Taasisi kumi za usalama wa taifa zenye nguvu zaidi duniani

 



Katika dunia ya leo mataifa hayategemei tu majeshi ya nchi peke yake bali pia taasisi za kiintelijensia zinazosimamia usalama wa taifa na kulilinda dhidi ya vitisho vya ndani na nje ya nchi. Kwa kawaida taasisi hizi huwa na ufahamu mpana wa tabia na mienendo ya watu, viongozi na mataifa jirani. Ufahamu huu ambao hutokana na kukusanya taarifa, kuzichambua na kuzipa taasisi nyingine za serikali ili zifanyiwe kazi, huzifanya taasisi za usalama wa taifa za nchi mbalimbali kuogopwa sana ndani na nje ya nchi. Umahiri wa kufanya kazi wa taasisi hizi ndio hufanya taasisi ya usalama wa taifa fulani kuwa ya kuogopwa na bora zaidi kuliko ya taifa jingine.

Hapa chini ni orodha ya taasisi kumi za usalama wa taifa ambazo ni bora na zinazoogopwa zaidi duniani.

1. ISI (Inter-Services Intelligence), Pakistan


Makao Makuu: Islamabad, Pakistan

Kuanzishwa: 1948

ISI ndiyo taasisi inayosimamia usalama wa taifa la Pakistan. Taasisi hii ina nguvu kubwa sana kiasi kwamba kiuhalisia ndiyo hasa inayoongoza nchi ikishirikiana na Jeshi la Pakistan. Katika chambuzi nyingi za kiusalama ISI inatajwa kuwa ndiyo taasisi nguli zaidi ya Usalama wa Taifa ulimwenguni.

Toka kuanzishwa kwake ISI imekuwa mhimili wa serikali zote zilizowahi kuiongoza Pakistan. Kushindwa vita kwa iliyokuwa Jamhuri ya Soviet (sasa Urusi) dhidi ya Afghanistan ni mojawapo ya mafanikio makubwa katika historia ya ISI, ambapo kwa kiasi kikubwa Pakistan iliisaidia Afghanistan.

2. Mossad (HaMossad leModiʿin uleTafkidim Meyuḥadim), Israel

Makao Makuu: Tel Aviv, Israel

Kuanzishwa: 1949

Mossad inachukuliwa kama baba wa taasisi za usalama wa taifa duniani. Taasisi hiyo imekuwa sehemu ya kazi ngumu na za kutisha zaidi katika nyanja ya usalama wa nchi, yumkini kuliko taasisi nyingi za aina yake duniani. Inaaminika kuwa kama sio kazi nzuri ya Mossad huenda taifa la Israel lingeshaangamizwa na maadui zake siku nyingi.

Mojawapo ya kazi mashuhuri ya Mossad inayokumbukwa ni Oparesheni Thunderbolt. Oparesheni hiyo iliyofanyika Jumapili ya Julai 4 mwaka 1976, ilikuwa ya uokozi wa mateka wa Israel katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe Uganda, enzi za utawala wa Idi Amin.

Katika kuiandaa oparesheni hiyo, wana usalama hao wa Israel walitengeneza msafara wa magari kufanana kabisa na msafara wa Idi Amin na kufanikiwa kuingia uwanja huo wa ndege, kuokoa mateka na kulipua ndege za Jeshi la Uganda.

Oparesheni yao nyingine mashuhuri ni Wrath of God au kwa Kiswahili kisicho rasmi, Oparesheni Hasira ya Mungu. Oparesheni hii ilifanyika baada ya tukio la kuuawa kwa wanariadha 11 wa Israel kwenye michezo ya Olimpiki jijini Munich mwaka 1972. Shambulio hilo dhidi ya wanariadha wa Israel lilifanywa na kundi la Kigaidi la Kipalestina la Black September. Mara tu baada ya tukio hilo, Mossad iliapa kulipa kisasi na kutumia waajiriwa wake maeneo mbalimbali duniani kuwatafuta wote walioshiriki kuua, kufadhili na kuratibu tukio hilo na kuwaua mmoja baada ya mwingine mpaka walipomalizika, kazi ambayo inaaminiwa ilichukua zaidi ya miaka 20.

3. CIA (Central Intelligence Agency), Marekani


Makao Makuu: Fairfax, Virginia, Marekani

Kuanzishwa: 1947

CIA inafahamika kuwa ndiyo taasisi ya usalama wa taifa ambayo imeipa Marekani nguvu iliyo nayo duniani. Taasisi hii hufanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa Marekani inabaki kuwa taifa lenye nguvu na ushawishi ulimwenguni.

Moja ya oparesheni mashuhuri za CIA ni Opareshi PBSUCCESS, ambapo kati ya Juni 18 hadi Julai 27 mwaka 1954, waasi waliokuwa wakifadhiliwa na Marekani waliipindua serikali ya Rais Jacobo Abernz iliyochaguliwa na wananchi Kidemokrasia nchini Guatemala. Oparesheni nyingine ni Oparesheni Geronimo ambapo kiongozi wa Al Qaeda Osama bin Laden aliuawa nchini Pakistan mwezi Mei mwaka 2011.

