yeye hakukubali kufanya vipimo. Kwa kawaida wanaume kupima uzazi huhitaji kupeleka mbegu, na wanaume wengi hawapendi hilo suala. Nilimuelewa mume wangu, hivyo tukawa tukienda kwa madaktari tunapewa ushauri tuu au mimi ndiye napimwa lakini yeye hapimwi.

Kipindi chote hicho, nilikuwa bado naendelea na uhusiano wangu kwa siri na Severin. Huyu kijana nilianza naye uhusiano zamani kabla sijaolewa. Nakumbuka miezi michache kabla ya ndoa yangu nilibeba ujauzito wa Severin, lakini kwa kuhofia itakuwaje, nilitoa ile mimba. Mbaya zaidi, bila kujua, Michael ndiye aliyenipa pesa ya kutolea mimba, kwani hali ya uchumi ya Severin haikuwa nzuri. Mwanzoni mwa ndoa yetu nilijiweka mbali kabisa na Severin, kwa kuhofia kama Michael angejua ningepata shida kwenye ndoa. Lakini baada ya kuanza kusumbuliwa na suala la watoto nilianza kumtafuta tena ili kujifariji. Tulianza mahusiano ya kuonana tuu bila kufanya chochote. Niliogopa, nikihisi Michael angejua na labda angefanya kitu cha ajabu, kwani najua watu wapole huwa wana hasira mbaya sana.

Baada ya kutafuta watoto kwa muda bila kupata ushirikiano mzuri wa Michael, nilianza kutafuta faraja zaidi kwa Severin. Nilianza uhusiano wa mapenzi naye, tukazidi kuwa karibu. Huo ulikuwa mwaka wa tano wa ndoa yetu. Wakati huo nilisimamia baadhi ya biashara zetu ambazo mume wangu aliziweka chini yengu. Kiukweli mume wangu alinipenda mno, na alionesha kuniamini sana kiasi cha kunipa uhuru kufanya kila kitu bila kufuatiliwa. Hakuonekana kuwa mwenye wivu namimi lakini mara nyingi alirudia kuniambia kuwa siku akigundua nina mwanaume mwingine hatanisamehe. Hakuonekana kunifuatilia kwa namna yoyote, sio kwa simu wala kwa njia yoyote, japo pia nilikuwa makini sana asigundue uhusiano wangu na Severin.

Siku moja nikiwa kwenye moja ya ofisi zetu, nilianza kuhisi kichwa kinaniumwa kwa nguvu sana na homa kali. Niliita dereva anipeleke hospitali, nikampigia simu Michael ambaye alikuja upesi pale hospitali. Alikuta nimechukuliwa vipimo na kupumzishwa kidogo, akanipa pole. Nikiumwa Michael alionesha kunijali kunijali kama mtoto mchanga. Baada ya muda daktari alikuja akiwa na karatasi mkononi. Alionesha sura ya tabasamu huku akitupongeza mimi na mume wangu, sikuamini kusikia nina ujauzito, na ghafla maumivu ya kichwa na udhaifu ukaisha, nikainuka kwa haraka kumkumbatia Michael. Cha kunishangaza mume wangu hakuonekana kufurahishwa hata kidogo na habari ile. Nikamtazama kwa muda nikiwa na mshangao, akawa mnafiki kidogo mbele ya daktari na kunipongeza. Nilipata matibabu kidogo siku hiyo, nikaruhusiwa kurudi nyumbani. Tulirudi na Michael, lakini tukiwa kwenye gari hakuonekana mwenye furaha. Moyoni niliamua nitaachana kabisa na Severin kuanzia siku hiyo kwani sikutaka tena kumsaliti Michael. Nilisema sasa Mungu amenipa kila kitu, hivyo inatakiwa niwe mwanamke muaminifu kwa ndoa yake.

Kuanzia siku hiyo Michael alinibadilikia sana. Tofauti kabisa na matarajio yangu, hakuonesha kunijali hata kidogo. Mimba ilinisumbua kwa kutapika mara kadhaa, homa za hapa na pale na hali za kujisikia vibaya, lakini mume wangu hakuonesha kujali. Nilikaa ndani nikilia, mara chache nilijaribu kumwambia kuwa amebadilika, lakini hakuonesha kujali bali alinijibu kifupi kuwa yuko sawa. Ujauzito wangu ulikuwa safari yenye mateso, nilitamani kupata faraja kwa Severin lakini niliogopa, ila pia Severin alipojua nina ujauzito aliogopa na kuanza kujiweka mbali namimi. Baadaye nilikata kabisa mawasiliano na Severin, nikabaki mpweke, nisiyeelewa nini kimetokea kumbadilisha mume wangu. Hata hivyo sikuwa na ujasiri wa kulalamika. Michael alinipatia kila nilichohitaji, isipokuwa wakati wote wa ujauzito wangu alionekana mwenye kisirani namimi au kama mtu aliyeudhiwa.

