USHUHUDA WA KWELI WA KICHAWI A:22-24
USHUHUDA WA KWELI WA KICHAWI A-22
Wakati nikiishi mkoani Mwanza, alikokuwa anafanyia kazi Mzee wangu, na nikiwa na miaka 11 tu, kuna siku wazazi wangu wakiwa wamelala huku wamefunga milango na madirisha yote, walikuja kugutuka kutoka usingizini mishale ya saa 9 usiku na kukuta madirisha yote ya chumbani kwao na mlango yamefunguliwa. Na kwavile kulikuwa na mbalamwezi, waliweza kuwaona bundi 4 wamesimama katika madirisha 2 ya chumbani huku wakiwatazama wazazi wangu waliolala kitandani. Baba alivaa ujasiri wa kuwatimua, ila baada ya kuamka watu 4 ndani ya familia tuliamka tukiwa tumechanjwa chale mwili mzima. Ilibidi familia iingie 'gereji' ndo mambo yakawa shwari.
USHUHUDA WA KWELI WA KICHAWI A-23
.Mwaka 1993 tukiwa tulipanga nyumba moja kule Tandika Mabatini, Dar es Salaam. Mwenye nyumba alitupa masharti kadhaa, kubwa kabisa likiwa ni katazo la kuingia nyumbani baada ya saa 6 usiku, au kwenda chooni/bafuni baada ya masaa hayo. Tulijitahidi kutii! Siku moja, mpangaji mwenzetu mmoja alikiuka masharti akaenda msalani saa 6 na ushee, tulisikia kelele za kuomba msaada, lakini hakuna aliyethubutu kwenda kutoa msaada. Kesho yake alfajiri tulimkuta jamaa bado ameanguka chooni. Mwenye nyumba alimfokea kwa 'kuyataka mwenyewe'. Ilibidi jamaa ahame nyumba baada ya siku 4. Ilikuja kubainika kuwa, Mwenye nyumba alikuwa anafuga majini na huwa anayafungulia masaa hayo yanaingia kazini, hivyo jamaa alikumbana nayo yakamshughulikia. Sisi nasi kwa uoga ilibidi tuhame kabla kodi yetu haijaisha..Muda haunitoshi kusimulia nilivyokutana na wachawi ' live' mara mbili, wakati nikiishi huko Kanda ya Ziwa.
USHUHUDA WA KWELI WA KICHAWI A-24
Miaka kadhaa nyuma, bibi yangu mzaa mama, katika umri wake wa makamo, mrembo na mwenye kinywa kilichosheheni meno imara na meupeeee, aliamka asubuhi moja tusiyoisahau mpaka leo, kinywani akiwa hana jino hata moja. Alikuwa kibogoyo kabisa kama alizaliwa na kukua bila meno.
Wakati ukoo mzima tumetunduwaa kwa mshangao, jamii ilitutuliza kwa kutuambia kuwa tuwe wapole na habari ndiyo ilikuwa imekwisha hivyo. Kuwa bibi yangu eti alifanya uzembe wa kuamka na kupiga kelele akidai meno yake hayamo kinywani.
Kumbe ilimpasa, baada ya kuona kinywa chake kitupu, angerudi kimya kimya kulala. Meno yake yangerejeshwa na walioyaazima kwenda kutafunia nyama na bisi!! Ni juzi tu tumemzika bibi yetu akiwa kibogoyo kwa miaka kibao, kwani meno hakurejeshewa tena. Uchawi wa migombani Unyakyusa huu!!
FUATILIA MUENDELEZO WA VISA HIVI A:1-30, B:1-30, C:1-30
Comments
Post a Comment