4. MI6 (Military Intelligence, Section 6), Uingereza

Makao Makuu: London, Uingereza

Kuanzishwa: 1909

MI6 ni moja ya taasisi kongwe zaidi za usalama wa taifa duniani. Taasisi hii ilianza kazi zake hata kabla ya Vita ya Kwanza ya Duni (WWI). Inasadikiwa kuwa taasisi hii ndiyo siri ya ushindi wa Uingereza katika vita mbalimbali ambazo imeshiriki duniani. MI6 ndiyo taasisi iliyoisaida Uingereza kuepuka mkono wa Hitler na pia kumshinda Hitler.

5. GRU (Main Intelligence Agency), Urusi


Makao Makuu: Moscow, Urusi

Kuanzishwa: 1918

Hii ndiyo taasisi kuu ya Usalama wa Taifa ya Urusi. Kabla ya anguko la Umoja wa Soviet (USSR) taasisi ya Usalama wa Taifa ya Urusi iliitwa KGB. GRU imeundwa kama kitengo cha kijeshi kinachoshughulika na ujasusi dhidi ya mataifa ya kigeni. Inaaminika kuwa baada ya anguko la USSR, GRU ndiyo imeisaidia Urusi kuweza kusimama imara mpaka kufikia kuwa taifa kubwa linaloogopwa duniani hii leo.

6. MSS (Ministry of State Security/Wizara ya Ulinzi wa Taifa), China


Makao Makuu: Beijing

Kuanzishwa: 1983

MSS ndiye msimamizi wa usalama na intelijensia ya China. Inafanya kazi zote mbili za kutazama intelijensia ndani na nje ya mipaka ya China. Mbali na kazi yake ya kuilinda China na maadui wa nje pia inakisaidia Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) kuweza kutawala na kuongoza vizuri taifa hilo lenye wakazi zaidi ya bilioni moja.

7. RAW (Research and Analysis Wing), India


Makao Makuu: New Delhi

Kuanzishwa: 1968

Kwa kiasi kikubwa RAW inajisghulisha na ujasusi wa nchi za nje na matishio ya kiusalama ya India kutoka nje ya India huku taasisi ya IB ikishughulika na usalama wa ndani ya nchi. Moja ya kazi zake kubwa ni kutazama nyendo za majirani zake wakubwa hasa China na Pakistan.

8. BND ( Bundesnachrichtendienst), Ujerumani


Makao Makuu: Berlin

Kuanzishwa: 1956

Ukitazama teknolojia, BND inakwenda sambamba na CIA ya Marekani, Mossad ya Israel na MSS ya China. Hata hivyo mitambo ya BND ya kufanya ujasusi wa vifaa vya elektroniki inaaminika ndio bora zaidi duniani. BND pia inaongoza kwa kukusanya taarifa nyeti za kiusalama za eneo la Mashariki ya Kati na Amerika ya Kusini na husaidia taasisi nyingine duniani wanapohitaji taarifa hizo.

9. DGSE (General Directorate for External Security), Ufaransa


Makao Makuu: Paris

Kuanzishwa: 1982

Kama zilivyo taasisi nyingi za kijasusi hili linajishughulisha na usalama wa Ufaransa dhidi ya matishio ya kiusalama toka nje. Japo halina miaka mingi ukilinganisha na mashirika mengine ya kijasusi bado linaelezwa kuwa ni moja ya mashirika bora zaidi duniani.

10. ASIS ( Australian Secret Intelligence Service), Australia


Makao Makuu: Canberra

Kuanzishwa: 1952

Japo Australia haijaathiriwa na matatizo mengi ya usalama ya kimataifa lakini imejizatiti kwenye masuala ya usalama na ujasusi. ASIS ni moja ya mashirika imara zaidi ya kijasusi duniani na ni mdau mkubwa wa kiusalama wa eneo la Asia na Pasifiki.

Majasusi wa ASIS wametapakaa kote duniani na wanakusanya taarifa muhimu za kiusalama maeneo mengi. ASIS imekuwa ikifanya kazi zake kwa usiri mkubwa miaka mingi kiasi kwamba wako watu ndani ya Australia ambao hawakuwa wakiifahamu mpaka ilipotajwa Bungeni mwaka 1977.

Kwa hiyo usiku wa leo ukiingia kulala kwa amani na kuamka mambo yote yakaenda sawa bila matishio makubwa kama ugaidi na nchi kuvamiwa na uhalifu mkubwa wa hapa na pale basi jua kuwa yako mashirika kama hayo sehemu mbalimbali duniani ambayo yanafanya kazi, wakati mwingine kwa kushirikiana ili kufanya maishi yaende kwa usalama

Comments