Siku ya kujifungua ilifika na kwa bahati nilijifungua salama mtoto wa kiume. Lahaula, ile rangi ya kijana ilitaka kunifanya nimtupe chini nilipomuona. Rangi yangu ni nyeupe kabisa, yani sio ya kuchakachua wala kutumia chochote. Mume wangu pia ana asili ya weupe, japo kwa ajili ya utu uzima rangi yake imefifia kidogo, lakini si mweusi. Lakini mwanangu alikuwa mweusi, yani mwenye rangi kama mtu mzima. Niliogopa sana, nikamkumbuka Severin, ambaye ni mweusi tii. Hospitali niliyojifungulia ilikuwa ya binafsi na hakukua na uwezekano wa kuchanganya watoto kwani ni hospitali makini pia isiyo na msongamano.

Michael alipokuja, alimchukua mtoto, lakini niliona kitu cha ajabu alipomshika mikononi. Mume wangu alianza kutoa machozi mtoto akiwa kiganjani mwake. Nilistuka mno, na kumuuliza kwa uwoga,”Michael vipi?”. Alinitizama, akanipa hongera na kumrudisha mtoto kitandani kwake. Nashukuru chumba nilicholala hakukuwa na mtu mwingine, kilikuwa cha mtu mmoja. Nilihisi tumbo la kuhara, nikajua kwa hakika Michael ameona kuwa yule si mwanae na ndio sababu ya kulia.

Siku mbili baadaye niliruhusiwa kurudi nyumbani, nikiwa na kichanga wangu ambaye anazidi kukolea rangi. Nilikuta mume wangu amefanya manunuzi ya vitu vingi mno vya mtoto, yaani kila kilichohitajika na zaidi. Siku tatu baada ya kurudi nyumbani, usiku tukiwa chumbani, mtoto akiwa amelala, Michael alianza kuzungumza nami kwa upole sana.

“Mke wangu, kuna mambo muhimu nahitaji tuongee usiku huu”. Hapo nilisikia moyo ukipasuka kwa hofu. Alinikazia macho na kuendelea,”Nimekuoa, sasa ni miaka sita. Kwenye maisha yangu haijawahi kutokea mwanamke niliyempenda kama wewe. Niliwahi kupenda mara mbili, nilikuhadithia, lakini mara zote niliumizwa, na hivyo sikutamani kuumizwa tena na mapenzi. Nilikupenda nikijua hunipendi lakini nilijipa moyo ulipokubali kuolena namimi kuwa ungekuwa mke bora na ungeniheshimu. Nimekupa uhuru na nimekuamini siku zote, lakini kuna kipimo zaidi cha uaminifu nilikiweka kwako. Najua nilifanya makosa kutokwambia ukweli huu mara nilipojua, lakini sikustahili kutendewa kitendo ulichonitendea.

Ulipoanza kuhitaji mtoto nilimuona rafiki yangu daktari ili aangalie uwezo wangu wa kuzaa kwani sijawahi kumpa msichana mimba. Kwa bahati mbaya sana, dokta Minja aliniambia sina uwezo kabisa wa kuzaa. Mbegu zangu ni chache mno, na nyepesi kiasi kwamba hakuna chakulaninachoweza kula kikanisaidia. Kama unakumbuka kuna siku nilikuja nyumbani nina mawazo sana, nimeshuka moyo, nikakaa kama siku mbili nikiwa hali hiyo. Lakini sikuweza kukujulisha ukweli huo kwani nilikuona una shauku kubwa ya kuzaa. Nilijaribu kutumia lugha za namna fulani kukuonesha kuwa maisha yanaweza kuendelea bila kuwa na watoto lakini hukutaka kusikia hiyo habari.

Niliamua sitakwambia ukweli, lakini nilipanga ikipita miaka mitano ya ndoa yetu nitafanya mpango twende Uingereza au nchi yotote Ughaibuni, huko ndio ningekwambia na pia tungetafuta namna nyingine kwa kutumia teknolojia za wenzetu. Nikiwa kwenye mipango, karibu na kukamilisha, ndipo ulipopata ujauzito. Tangu siku ile, moyo wangu umepigwa na mkuki mzito. Ni kama umeshindwa kupenyeza kwenye kipimo changu cha uaminifu. Najua huyu kijana si wangu, ni wa mwanaume mwingine. Nilisubiri nithibitishe hilo baada ya kuzaliwa kwake, na nilijiahidi nitapima vinasaba, lakini wewe mwenyewe unaona hamna haja ya kufanya hivyo kwani hata sura na rangi vinaonesha”.

