Mwandishi wa tamthilia Eve Ensler , alikuwa maarufu miaka ya 1990 na kitabu chake cha Vagina Monologues.
Tamthilia hii inaeleza simulizi za wanawake kuhusu kudhalilishwa kingono zilizotolewa kwenye zaidi ya nchi 140.
Kila mahali tamthilia hii ilipotolewa iliwafanya watu wafurahi na wengine kudondosha machozi.
Kazi yake ya simulizi ya kitabu kipya, simulizi ya kubuni The Apology iliyoandikwa mithili ya barua iliyotumwa kwake kutoka kwa baba yake, akiomba radhi kwa namna alivyomdhalilisha kingono wakati wote wa utoto wake tangu akiwa na miaka mitano.Baba yake hakuwahi kumuomba radhi binti yake- na kwa miaka mingi baada ya kifo chake, Ensler akaamua kuomba radhi kwa niaba ya baba yake.
Mwandishi, ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za wanawake, alizungumza na BBC kuhusu athari za udhalilishaji aliofanyiwa.
Anasema kabla ya hayo alikuwa mwenye furaha. Anakumbuka kuwa alikuwa akimpenda sana baba yake, lakini mambo yalibadilikaje?
Anasema: ''Pamoja na kuwa hivyo mwanzoni sikuelewa nini kinaendelea, nilijua kuna kitu hakiko sawa''.
''Vitu vilikuwa vinatokea kwenye mwili wangu, na sikutaka vitokee. Na alikuwa baba yangu, mtu ambaye nilikuwa nampenda kuliko kitu chochote duniani.''
''Wakati hali hiyo ikiendelea baadae nikajua kuwa ni jambo ambalo sikulitaka, nilijisikia niliyeingiliwa. Ilitia kinyaa''.
Na nikaanza kuona namna gani mapenzi yasiyo ya kawaida aliyokuwa akionyesha kwangu yakampumbaza kila mtu kwenye familia kushindwa kuuona ukweli.
Ilianza kubadilika -nilipokumbuka kwa uwazi kabisa- usiku ambao nilifanya jambo kuepuka kudhalilishwa, kwa hakika nilijifanya nimekufa.Nilijifanya sikuwa hapa.
Aliacha usiku huo. Hali iliishia hapo kuhusu kunidhalilisha kingono. Nilikuwa na umri wa miaka 10.
Mapenzi yasiyo ya kawaida ya baba yake kwake yalikuwa wazi kwa kila mtu kwenye familia. Dada na Kaka yake hawakufahamu aina ya mapenzi aliyokuwa nayo kwake lakini mama yake alikuwa akihisi.
Miaka kadhaa baadae, mama yake alimwambia kuwa alijua udhalilishaji aliokuwa akiupitia.
Lakini baadae alimwambia kwamba kuna ishara nyingi alizoziona.Alimwambia alikuwa akiugua maradhi ya maambukizi, ndoto, na pia mabadiliko ya tabia na hisia.
Kisha mama yake akaanza kukumbuka vitu, kwa mfano wakati fulani mjomba wake alimwambia kuwa anafikiri baba yake alikuwa akimtilia maanani sana.
Ensler anasema alikuwa na ndugu zake na walezi wake waliokuwa wakimtunza ambao walimpenda sana. Na anafikiri kuwa ndio waliookoa maisha yake.
Kupigwa
Baba yake aliacha kumdhalilisha kingono, lakini akaanza kumpiga tena alikuwa akimpiga vibaya sana.
''Tunawafahamu vizuri wanaotunyanyasa, ninaweza kukumbuka baba yangu alikuwa akiniita nikiwa juu nilikuwa ninajua kwa kusikia sauti tu kuwa ni kwa kiasi gani nitapokea kipigo.
''Nilikuwa ninajitazama kwenye kioo , na nikajisemea kwa sauti: ''Utaondoka sasa hivi. Hautakuwa hapa. Hutajisikia chochote, hutahisi chochote atakachokufanyia''.
Njia hii ilimsaidia sana.kwa aliyoyapitia hakuona kama alikuwa na thamani ya kupendwa na mtu yeyote.
Msamaha
Je, ukiwa mtoto ulipenda baba yako aseme samahani? Ensler aliulizwa na BBC
''Mimi ndiye niliyekuwa nasema samahani wakati wote na kwa sababu moja, alikuwa ananifanya nijione mkosaji wakati wote. Jina langu la kati kati lilikuwa ''Samahani''.
Akili yangu ilikuwa ikiniambia kuwa kama nitasema samahani kila mara, naye atasema pia.
Anasema alifikiri hali hiyo pia itamuondoa kwenye hali ya kujisikia kuwa yeye ndio mbaya zaidi kila mara.
Baba yake Ensler hakuwahi kumwambia 'samahani' kwa kuwa kwa mujibu wa Ensler baba yake alizaliwa kwenye miaka ambayo wanaume walikuwa hawakosei. ''Baba yangu alikuwa mtendaji mkuu wa Kampuni -alikuwa mtendaji mkuu wa familia, alikuwa sawa kwa kila jambo na kila hali''.
Jambo la kutokubaliana na Baba ilikuwa kosa lenye kustahili adhabu.Alikuwa anakuchapa kibao cha uso.
Kifo
Baba yake Ensler alikuwa mgonjwa kwa muda kabla ya kifo chake. Alikuwa na saratani ya mapafu lakini si baba yake wala mama aliyempa taarifa kuwa anakufa.
Ilikuwa siku chache baada ya kifo chake alipigiwa simu. ''kuna kitu unahisi kama hujawa karibu wala kuwa na uwezo wa kusema kwaheri''.
''Nilijisikia vibaya sana nilijihisi ganzi''. Alisema Ensler.
Sikuwa na hasira
Ensler anasema hakuwa na hasira na ilimchukua miaka kadhaa kujua ukubwa wa udhalimu aliofanyiwa.
''Nilikumbuka niliwahi kuwasimulia vichekesho marafiki zangu kuhusu baba yangu nikiwa chuoni nikawaambia aliwahi kunipiga kisha akamfokea mama yangu aende jikoni akachukue kisu anichome.''
''Hakwenda popote kisha akamwambia tena. Mama aliondoka chumbani. Lakini bahati mbaya hakurudi tena''.
''Lakini nakumbuka nikiwa na miaka 20 niliwasimulia marafiki zangu huku nikicheka nao wakapigwa na bumbuwazi kuwa: ''umesemaje?''
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Ensler kupata mrejesho kutoka kwa ulimwengu kuwa mambo aliyoyapitia yalikuwa mabaya mno.Hali hiyo ilimuogopesha.
Ensler anasema kitabu chake cha The apology ni tiba tosha, aliweza kumwelezea baba yake kuanzia kwenye hali yake ya ukatili mpaka kwenye kuomba msamaha. Kutoka kwenye ubabe mpaka kuwa katika hali ya kutojiweza. ''Kubwa zaidi ni kuwa baada ya kuandika kitabu hiki nimehisi maumivu, chuki dhidi yake vimekwisha kabisa
Comments
Post a Comment