Skip to main content

VCCM: Kama kuna mahali tuliwakwaza tunaomba radhi


   
 
 
UVCCM pc

Mwenyekiti wa umoja huyo Taifa, Kheri James



Dar es Salaam. Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umeomba radhi iwapo kuna mahali walitofautiana kimtazamo na makundi mengine na kutaka vijana wengi kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika majukumu yake ya kuiongoza nchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana Jumapili Machi 28, 2021 na mwenyekiti wa umoja huyo Taifa, Kheri James wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma akibainisha kuwa huu ni wakati wa kusamehe ya nyuma na kufungua ukurasa mpya wenye mambo yatakayokuwa na tija kwa Taifa.

“Inawezekana katika siasa zetu na hekaheka za kutofautiana kimitazamo yapo mambo ambayo huko nyuma yalipelekea umoja wetu ukatetereka, sisi kama umoja wa vijana hatuoni aibu kusema tunaomba radhi kwa hayo kama tuliyatenda na tupo tayari kuyarekebisha ili kutengeneza jukwaa safi kwa rais wetu kuanza upya akiwa na watu walioshikamana ili nchi yetu iweze kwenda mbele.”

“Vijana wa nchi hii ndio watakuwa wanufaika wa kwanza Serikali ikiwa imara na vijana wa nchi hii ndio watakaokuwa wahanga wakubwa nchi ikiwa dhaifu.”

“Kwa hiyo ninasisitiza vijana tunahakikisha maneno na matendo yetu yanafanana na dhamira ya rais wetu ili kumrahisishia kazi yake mpya aliyopewa ya kutuongoza kama mkuu wa nchi ili sisi tuwe ni nguzo ya umoja, mshikamano na maendeleo ya nchi yetu,” amesema James

Comments