Michael aliongea huku machozi yakimtoka. Wakati huo mimi niliweka mikono kichwani nikimsikiliza, na kutamani niwe naota. Nilikumbuka wakati nabeba ujauzito, uhusiano wangu na Severin ulikuwa umeshamiri, japo pia tulishiriki na mume wangu mara kwa mara. Nilitamani nimdanganye Michael, lakini angepima vinasaba na hali ingekuwa mbaya zaidi. Nilijilaumu mno, sana yani. Hapa ninapoandika, sina ndoa tena. Naishi maisha ya shida kiuchumi. Severin alishaoa na hakuhitaji tena kusikia toka kwangu. Mume wangu naye hataki kunisikia, japo bado hajaoa. Kama kuna upumbavu niliwahi kuufanya kwenye maisha yangu ni wa kumsaliti mwanaume ambaye alinipenda kwa moyo wake wote. Simlaumu kwa kushindwa kunisamehe, japo nilimuomba sana msamaha. Hivi karibuni walau ameanza walau kujibu jumbe zangu za simu ingawa kwa kifupi, japo simu zangu bado hataki kupokea. Kama ningepewa nafasi nyingine ya kuwa mke wa Michael Kalinye Nguzye, naahidi kuwa mke bora maisha yake yote. Kama barua hii itamfikia, basi iwe ni njia sahihi kumuonesha ni kiasi gani najutia kosa langu.

MIAKA MITANO BAADAYE

Nimekaa kimya, nikatulia kwanza nisimsumbue Michael kwa muda mrefu, tangu nilipotuma ile barua karibu mwaka mzima ukapita. Nikiwa na kijana wangu, maisha yametubadilikia sana huku sina tumaini lolote zaidi ya kuhangaika na shughuli za hapa na pale kujiweka bize na kupata pesa. Nilirudi nyumbani, wazazi wakanilaumu sana kwa kuikosea heshima ndoa yangu, lakini baadae wakanisamehe, si unajua tena mtoto akinyea mkono, huukati.

Siku moja nikiwa sina hili wala lile, nimekata kabisa tamaa kabisa ya kurudiana na mume wangu, nikapokea simu ya rafiki yake mmoja. Kusema kweli, nilipokosana na Michael, marafiki zake wote walikata kabisa mawasiliano na mimi. Hata ambao nilijaribu kuwatafuta ili waniombee msamaha, baada ya kujua, hawakuendelea kuwasiliana tena na mimi, walinikatia. Sasa siku hiyo nikashangaa sana kupokea simu ya shemeji yangu huyo, Hamza, waliyefanya naye biashara kwa muda mrefu hivyo kuwa marafiki wa karibu sana. Nilipopokea simu, aliongea na mimi kama mtu mwenye hofu kubwa, akasema Michael amepata ajali mbaya ya gari na wakati huo yuko hospitali ya Kabanga wilayani Kasulu. Nilistuka sana, nikamuuliza hali yake ambayo niliambiwa si nzuri hata kidogo.

Niliishi Kigoma mjini, umbali wa zaidi ya nzima kutoka Kasulu. Niliaga nyumbani kwa haraka sana, nikatafuta gari kuelekea huko. Nilimkuta mume wangu amelala, hajitambui, ameumia kwa ndani. Daktari alisema madhara ya ajali ile yanaweza yakawa makubwa hasa kichwani, ingawa kuna matumaini makubwa ya kupona. Siku hiyo hakuamka, wala kesho yake, mpaka baada ya siku tatu. Aliamka na kujitambua, lakini hakuweza kusogeza miguu yake. Ilionekana kuna mishipa ya kichwa imeumia ambayo imemsababishia kupooza miguu. Sitasahau jinsi alivyolia alipogundua kuwa hataweza kutembea tena. Moyo uliniuma sana, nikamuangalia Michael wangu, mwanaume mtanashati, aliyefanya shughuli zake kwa nguvu na jitihada nyingi, kwa sasa alilala tu kitandani akisubiri kuhudumiwa kwa kila kitu.

Nilijisikia vibaya sana, licha ya kuwa sikuwa nimepata msamaha wake. Moyo wake mzuri na tabia yake njema, haikumstahili kupata mateso hayo. Nafsini niliona kuwa hii ni fursa ya kumuonesha bado nampenda. Nilikusudia kumuhudumia, hata kama hangenisamehe kama angekuja kupona. Niliomba niende naye nyumbani kwake kwa ajili ya kumuhudumia, akakataa. Alidai kuwa atakuwa mzigo kwangu, jambo ambalo hataki. Alirudi nyumbani lakini nafsi yangu haikupata amani hivyo nilimtembelea kwake kila siku, kwani sote tuliishi Kigoma mjini.

Baada ya kuwa naenda kwake, kumuhudumia, kwa muda wa wiki moja, nilimuomba tena nihamie pale ili iwe rahisi kumuhudumia. Pale kwake aliishi na kijana wa kiume aliyemsaidia kazi na kumuhudumia, lakini nikiwepo nilihakikisha namfanyia Michael kila kitu. Alipojaribu kukataa sana, huku akiona kama ananitesa, kuna siku nilianza kumwambia jinsi nilivyo tayari kumuhudumia. “Umeishi na mimi vizuri sana Michael. Najua kosa nililokutenda, ilikuwa ngumu kunisamehe, na wala sikulaumu kwa hilo. Lakini huu ni wakati wangu wa kurekebisha kosa langu, na kukufanya unisamehe tena. Nia yangu si kurudi kuwa mke wako, japo niko tayari kwa hilo hata ukiwa katika hali hii, lakini nataka nafasi kukuonesha kwamba moyo wangu unashukuru kwa upendo ulionionyesha. Na hata nilipokukosea uaminifu, haukunifukuza kama mbwa wala kunichukia. Naomba uwe na amani mimi kukuhudumia, mpaka pale utakapopona, kwani naamini kuna siku utakuwa mzima tena.”

Nikiongea hivyo, Michael alilia sana. Akanyoosha mkono wake, akanivuta karibu naye aliyekuwa amelala kitandani. “Nashukuru sana mke wangu. Sina tena ujasiri wa kuendelea kukusukumia mbali. Nimeona ni kiasi gani ulijutia kosa lako. Kipindi nakuacha nilitaka nikupe kiasi cha fedha ili usipate shida ya maisha, lakini badae niliamua nikuache kwanza ujutie kosa lako na kujifunza. Ukweli ni kwamba sikuwa na mpango wa kukusamehe kabisa, ila nilipanga nikutafute nikusaidie kimaisha. Nilipopata ajali, mtu wa kwanza kumfikiria ni wewe Jovina wangu. Siwezi kukudanganya, nilifurahi sana ulipokuja na hasa ulipokuwa tayari kunihudumia, lakini nilikuonea huruma na aibu pia kwani sikukubali msamaha wako.

Nakupenda sana Jovina, sijawahi kupenda mwanamke mwingine yeyote zaidi yako, na sidhani kama naweza kupenda tena. Kama uko tayari tuendelee kuishi, hapa ni kwako mama, umlete na kijana wetu, nitafanya taratibu atatumia jina langu na atakua mwanangu.”

Maneno ya Michael yalinitoa machozi na kunifanya nijihisi kama nimetua mzigo mkubwa sana. Niliuhitaji msamaha wake kwa muda mrefu na sasa ombi langu lilikuwa linajibiwa. Nilimshukuru sana na kumuahidi kumpenda kwa moyo wote. Kipindi tuko mbali, niligundua kuwa nampenda mume wangu, wala sikuwahi kutamani kuwa tena na Severin, kiasi cha kutomtafuta hata kumpa habari za mwanae. Kwangu alikuwa kama matapishi niliyoyatoa, sikumtaka tena. Michael aliniuliza habari za mtoto siku za mwanzo nilizoanza kumuhudumia, nikamueleza kuwa hata baba yake hatujawahi kuwasiliana naye.

Nashukuru sana, baada ya matibabu, mazoezi ya kila siku na ushauri wa kisaikolojia, mwaka jana Michael ameanza kutembea, japo kwa taabu kidogo. Siku zinavyoendelea mume wangu anazidi kupona, miguu yake ikiendelea kupata nguvu. Naamini atapona kabisa. Mapenzi kati yetu yameanza kwa upya, huku tukimlea mtoto wetu kwa furaha ambaye ameanza shule na anatumia jina la Michael kama baba yake. Ndoa yangu imekuwa na amani na furaha kuliko ilivyokuwa mwanzo. Kitendo cha mume wangu kunipa nafasi nyingine, nafasi ya kuonesha kuwa mke sahihi kwake, kimenifunza mengi mno na kamwe sitaichezea ndoa yangu kwani nimejua mume mzuri niliyenaye. Natumai wanandoa wenzangu, na wale wanaotarajia kuwa kwenye ndoa, mtajifunza kutokana na kosa langu jinsi gani uaminifu ni muhimu mno kwa ndoa. Unapoamua kuoa au kuolewa, fanya maamuzi ya kuachana na nyuma yako. Uaminifu ni nguzo muhimu mno kwa ndoa yenye furaha.

MTUNZI NA MWANDISHI: Grace G.R

…………………………MWISHO…………

Comments